Serikali yatoa ubani wa Sh1 milioni kwa wafiwa ajali ya ndege

Muktasari:

  • Serikali imetoa ubani wa Sh1 milioni kwa kila familia ya watu 19 waliofariki katika ajali ya ndege iliyotokea jana mjini Bukoba.

Mwanza. Serikali imetoa ubani wa Sh1 milioni kwa kila familia ya watu 19 waliofariki katika ajali ya ndege iliyotokea jana mjini Bukoba.


Pamoja na ubani huo, Serikali pia italipia gharama zote za mazishi za watu hao wanaotarajiwa kuzikwa maeneo mbalimbali nchini kulingana na maamuzi ya familia.


Akizungumza leo Jumatatu Novemba 7, wakati wa ibada maalum ya kutoa heshima za mwisho kwa watu 19 waliofariki katika ajali hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa husika kusimamia utekelezaji wa agizo la kugharamia mazishi.


Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila aliueleza umma kuwa Serikali imetoa ubani ya Sh1 milioni kwa kila familia kusaidia shughuli za msiba.

Miili 19 ya waliofariki ajali ya ndege ikiagwa Kaitaba

Shughuli ya kuaga na kutoa heshima za mwisho zinaendelea katika uwanja wa Kaitaba kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za kifamilia.


Ajali hiyo iliyokea baada ya ndege kutwaa na kuzama ndani ya maji ya Ziwa Victoria, hatua chache kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba. Uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo unaendelea.