Sh4 bilioni zatengwa kuwawezesha wanawake wajasiriamali

Mwenyekiti wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Mercy Sila akizungumzia tuzo za wanawake wajasiriamali zinazotarajiwa kutolewa na taasisi hiyo Machi 16, 2024. Katikati ni Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark Afrika Elibariki Shammy na Mkurugenzi wa TWCC Mwajuma Hamza.

Muktasari:

Wakati dunia ikielekea kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake, wajasiriamali wanawake wamekumbukwa kwa kuandaliwa tuzo ya kuendeleza biashara zao ili kutoa hamasa kwa wengine

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha kundi kubwa la wanawake lililopo kwenye sekta ya biashara linafanya shughuli zao kwa tija, Shirika la Trade Mark Afrika limetenga Sh4 bilioni zitakazotumika kwa miaka sita kutoa mafunzo na uwezeshaji wajasiriamali wanawake.

Fedha hizo zitatolewa kati ya mwaka 2024 hadi 2030 kupitia mradi ulio chini ya Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) unaolenga kuwajengea uwezo wanawake kufanya biashara ndani na nje ya nchi.

Hii ni awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo ulioanza mwaka 2016 hadi 2023 huku Sh7.5 bilioni zikitumika kuwawezesha wanawake zaidi ya 20,000 waliofikiwa na mradi huo.

Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark Africa, Elibariki Shammy amesema utekelezaji wa mradi huo unakwenda sambamba na utoaji wa tuzo kwa wanawake wanaofanya vizuri kwenye biashara ili kutoa hamasa kwa wengine ili waongeze juhudi.

Shammy amesema wanawake wafanyabiashara wanapitia changamoto nyingi zinazowafanya wengi wao wakate tamaa au kushindwa kukuza mitaji yao, hivyo uwepo wa miradi inayowajengea uwezo na kuwapa motisha wanaofanya vizuri ni hatua ya muhimu.

“Kuna changamoto nyingi zinazowakabili wanawake wafanyabiashara kuanzia kwenye mazingira yenyewe ya biashara, masuala ya kifamilia, kukosa kuaminiwa kwenye taasisi za fedha zinazotoa mikopo na mambo mengine mengi.

“Ndiyo maana mradi huu upo na tangu umeanza tunaanza kuona mabadiliko, angalau baadhi ya wanawake wamekuza biashara zao kutoka hatua moja kwenda nyingine, ili kuwapa hamasa wengine ni lazima hawa wapewe motisha ikiwamo hizi tuzo zinazoenda kutolewa na TWCC katika kusherehekea mafanikio ya wanawake,” amesema Shammy.

Akizungumzia tuzo hizo zitakazotolewa Machi 16, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TWCC, Mwajuma Hamza amesema zitahusisha vipengele 20 kutoka kwenye sekta mbalimbali ikiwamo ya kilimo, uzalishaji, madini, usafirishaji, biashara nje ya nchi, mawasiliano, usimamizi wa hafla, mama lishe, ufugaji na ufungashaji.

Vipengele vingine ni ujenzi, afya, elimu, utalii, uhandisi, biashara za kuvuka mipaka, sanaa na teknolojia ya habari.

Amesema tuzo hazitatolewa kwa watu kupigiwa kura bali kuomba au kupendekezwa na watu wengine watakaovutiwa na kazi za wahusika kisha timu ya chemba hiyo itapitia maombi na mapendekezo hayo kwa kuangalia vigezo vilivyowekwa.

Amevitaja vigezo hivyo kuwa ni uendelevu wa biashara, kiasi cha mtaji kisichopungua Sh5 milioni, nembo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa wafanyabiashara wanaohusika na uzalishaji, umiliki wa biashara na waliojikita kwenye kilimo biashara.

“Nitumie fursa hii kuwaita wanawake wajasiriamali kujitokeza kuomba kutuma maombi au kama kuna mwanamke unaona anastahili unaweza kumpendekeza sisi tutafuatilia kuhakikisha amekidhi vigezo vyetu na kama anastahili basi atakuwa miongoni mwa tutakaowatambua,” amesema Mwajuma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila amesema jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali zinaongeza hamasa ya wanawake kuingia kwenye biashara na kujitengenezea kipato.

“Tunaona Serikali inafungua nchi na kuboresha mazingira ya uwekezaji, wanawake wanaendelea kuchangamkia fursa hii na kufanya biashara ingawa bado biashara nyingi ni zile ndogo ndogo na ukweli ni kwamba wanawake wanaogopa kukua kwa kuhofia changamoto watakazokutana nazo mbele endapo watakuza biashara zao,” amesema Mercy.