Sh166 bilioni zatumika elimu bure
Muktasari:
- Serikali ya Tanzania imesema hadi kufikia Februari 2021 imetumia Sh166.17 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa elimu msingi bila ada pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu nchini.
Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema hadi kufikia Februari 2021 imetumia Sh166.17 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa elimu msingi bila ada pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu nchini.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 13, 2021 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha bungeni mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/22.
Amesema Serikali imeboresha miundombinu ya shule za msingi 1,372 na sekondari 554 kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.
Majaliwa amesema pia Serikali imekarabati shule 18 za wanafunzi wenye mahitaji maalumu na imeongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi 142,179.
Majaliwa amesema Sh464 bilioni zitatumika kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ikilinganisha na Sh450 bilioni zilizotumika kwa wanafunzi 130,883 mwaka 2019/2020.