Wananchi wadai ahadi ya Serikali kujenga barabara

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kahe Mashariki, wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wakitengeneza barabara yao katika maeneo mabovu.

Muktasari:

  • Barabara hiyo ambayo ina urefu wa Kilometa 12, maeneo mabovu yenye urefu wa mita 500 na imekuwa shida kupitika katika kipindi cha mvua.

Moshi. Wananchi wa Kata ya Kahe Mashariki, wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wameungana na kujitolea kutengeneza barabara yao katika maeneo mabovu ili kuondokana na changamoto ya usafiri na usafirishaji wanayokumbana nayo vipindi vya mvua.

Barabara hiyo ambayo ina urefu wa Kilometa 12, maeneo mabovu ni mita 500, ambayo yamekuwa shida kupitika katika kipindi hiki cha mvua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kutengeneza barabara hiyo hivi karibuni, wananchi hao wamesema wamechoshwa na ahadi za Serikali za muda mrefu za kutengeneza barabara hiyo ambayo imekuwa mbovu katika vipindi vyote vya mvua na kukwamisha shughuli za maendeleo.

Edwin Molla mkazi wa kijiji cha Soko, amesema wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuondoa adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao yao, ambayo yamekuwa yakiharibikia njiani kutokana na ubovu wa barabara.

"Babarara hii imekuwa korofi kwa muda mrefu na tumekuwa tukitaabika sana katika kipindi cha mvua kama hiki, na sasa tumeamua kujitolea kujaza vifusi ili kuiwezesha kupitika," amesema.

Kwa upande wake Gabriel Gasper ambaye ni dereva bajaji, amesema barabara hiyo imekuwa kero kwa muda mrefu hali ambayo imekuwa ikiwafanya kushindwa kuzifikia huduma za kijamii ikiwemo hospitali, shule na nyingine wakati wa mvua na kuiomba serikali kutekeleza ahadi yake.

"Kwetu madereva hili ni tatizo kubwa kwetu, leo tunajaza vifusi maeneo korofi lakini tayari serikali iliahidi kutengeneza barabara hii, tunsomba itekekeze sasa ahadi yake, ili tuweze kusafiri maeneo salama," amesema Gasper.

Akizungumza Diwani wa kata hiyo, Kulwa Mmbando, amesema walikubaliana katika kikao cha maendeleo ya Kata na kutoa Sh1 milioni kukarabati barabara hiyo wakati wakisubiri mvua zikatike ili mkandarasi aanze kazi ya ukarabati wa barabara hiyo.

Mmbando amesema tayari serikali imetenga Sh120 milioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo lakini kwa sasa mkandarasi ameshindwa kuanza kazi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha 

"Kutokana na ubovu wa barabara, mazao yetu yanaharibika njiani na kupoteza thamani. Pia tunapata shida ya kufika hospitali, shule na masokoni, lakini serikali imetoa Sh120 milioni kwa ajili ya kutengeneza barabara hii ili tuweze kuboresha maisha yetu," amesema Mmbando.

Alipotafutwa Meneja wakaka wa barabara za vijijini na Mjini (Tarura) Wilaya ya Moshi, Orota Africano amesema kwa sasa hataweza kuzungumzia suala hilo kutokana na mazingira aliyopo na kuomba atafutwe Jumatatu.