Sh50 bilioni zahitajika kukarabati barabara zilizoathiriwa na mafuriko

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,  Profesa Kitila Mkumbo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mafanikio ya Serikali kuelekea miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.

Muktasari:

  • Takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha mtandao wa barabara nchini umefikia kilomita 11,969.

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema takribani Sh50 bilioni zinahitajika kukarabati barabara zilizoharibiwa na mafuriko ili ziweze kurudi kwenye hali yake.

Profesa Mkumbo ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 17, 2024 jijini Dodoma, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwenye kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema katika kipindi cha miaka 60 zipo changamoto ambazo zimejitokeza na zitaendelea kutatuliwa kila siku ili kuleta ustawi wa Taifa, ikiwamo ya uharibifu wa miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mafuriko.

“Na hatusemi kwamba changamoto hazipo, zipo kama sasa hivi tumepata mafuriko barabara zetu nyingi zimeharibika, ukarabati peke yake takribani Sh50 bilioni zinahitajika ili kurudisha zilivyokuwa awali,” amesema Profesa Mkumbo.

Amesema kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano mtandao wa barabara umekua.

Profesa Kitila amesema hadi mwaka 2000 mtandao wa barabara za mikoani zilizojengwa kwa lami na zege Tanzania nzima zilikuwa kilomita 4,179.

Amesema malengo yalikuwa ifikapo mwaka 2025 mtandao ufike kilomita 13,000 lakini kwa takwimu za mwaka 2022 mtandao wa barabara nchini umefikia kilomita 11,969.

Kuhusu ukuaji wa uchumi, Profesa Kitila amesema unakua vizuri hadi kufikia wastani wa asilimia saba lakini hali ilikuwa mbaya mwaka 2020/2021 kutokana na Uviko-19, uchumi uliporomoka hadi kufikia asilimia moja lakini kwa sasa umeimarika kufikia asilimia 5.2.

Kwa upande wa elimu, amesema lengo la Serikali lilikuwa kuandikisha asilimia 100 ya watoto wote wenye umri wa kuanza shule ya msingi ambao ni miaka sita hadi 13 ifikapo mwaka 2025, lakini mpaka sasa lengo limevukwa kwa kuandikisha asilimia 108.5.

Amesema bado kuna mdondoko mkubwa wa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali.

Profesa Kitila amesema wanaomaliza shule kwa elimu ya msingi ni asilimia 70, huku wanaomaliza elimu ya sekondari ni asilimia 48.

Kwa upande wa afya, amesema huduma kwa sasa zimeboreshwa, kina mama wengi wanajifungulia kwenye vituo vya afya ambavyo vina wataalamu, hivyo kupunguza vifo vya kina mama na watoto vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 1,000 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 1970 hadi kufikia vifo 104 kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 2022, lengo la Serikali lilikuwa kupunguza vifo hivyo hadi kufikia 265 mwaka 2025.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, Serikali bado ipo kwenye mapambano na ugonjwa wa Malaria ambao ndiyo unasababisha vifo vya watoto wachanga nchini, kwa kuua mbu ili kutokomeza ugonjwa huo.