Sh45 bilioni kusaidia kuboresha afya za kina mama

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Maendeleo na Afrika, Andrew Mitchell (kushoto) akizungumza na wananchi na viongozi wa Zanahati ya Vingunguti alipotembelea kukagua mradi wa huduma za uzazi wa mpango na afya kwa kina mama.

Muktasari:

  • Ni msaada wa Serikali ya Uingereza kupitia mradi unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la EngenderHealth.

Dar es Salaam. Serikali ya Uingereza imetoa msaada wa Sh45 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa miaka miwili wa huduma za uzazi wa mpango na afya za kina mama.

Awali, mradi huo unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la EngenderHealth, ulionza mwaka 2019 ulikuwa unafikia tamati Agosti 2024.

Kwa nyongeza ya fedha hizo, mradi sasa utafikia tamati Agosti 2026.

Hayo yamebainishwa jana Aprili 4, 2024 na Waziri wa Uingereza anayesimamia masuala ya Maendeleo na Afrika, Andrew Mitchell alipotembelea Zahanati ya Vingunguti, jijini Dar es Salaam kukagua mradi huo.

“Uingereza na Tanzania ni marafiki, Serikali yetu inaamini wanawake wana uhuru wa kuchagua kama wanahitaji kuwa na watoto, kwa wakati gani na wangapi, ndiyo maana tumeamua kutoa fedha hizo,” amesema Mitchell.

Mkurugenzi Mkazi wa EngenderHealth, Dk Moke Magoma amesema mradi huo unahusika katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na unalenga kuboresha afya za kina mama nchini.

“Tulikuwa tunaufadhili wa mradi wa miaka mitano uliotarajiwa kuisha Agosti, sasa ufadhili mwingine umeongezeka wa miaka miwili wa Sh45 bilioni. Katika kipindi cha miaka minne tuliwafikia watu zaidi ya milioni mbili nchi nzima,” amesema.

“Tupo katika mikoa minane ya Tanzania Bara yenye asilimia 40 ya watu wa nchi. Mradi unachangia asilimia 30 za huduma zote za afya, hasa za uzazi wa mpango zinazotolewa katika mikoa minane,” amesema Dk Magoma.

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Tanga, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro. Kwa Zanzibar amesema wapo mikoa yote.

Dk Magoma amesema miongoni mwa majukumu yanayotelekezwa katika mradi huo ni kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Katika utekelezaji wa mradi huo, amesema wananunua vifaatiba ili kuendeleza huduma, na kupata ubora wa taarifa ili kutoa huduma kwa kutumia takwimu sahihi.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema Tanzania na Uingereza ni marafiki wa siku nyingi na wamekuwa wakishirikiana katika masuala ya sekta za afya, hasa kuboresha afya za kina mama.

“Si umeona amekuja na ametoa msaada wa fedha Sh45 bilioni, hii inatokana na uhusiano mzuri kati yetu na Uingereza,” amesema Dk Mollel.

Amesema masuala ya kupanga uzazi yanahusisha mama na mtoto na ili upate mama mwenye afya bora lazima kuwapo mchakato wa namna ya kuzaa, kuwalea, na kuwatunza vizuri watoto.

“Hatusemi watu wasizae, hapana, bali ni kupanga uzazi kulingana na uwezo wao wa kuwalea na kuwasomesha ili kujenga jamii yenye uwezo mkubwa wa akili,” amesema Dk Mollel.