Sh110.8 bilioni kuing’arisha Dodoma

Meya wa jiji la Dodoma, Prof Davis Mwamfupe, akizungumza na waandishi wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communication Ltd jijini Dodoma wakati wa mahojiano maalum.

Dodoma. Mwonekano wa Jiji la Dodoma umeendelea kubadilika kutokana na uwekezaji katika miradi mbalimbali yenye thamani ya Sh110.8 bilioni itakayoiwezesha halmashauri kujiendesha na kujitegemea kwa kipato.

Ni halmashauri ya kwanza nchini kati ya 122, ambayo imeweka vitega uchumi vyenye thamani kubwa ya mabilioni ya shilingi.

Fedha hizo ni mgawanyo wa mapato ya ndani ambayo uwekezaji wake ni Sh68 bilioni katika miradi ya ujenzi wa hoteli mbili, moja ikiwa katika mji wa Serikali, Mtumba yenye thamani ya Sh59 bilioni na moja inajengwa katikati ya Jiji ikiwa na thamani ya Sh9 bilioni.

Fedha nyiingine ni mkopo kutoka Benki ya Dunia ambazo thamani yake ni Sh42.8 bilioni zilizojenga Soko la Ndugai, Stendi ya mabasi ya mikoani, eneo la burudani Chinangali na maegesho ya malori Nala, miradi ambayo imezinduliwa na kuanza kazi.

Hayo yameelezwa na Meya wa Jiji, Profesa Davis Mwamfupe alipofanya mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu mwonekano mpya wa Jiji la Dodoma, tofauti na miaka kadhaa iliyopita.

Profesa Mwamfupe amezungumzia miradi mikubwa ya uwekezaji wa jiji hilo ambalo limetajwa kuwa mfano kwa maeneo mengine kutokana na kasi kubwa ya uwekezaji wake.

Katika mazungumzo hayo, Mwamfupe anasema macho yao yako kwenye uwekezaji kutokana na kukua kwa mahitaji ya watu katika kipindi ambacho Serikali imepunguza mtiririko wa fedha kwa halmashauri.

Aidha, katika miradi huyo, alisema wamewekeza fedha nyingi kwa kutumia mapato ya ndani na mkopo kutoka Benki ya Dunia na kwamba miradi mingi inatarajia kuanza kazi Machi mwaka huu.


Fedha za ndani

Kwa mujibu wa Mwamfupe, jiji hilo limejenga hoteli kubwa katika mji wa kiserikali wa Mtumba, ambayo inagharimu Sh59 bilioni na awamu ya kwanza iliyogharimu Sh18 bilioni ipo hatua za mwisho wakitaraji kuifungua Februari.

Kiongozi huyo alisema ujenzi wa awali unahusisha kumbi 10 za mikutano mikubwa zilizojengwa kisasa zaidi ambazo zitaanza kuliingizia Jiji mapato.

“Hoteli hiyo imejengwa katika mji wa Mtumba. Ina kumbi zaidi ya 10 za mikutano na awamu ya pili itakapokamilika kutakuwa na kumbi za hadhi ya mikutano ya kimataifa kwa marais wa nje kuja kufanyia mikutano yao,” anasema Mwamfupe.

Meya anasema hoteli hiyo itakuwa na hadhi ya juu ikiwemo suala la ulinzi kwani itapokea wageni wa kila namna kutoka pembe za dunia, hivyo ujenzi wake unahitaji umakini mkubwa.

Mradi mwingine unaogharimu fedha za ndani ni hoteli kubwa ya ghorofa 11 ambayo imejengwa katikati ya jiji iliyogharimu Sh9 bilioni ambayo ujenzi wake uko katika asilimia 95.

Anaeleza kwamba hoteli hizo wamezijenga kwa kutumia mapato ya ndani na hazina madeni, lakini uendeshaji wake utakuwa ni wa ubia na sekta zingine ili jiji liweze kupata mapato ya kutosha.


Miradi ya mkopo

Profesa Mwamfupe anataja miradi ambayo Jiji limekopea fedha katika Benki ya Dunia na tayari imeanza kuzalisha kuwa ni stendi ya mkoa, Soko la Ndugai, eneo la maegesho ya malori la Nala na eneo la burudani la Chinangali Park.

