Sh300 bilioni kunufaisha wafanyabiashara wadogo, wa kati

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Wafanyabiashara zaidi ya 2,000 wanaofanya biashara ndogondogo na za kati watanufaika.

Dar es Salaam. Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imepanga kutumia Sh300 bilioni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati (SME) ili kuchochea ukuaji wa uchumi unaogusa watu wengi.

Mkakati huo unaenda kutekelezwa wakati ambao benki hiyo imepata faida ya Sh13.6 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 kabla ya kodi, huku faida baada ya kodi ikiwa Sh10.7 bilioni.

Mkurugenzi wa TCB, Adam Mihayo amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari akielezea utendaji wa taasisi hiyo katika kikao kilichoratibiwa na Msajili wa Hazina.

Mihayo amesema SME ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi kwani zinachangia takribani asilimia 30 ya ukuaji huo.

“Tunataka kufanya uwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya uzalishaji, tumewaona SME watakuwa na faida kwa nchi yetu kwa sababu wanachangia asilimia 30 ya ukuaji wa uchumi,” amesema.

Amesema kuwasaidia kuwajengea uwezo wa mtaji kutawafanya kukua, kuajiri watu wengi zaidi na kupanua wigo wa kodi.

Kupitia fedha zilizotengwa, amesema wajasiriamali zaidi ya 2,000 wanatarajiwa kunufaika ili kuchochea ukuaji wao kiuchumi.

Amesema wamechagua kukuza SME kwa sababu zinagusa sekta nyingi nchini, akitoa mfano wa kilimo kilichoajiri watu wengi.

“Pia kuna wajasiriamali wengi ambao kupitia wadau wetu kama vile Benki ya Kilimo, inatupa chachu ya kuendelea kuwasaidia,” amesema Mihayo.

Amesema benki hiyo imekuwa ikiweka mikakati kwa kuangalia vipaumbele vya Serikali.

Katika hilo, amesema TCB imesaidia kwenye uingizaji wa mabehewa ya treni yatakayotumika katika reli ya kisasa (SGR).

“Si hivyo tu, hata wakandarasi wakubwa wa SGR ni wateja wetu, wale wasaidizi tumekuwa tukiwaisaidia. Usaidizi huu tunataka kuupeleka sehemu nyingine, tuko katika maongezi na wenzetu wa Tarura (Wakala wa Barabara za Vijini na Mijini) kuhakikisha tunawawezesha wakandarasi kimtaji kukamilisha miradi yao mapema,” amesema.

Amesema miradi ikitekelezwa mapema, thamani ya kiuchumi ambayo Serikali ilitarajia kuipata inaanza kuonekana mapema.

Mihayo amesema pia wamejipanga kuhakikisha wanafanya uwekezaji wa kutosha katika huduma za kidijitali ili kuongeza wigo wa watu kuzifikia kwa urahisi.

“Kama taasisi pia inatusaidia badala ya kutegemea tu mapato ya riba, tunatengeneza wigo mpana wa kupata mapato mengine. Hii itatusaidia kushusha gharama zetu na kuwezesha huduma kupatikana kwa urahisi,” amesema.

Kupitia uwekezaji huo, amesema wanaamini watapunguza muda ambao unatumika kutoa huduma hivi sasa.

“Tunaamini kwa kufanya hivi ndani ya miaka mitatu hadi mitano tutakua na kuwa benki namba tatu nchini, tunaamini inawezekana,” amesema Mihayo.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema ni vyema benki hiyo ikawa inawakumbusha wateja kila wakati kuwa TCB ndiyo benki iliyounganishwa na nyingine, ikiwamo Benki ya Posta.

“Ni vyena kuwakumbusha wananchi kuwa hiyo ndiyo Benki ya Posta na hakuna kilichobadilika, badala yake imekuwa vizuri zaidi ya ilivyokuwa,” amesema Meena.