Sh1.8 bilioni zakabidhiwa vikundi 131, vijana watajwa kukwepa kulipa

Muktasari:
- Hundi hiyo imekabidhiwa leo Ijumaa Mei 23, 2025, na Mbunge wa Lupa Wilaya ya Chunya, Masache Kasaka.
Chunya. Halmashauri ya Wilaya la Chunya Mkoa wa Mbeya imekabidhi hundi ya Sh1.8 bilioni kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi 131, huku vikundi vinne vikigomea kupokea mkopo huo wa asilimia 10 kwa madai kiwango ni kidogo.
Vijana wametajwa kuwa vinara kukwepa kurejesha mikopo hiyo, hatua ambayo imetajwa kukwamisha utoaji wa mikopo kwa makundi mengine kwa wakati, licha ya Serikali ya kuzitaka halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 za mapato ya ndani kutoa mikopo kwa makundi hayo.
Mkopo huo umekabidhiwa na Mbunge wa Lupa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Masache Kasaka, Mei 23,2025 katika hafla fupi iliyo fanyika katika ukumbi wa Sapanjo, huku akionya walengwa kutokuwa kikwazo.
Masache amesema lengo la Serikali kutoa mikopo ni kuwekeza makundi ya vijana kuanzisha miradi ya kujikimu kiuchumi na kurejesha kwa wakati.
"Serikali itaendelea kutoa mikopo asilimia 10, hivyo ni vyema walengwa kuwa waaminifu kurejesha ili kuwezesha Halmashauri kutoa kwa vikundi vingine, vyenye uhitaji," amesema Masache.
Amesema serikali imetekeleza takwa la kisheria ambalo linaenda kukuza uchumi wa wananchi wa Chunya kuanzisha miradi kupitia mikopo hiyo.
"Tumesikia maombi ya vikundi yalikuwa mengi ambayo yalifika zaidi ya Sh5 bilioni, lakini pia tumeelezwa kipindi kilichopita halmashauri ilitoa mkopo wa 2.7 bilioni kati ya hizo Sh 1.4 biloini zimerejeshwa huku Sh 1.3 bilioni mpaka sasa bado hazijarejeshwa," amesema.

Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka (kulia),akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Dk Juma Homera utekelezaji wa mradi wa kituo cha afya Isangawane. Picha na Hawa Mathias
Masache amesema kutokana na urejeshaji hafifu amehamasisha walengwa kuwa wamaminifu ili kuwezesha vikundi vingine kunufaika.
"Leo vikundi 150 vimepata mkopo wa Sh 1.8 bilioni, nitoe rai kuwa waaminifu,lakini inasikitisha kuna watu awali walikopa na walishindwa kurejesha mpaka walienda kusakwa majumbani jambo ambalo halipendezi," amesema.
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Marietha Mlozi amesema kuwa mbali na kutoa mikopo kwa vikundi 131, vipo vingine vinne vimegoma kwa madai kiwango ni kidogo ambapo vilivyo kabidhiwa ni 127 pekee.
Amesema halmasharuri ilitoa tangazo la kuanza kutoa mikopo Februari, 2025, huku iliyoombwa ilifika zaidi ya Sh 5.7 bilioni, kutoka vikundi 256 .
Amesema baada ya kamati mbalimbali kupitia jumla ya Sh1.8 bilioni ,zilipitishwa kutoa mikopo kwa vikundi 131 kutoka maeneo mbalimbali.
"Halmashauri ilianza kutoa mikopo kuanzia mwaka 2017/2025 mikopo yenye thamani ya Sh 2.7 bilioni lengo ni kutekeleza malengo ya Serikali kuwezesha makundi hayo," amesema.
Amesema kabla ya utoaji wa mikopo halmashauri inatoa elimu ya ujasiriamali ya uendeshaji wa miradi, licha ya kuwepo kwa changamoto ya vikundi kuomba mikopo mikubwa, kufa na kushindwa kurejesha.
Mnufaika Salma Ngonyani Mkazi wa Kata ya Chokaa, ameshukuru Serikali kwa mikopo hiyo na kwamba inakwenda kuwa chachu kubwa katika uboreshaji wa miradi yao," amesema.
Kuhusu ucheleweshwaji wa mikopo amesema watahakikisha wanasimamia kikamilifu na kuwabana wanachama ambao wanakwamisha kutoa marejesho kwa wakati.