Sh700 bilioni kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro
Muktasari:
- Serikali imebainisha kuwa wastani wa Sh700 bilioni zitaihitajika kwa ajili ya kuhamisha kaya 22,000 zilizoko eneo la hifadhi la Ngorongoro ikiwa wananchi wote watataka kuondoka ili kupisha ikolojia ya uhifadhi kwenye eneo hilo.
Dodoma. Serikali imebainisha kuwa wastani wa Sh700 bilioni zitaihitajika kuhamisha kaya 22,000 zilizoko eneo la hifadhi la Ngorongoro ikiwa wananchi wote watataka kuondoka ili kupisha ikolojia ya uhifadhi kwenye eneo hilo.
Naibu Kamishina wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Christopher Timbuka mewaambia waandishi wa habari leo Julai 22,2022 jiji Dodoma wakati akizungumzia mpango wa uhamaji kwa hiyari unavyokwenda.
Dk Timbuka amesema kiasi hicho ni kikubwa lakini kwa namna ya umuhimu wa eneo hilo, fedha hizo ni ndogo na zinaweza kupatikana kwa muda mfupi kutoka kwenye eneo husika hasa kama shughuli za kibinadamu zitapungua.
Dk Timbuka amesema hadi kufikia Julai 18,2022, kaya 757 zenye idadi ya watu 4,344 na mifugo 8,276 zilikuwa zimejiandikisha kuhama kutoka Ngorongoro kwenda kijiji cha Msomemela wilaya ya Handeni ambako zoezi linaendelea hadi sasa.
Amesema idadi ya watu wanaohama katika eneo hilo wanaendelea kujiorodhesha kwa kasi ambayo hawakuitegemea, hivyo kuna kila haja ya kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba na miundombinu ya kuwapokea katika eneo hilo ambalo ni rafiki kwa shughuli za ufugaji na kilimo.
“Ni kweli gharama za kuhamisha watu ni kubwa, lakini mapato yanayotokana na eneo hilo na hasa yakishakuwa wazi yataongezeka zaidi kwa hiyo ni hali ya kawaida kabisa kwenye zoezi hili,” amesema Dk Timbuka.
Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo, Serikali inafanya mkakati wa kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na utalii hadi kufikia watalii 1.2 milioni na mapato kufikia Sh260 bilioni ifikapo mwaka 2025, hivyo kuomba wakazi wa maeneo hayo kuendelea kujiorodhesha ili waweze kuhama kwani hata huko wanakwenda kuna manufaa makubwa kuliko wanakotoka.
Amezitaja baadhi ya faida za kuwenda Msomela ni kumilikishwa ardhi, kuwa na nyumba za kudumu na kuwa na mashamba na kusomesha watoto kwa nafasi zaidi tofauti na walikotoka ambao vitu vingi vimezuliwa.