Serikali yawalipa wakulima Sh26 bilioni mauzo ya ufuta

Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Udinde Wilaya ya Songwe katika mkutano wa hadhara. Picha na Hawa Mathias.
Muktasari:
- Kilo 7.5 milioni za ufuta ziliuzwa na wakulima kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Katika msimu wa kilimo 2022/23 huku wakiwa wamelipwa zaidi ya Sh26 bilioni kati ya 28 bilioni zilizopatikana ikiwa ni awamu ya kwanza wakulima kuuza kwa mfumo tangu Serikali ilipoelekeza utaratibu kwa Wilaya ya Songwe.
Mbeya. Wakulima wa zao la Ufuta Wilaya ya Songwe, Mkoa wa Songwe wameanza kuona matunda ya kuuza mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani baada ya Serikali kuwalipa zaidi ya Sh26 bilioni kwa msimu wa kilimo 2022/23.
Akizungumza na wananchi leo Oktoba 9, 2023 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Udinde, Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo amesema mfumo huo ni rafiki kwa wakulima na kurejesha kicheko huku akisisitiza kujiunga kwenye Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos) ili kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha.
“Tumepigania kuanza kwa mfumo huu ambao baadhi yao walikuwa wakipinga, lakini sasa wamepokea mabilioni ya fedha ambazo zinasababisha kubadilisha maisha ikiwepo kusomesha watoto na kumudu gharama za mahitaji,”amesema.
Amesema wameweka mikakati ya kuwawezesha wakulima wa ufuta kupata mbegu bora za ufuta katika msimu ujao ili kuongeza tija na kuzalisha zaidi ya tani 7.5 milioni ambapo mahitaji huenda yakawa makubwa zaidi.
“Mfumo huo umekuwa rafiki kwa wakulima kwani masoko yapo ya uhakika na mbunge kwa kushirikiana na halmashauri tutaboresha kilimo hicho sambamba na kuhamasisha kujiunga na Amcos ili kuweza kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na wadau wa kilimo kwa kushirikiana na Serikali,”amesema.
Mulugo ametaja miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima kujua faida ya mfumo wa stakabadhi ghalani na kugawa bure mbegu bora za ufuta sambamba na kuboresha maghala ya kuhifadhia mazao ili kuwepo kwa maeneo salama ya kutunzia mara baada ya mavuno.
“Pia tunaendelea kuhamasisha wakulima kujiunga kwenye vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) ili kuweza kupata mikopo na kupanua wigo wa kuzalisha baada ya kuwepo kwa masoko ya ndani na nje ya nchi jambo litasaidia Serikali kupata mapato kupitia sekta ya kilimo,”amesema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songwe, Cecilia Kavishe kwa msimu huu wa kilimo 2022/23 halmashauri imeweza kuingiza mapato ya zaidi ya Sh799 milioni baada ya kuanza kuuza zao la ufuta kwa mfumo wa stakabadhi gharani.
“Kwa msimu huo huo wakulima wamelipwa Sh26 bilioni kati ya Sh28 bilioni na hakuna anayedai huku wakieleza kuona umuhimu wa kuuza kwa mfumo huo na kuacha kutegemea madalali ambao wamekuwa wakinunua kwa bei kandamizi,”amesema.
Kavishe amesema mfumo huo ulioelekezwa na Serikali ya awamu ya sita umekuwa rafiki kwani hata katika suala la ukusanyaji wa mapato wamekuwa hawatumii nguvu tofauti na miaka ya nyuma sambamba na wakulima kuonyesha furaha ya kuongeza uzalishaji katika msimu ujao wa 2023/24.
Mkulima wa ufuta Kijiji cha Udinde, Stella Mwanatwa amesema kuwa Serikali imefanya jambo jema kuja na mfumo huo kwani awali walikuwa wakilanguliwa na wanunuzi kwa madai ya kukosa ubora
“Tumenyonywa kipindi kirefu sasa imetosha tunamshukuru Mbunge wetu, Philipo Mulugo amekuwa akitupigania sana kwenye vikao vya Bunge sasa wanaona matunda kutokana na kulipwa kwa wakati na kuchangia kuanza maandalizi katika msimu ujao,”amesema.