Sh50 milioni faini kwa anayehatarisha usalama wa reli

Muktasari:
- Shirika la Reli Tanzania (TRC) latoa tahadhari kwa wananchi mkandarasi anapofanya majaribio ya umeme.
Chamwino. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limewatahadharisha wananchi kuhusu madhara ya umeme wa kuendeshea reli ya kisasa (SGR), likieleza adhabu ya kuhatarisha usalama wa abiria ni kifungo jela miaka mitano, faini ya Sh50 milioni au vyote kwa pamoja.
Hayo yameelezwa leo Aprili 9, 2024 na Mwanasheria wa TRC, Jonas Maheto wakati wa utoaji wa elimu ya usalama kwa wakazi wa vijiji vitatu vya wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
Elimu imetolewa katika vijiji vya Igandu, Chimwaga na Chibwe, huku Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja akishuhudia.
Amesema sheria za reli ni kali tofauti na za barabarani kwa sababu reli inapita kwenye njia yake haichangamani na matumizi mengine.
Maheto amesema kosa la kwanza ni la kuhatarisha usalama wa abiria na miundombinu, ambalo anayepatikana na hatia adhabu ni ama kifungo cha miaka mitano jela, faini ya Sh50 milioni au vyote kwa pamoja, lengo likiwa ni kusaidia watu kuwa salama.
“Unavyokaa juu ya tuta la reli, ukanaswa na umeme maana yake wewe ndiye uliyehatarisha usalama, hata kama umeumizwa na treni, umekatwa mguu au mkono utasubiriwa upate nafuu na utapelekwa mahakamani kwa kusababisha hatari,” amesema.
Maheto ametaja kosa lingine ni wizi wa miundombinu kwa watu kuchukua kokoto, kukata uzio, kuchomoa mataruma ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano na kuendelea.
“Wapo watu hawaibi wanaamua kutoa kokoto mahali pake au kuchomoa misumari kuitupa pembeni, huo ni uharibifu maana unapoharibu treni inaweza kutikisika na kuacha njia. Unaweza kujikuta una makosa matatu au manne kwa pamoja kwa hiyo utapata adhabu kali,” amesema.
Maheto amesema adhabu kwa uharibifu wa miundombinu ya reli ni kifungo cha miaka 14 jela na kosa hilo halina faini.
Kosa lingine ni uvamizi na uchafuzi wa mazingira ya miundombinu ya reli.
Msiguse vyuma na nyaya
Mhandisi wa TRC, Christina Samwel amesema ujenzi wa kipande cha pili cha SGR kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma kimefikia zaidi ya asilimia 96.
Amesema hatua waliyofikia ni mkandarasi kutaka kuingiza umeme kwenye njia ya reli.
Ameeleza kutoka Morogoro hadi Ihumwa tayari vituo vya kupokea umeme vimeshawekwa nishati hiyo ambayo ni kilovoti 220.
Amesema umeme huo ni mara 1,000 zaidi ya umeme unaotumika majumbani, hivyo wananchi wakae mbali na vituo hivyo kuepuka madhara.
Christina amesema mwishoni mwa Aprili, mkandarasi ana mpango wa kuanza kufanya majaribio ya kupitisha umeme kwenye njia ya reli.
“Hivyo hizo nyaya zilizopita katika njia ya reli mwisho wa mwezi wataanza kufanya majaribio ya kupitisha umeme, tunaomba wananchi msisogee kwenye miundombinu ya reli maana zile nyaya na vyuma vitakuwa na umeme, tukae mbali,” amesema.
Amesema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limepeleka umeme wenye nguvu ya kilovoti 220 lakini itapunguzwa hadi kilovoti 27.5, ambazo ni mara 100 zaidi ya umeme unaotumika majumbani.
Christina amesema kwa kuzingatia usalama wa wananchi, mradi umeweka vivuko maalumu vya kuvuka watu chini na juu, hivyo watumie njia sahihi kupita.
Amesema mkandarasi amepewa muda wa kukamilisha mradi hadi Oktoba, 2024.
Ofisa Jamii wa TRC, Lightness Mngulu amesema kwa kuwa kazi ya ujenzi wa vivuko na uzio haijakamilika vitafungwa vivuko vya muda wakati wa majaribio.
Kwa upande wa Mayanja amesema lengo la Serikali si kupoteza maisha ya watu au kusababisha ulemavu bali ni kuleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Kwa hiyo mhakikishe hampiti katika njia ya reli, kwa usalama wetu tutumie vivuko vya kuvukia sisi na wanyama,” amesema.
Amewataka TRC kufikisha elimu katika maeneo ya mkusanyiko wa watu kama vile shuleni kwa kuweka alama zenye maelezo ya jinsi ya kuepuka hatari, wakati majaribio yatakapoanza.