Sh105 milioni zalipwa watumishi wasio na mikataba halali

Ripoti ya CAG yatua bungeni

Muktasari:

  • Kwenye ripoti yake ya mwaka 2019/20, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini taasisi nne zililipa wafanyakazi 15 wasio na mikataba halali zaidi ya Sh105.6 milioni.

Dar es Salaam.  Wakati wahitimu wengi wakihangaika kutafuta ajira, wajanja wa mtaa wanapokea mishahara tu kwenye ofisi za umma.

Kwenye ripoti yake ya mwaka 2019/20, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini taasisi nne zililipa wafanyakazi 15 wasio na mikataba halali zaidi ya Sh105.6 milioni.

Wafanyakazi hao ambao watatu walilipwa Sh4.84 milioni na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa huku wawili wakichukua Sh10.54 milioni pale Hospitali ya Mirembe na Chuo cha Isanga walilipwa kinyume cha kanuni za kudumu za utumishi wa umma za mwaka 2009 zinazohitaji waajiri kuingia mkataba unaoonesha masharti ya kazi husika kwa watumishi wanaoajiriwa.

Hawakuwa peke yao, wengine saba walichota zaidi ya Sh64.54 milioni Hospitali ya Rufaa Tumbi na watatu wakaingia Suma JKT, idara ya zana za kilimo na kuondoka na Sh25.68 milioni.

“Ukaguzi niliofanya umebaini watumishi 15 waliaojiriwa kwa muda mfupi kwa masharti yasiyo ya pensheni bila ya kuwa na mikataba, walilipwa Sh105.6 milioni kinyume na kanuni za utumishi wa umma,” amesema CAG Kichere.

Kwa kutokuwa na mikataba ya ajira, CGA anaonya kwamba taasisi hizo zinaweza kushindwa kudhibiti utendaji wa watumishi hao.

Pia, kunaongeza hatari ya kulipa adhabu zisizostahili endapo kutatokea migogoro kwani taasisi hazitakuwa na uthibitisho wa masharti yaliyopo kwenye mikataba kati yao na watumishi.

“Menejimenti za taasisi hizo kuhakikisha zinafuata matakwa ya sheria, kanuni na taratibu katika kuandaa na kuhuisha mikataba pale muda wake unapoisha. Pia, zifanye tathmini kubaini utendaji wa watumishi hao,” ameshauri Kicehere.