Serikali yawaonya walimu dhidi ya mikopo inayodhalilisha
Muktasari:
- Baadhi ya walimu wamedaiwa kukabidhi kadi zao za benki kwa wakopeshaji wasio rasmi, ambao hujikuta wakichukua mishahara yote kila mwezi, na kuwaacha katika hali ngumu ya maisha.
Arusha. Serikali imewaonya walimu nchini dhidi ya kukimbilia mikopo kutoka taasisi zisizo rasmi ambazo zimekuwa zikiwawekea masharti kandamizi, ikiwemo kutaka dhamana ya kadi za benki wanazolipwa mishahara, hali inayowadhalilisha na kushusha heshima ya taaluma yao.
Akizungumza katika kongamano la walimu 220 kutoka shule mbalimbali za Wilaya ya Karatu lililoandaliwa na Benki ya NMB, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Juma Hokororo amesema baadhi ya walimu wamejikuta wakikumbwa na msongo wa mawazo na matatizo ya kifedha kutokana na mikopo hiyo.
“Kuweni na nidhamu kwenye mikopo mnayochukua, mingine mnachukua mitaani, mnapewa masharti ya kudhalilisha, kushusha utu wenu, na bado mnakubali kwa sababu ya shida ya fedha, mwisho wa siku hamwezi hata kulipa na mnaingia kwenye matatizo makubwa ya kifedha,” amesema Hokororo.
Amesema kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakikabidhi kadi zao za benki kwa wakopeshaji wasio rasmi, ambao hujikuta wakichukua mishahara yote ya walimu kila mwezi, na kuwaacha katika hali ngumu ya maisha.
“Mikopo hiyo haiwezi kuwasaidia kujenga uchumi wenu, hakikisheni mnachukua mikopo kutoka taasisi rasmi zenye masharti nafuu na ya haki.”
“Hakuna fedha inayotosha kutoka kwenye chanzo kimoja bali wekezeni pia, kama unataka kufuga, kulima au kufungua biashara fanya hivyo sasa hivi maana ndio itakayoweza kukusaidia kujikwamua kiuchumi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Idara ya wateja binafsi kutoka makao makuu ya Benki ya NMB, Ally Ngingite amesema kongamano hilo linalojulikana kama ‘Mwalimu Spesho’ imekuwa ikitolewa kwa zaidi ya muongo mmoja na tayari limewanufaisha zaidi ya walimu 120,000 kote nchini.
“Kupitia ‘Mwalimu Spesho’ tunatoa elimu ya nidhamu ya kifedha, uwekezaji, afya ya akili, mikopo yenye masharti nafuu, na maandalizi ya maisha ya kustaafu,” amesema Ngingite.
Amesema elimu hiyo inalenga kuwawezesha walimu kuwa na maarifa ya kufanya maamuzi sahihi ya kifedha kwa ajili ya ustawi wao wa sasa na maisha ya baada ya kustaafu.
Mmoja wa walimu waliohudhuria kongamano hilo, Matilda Mathias kutoka Shule ya Sekondari Karatu, amesema elimu waliyoipata ni mkombozi mkubwa kwa walimu wengi wanaokumbwa na changamoto za kifedha kutokana na mikopo isiyo rasmi.
“Walimu ndio waathirika wakubwa wa mikopo ya mitaani, wengi wetu hatuna elimu ya kifedha, hivyo tunaishukuru NMB kwa kutufikia na kutupa mbinu za kujikwamua kiuchumi,” amesema.