Serikali yawaonya wakuu, wamiliki shule ambazo hazijafungwa

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi kuhusu shule ambazo bado hazijafunga. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali itawachukulia hatua wakuu wa shule au wamiliki wa shule binafsi watakaokaidi agizo la kuwaruhusu wanafunzi kwenda kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Mkazi.
Moshi. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali itawachukulia hatua wakuu wa shule au wamiliki wa shule binafsi watakaokaidi agizo la kuwaruhusu wanafunzi kwenda kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Mkazi.
Amesema wanazo taarifa za majina ya baadhi ya shule ambazo bado hazijafunga kwa ajili ya kuwaruhusu wanafunzi kushiriki Sensa itakayofanyika Jumanne Agosti 23 mwaka huu
Waziri Mkenda ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 21, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Amewaagiza wadhibiti ubora wa kanda hadi ngazi ya halmashauri kote nchini kutoa taarifa ya shule ambazo hazijafuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Wadhibiti ubora wote wa kanda hadi halmashauri watatupa taarifa ni shule ngapi ambazo hazijafuata meelekezo yaliyotolewa na Serikali na sisi tutachukua hatua kwa wenye shule na wakuu wa shule” amesema Profesa Mkenda
“Sekta binafsi tunapenda kufanya nao kazi lakini ni vizuri wakajaribu kuzingatia mantiki ya maelekezo ya Serikali, ukisema unafunga shule tarehe 22 yule mtoto kama ni wa Kagera au Ruvuma atafika lini nyumbani kwenda kuhesabiwa?” amehoji Profesa Mkenda
Amesema kuwa wanafunzi wanatakiwa wapate muda wa kutosha nyumbani huku akiagiza kuwa shule ambazo hazijafunga ziwaachie wanafunzi.
“Suala la wanafunzi kurudi nyumbani kwa ajili ya Sensa lazima iendane na mantiki yake kwamba wapate muda wakutosha nyumbani kwa ajili ya kushiriki Sensa, shule zote ambazo bado hazijawaachia wanafunzi zifanye hivyo mapema na wahakikishe muda wote wa sensa watoto wako nyumbani,”
"Sasa niombe shule zisiwe zinafanya kazi wakati wa kipindi cha Sensa na wale ambao wanataka kufunga shule siku moja tuu ya sensa kwa kweli wanatufanya tuanze kuamini kwamba kuruhusu "flexibility" wana "abuse" nafasi hiyo," amesema Profesa Mkenda