Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh100 milioni kugharamia matibabu ya macho bure

Mmoja wa wananchi waliotembelea maonyesho ya Sabasaba mwenye nguo ya madoa meupe akipatiwa huduma ya upimaji na matibabu katika banda la Yas ikiwa ni utekelezaji wa kliniki maalumu ya upimaji macho bure.

Muktasari:

  • Yas yatoa Sh100 milioni kufadhili huduma za uchunguzi, dawa, miwani na upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo

Dar es Salaam. Wananchi 15,000 wanatarajiwa kunufaika na huduma bure za uchunguzi wa macho, dawa, miwani na upasuaji wa mtoto wa jicho kupitia Kambi ya Sabasaba.

Kambi hiyo inayofanywa katika maonyesho yanayoendelea ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DiTF) imefadhiliwa na Yas Tanzana kwa ushirikiano na Kliniki ya Khoja Shia Ithna-Asheri Charitable Eye Centre

Akizungumzia kambi hiyo jana Jumatano Julai mosi 2026, Mwenyekiti wa Khoja Shia Ithna-Asheri Charitable Eye Centre, Anwar Rajpar amesema kambi hiyo inatarajiwa kugharimu Sh100 milioni ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za afya ya macho kwa wananchi.

Amesema tangu kuanzishwa kwa kambi hizo zaidi ya watu 300,000 wamefanyiwa uchunguzi wa macho, kupatiwa ushauri wa kitabibu, dawa, miwani na upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo.

“Kwa kawaida kambi zetu zinazofanyika mikoani huhudumia takribani watu 4,000 lakini kwa Sabasaba tunatarajia kuwafikia kati ya watu 10,000 hadi 15,000 kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi,” amesema Rajpar.

Amesema wagonjwa watakaobainika kuhitaji upasuaji hawatafanyiwa katika Viwanja vya Sabasaba kutokana na kukosekana kwa chumba cha upasuaji badala yake watapelekwa katika kliniki ya kituo hicho iliyopo Temeke watakapopatiwa huduma hiyo bila malipo.

Rajpar amesema Yas imekuwa mshirika mkuu wa kambi hizo na kwa miaka miwili iliyopita, ikitoa Sh300 milioni kila mwaka kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) huku gharama za upasuaji wote wa mtoto wa jicho zikigharamiwa na BETA Trust ya Uingereza.

Amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kufanyiwa uchunguzi wa macho mapema, akisisitiza kuwa huduma hizo zinatolewa kwa watu wote bila kujali umri, dini au kabila.

Mkurugenzi wa Kanda ya Dar es Salaam ya Kusini Yas, Robert Kasulwa amesema udhamini wa kambi hiyo ni sehemu ya dhamira ya kampuni ya kurejesha kwa jamii kwa kusaidia wananchi kupata huduma muhimu za afya.

“Hii ni sambamba na kuendelea kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali,” amesema.

Akizungumzia ushiriki wao Sabasaba amesema wanalenga kuhamasisha wananchi kufanya malipo kwa njia ya kidijitali badala ya kutumia fedha taslimu.