Anasema Stendi imegharimu Sh20 bilioni, Soko la Ndugai Sh14 bilioni, maegesho ya malori Sh5.9 bilioni na eneo la burudani na mapumziko la Chinangali limegharimu Sh2.9 bilioni.

“Huo wote ni uwekezaji ambao tunalenga kuwa unakwenda kutufikisha mahali salama katika mapato, tunaamini kuwa makusanyo yake yataendelea kuliweka Jiji katika ramani ya kuwa mfano wa mapato yake,” amefafanua Mwamfupe.

Kwa mujibu wa Meya, tayari vituo vingi ikiwemo Chinangali wameshakodisha kwa watu binafsi, hivyo wanaanza kukusanya kodi.


Mapato ya viwanja

Profesa Mwamfupe anazungumzia madai kuwa Dodoma inaongoza kwa mapato kutokana na mauzo ya viwanja kwa watumishi waliohamia, akisema ,“kama wanasema tulitegemea viwanja, sawa, lakini ni halmashauri gani haina viwanja mbona wao hawakuuza huko.”

Amesema uuzaji wa viwanja haujaisha na bado wanaendelea kupima na kuuza lakini kasi yake imepungua na ndiyo maana wakaona waingie na mkakati mpya wa kutafuta mapato mengine ili waendelee kuwa juu.

Hata hivyo, anasema kuendelea kuongoza kwa mapato bila ya kutoa huduma bora haitakuwa na maana kwao bali wangetamani kuendelea kuongoza kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Anasema kwa sasa hawakimbilii kujitegemea kama ambavyo Serikali inawataka, kwani wakifanya hivyo kama hawajajiimarisha wanaweza kujikuta wanakwama mbele ya safari.

Meya anasema vitega uchumi vikienda na huduma kwa watu, kufikia mafanikio ni jambo rahisi sana lakini ikiwa kinyume na hapo itakuwa ni ndoto kuyafikia malengo.

“Mahali pengine tunatakiwa kuwa na msimamo, ndiyo maana leo tumeagiza mabasi yote sasa yaende stendi ya mkoa na hakuna kukata tiketi kwenye majumba ya watu, bali wote waende kule stendi, vinginevyo majengo yale tutakuwa tumeyajenga lakini muda mfupi yatakuwa makao ya popo.


Huduma za taka

Kiongozi huyo wa baraza la madiwani amengumzia uchafu katika baadhi ya mitaa ya jiji akikiri kuwa kuna shida na harufu mbaya inayosababishwa na mitaro ya maji taka kuziba.

Hata hivyo, alitaja miundombinu ya zamani kuwa chanzo cha kuziba kwa mitaro hiyo ambayo kwake anaona inamchafulia sifa ya mji huo uliobeba hadhi ya makao makuu.

“Tumeshaingia mkataba na wenzetu wa Korea ambao wanashirikiana na kampuni moja ya Kitanzania katika kuhakikisha tatizo hilo linakwisha na kwa kuanza tumeanza na hapa katikati ya mji na katika kata ya Chamwino ilimaliza tatizo hilo,” amesema.


Sekta binafsi

Mwamfupe alisema sekta binafsi ndiyo ufunguo wa mafanikio, hivyo jiji limetenga maeneo mengi kwa ajili ya uwekezaji ambayo wakiimarisha itakuwa msaada mkubwa kuibadilisha Dodoma.

Anasema hakuna mafanikio ambayo mtu anaweza kuyapa binafsi asipokuwa na ushirikiano na wengine katika kutengeneza ushindani wa kihuduma ambao huwafanya watu wapate huduma bora.

Kwake anaona uchumi wa mtu mmoja mmoja na Serikali ukienda na huduma kwa watu, itakuwa moja ya sifa nzuri katika ujenzi wa makao makuu katika jiji hilo lakini kama haitakuwa hivyo basi watu wasahau.


Migogoro ya ardhi

Meya anatamba kuwa wamefanikiwa kumaliza migogoro ya ardhi ambayo ilidumu kwa miaka mingi iliyokuwa imesababishwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa kuruhusu watu wapimiwe ardhi yao na kupewa ruhusu ya kuuza watakavyo wao.

Wito wake kwa wafanyakazi ni kuwataka wabadilike na kusisitiza pawepo na utulivu kwani kwenye amani maendeleo huonekana bali kusikokuwa na amani siku zote hakuna maendeleo.