Shahidi adai Mukama hakutambuliwa na mfumo wa TLS kama wakili

Muktasari:

  • Mukama anakabiliwa na mashtaka mawili ya kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa, na kuzuia watumishi wa umma kufanya kazi yao.

Dar es Salaam. Ofisa Maadili kutoka  Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Vivian Swai (32), ameieleza mahakama kuwa mfumo wa mawakili wa TLS ulithibitisha kuwa namba 4696 ya uwakili iliyotajwa na mshtakiwa Baraka Mukama kuwa ni yake, ilikuwa na jina la Nyando Nashon.

Mukama anakabiliwa na mashitaka mawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambayo ni kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa na kuzuia watumishi wa umma kufanya kazi yao.

Swai ametoa maelezo hayo, leo Machi 27, 2024, alipotoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, wakati wa usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali, Happy Mwakamale, amedai Mei 23, 2023 akiwa ofisini jioni aliona taarifa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuwa wakili azua tafrani Mahakama ya Kisutu.

"Kutokana na majukumu yangu ya kazi ambayo ni kusimamia maendeleo ya mawakili, kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kukamata mawakili vishoka kisha kutoa elimu baada ya taarifa hiyo kesho yake nilichukua nafasi ya kufika Mahakama ya Kisutu," amedai Swai na kuongeza:

"Nilipofika nilionana na Inspekta Sultan ambaye ni kiongozi mahakamani hapo kisha nilimuuliza kuhusu taarifa za Mukama, aliniambia alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam."

Amedai baada ya kupewa taarifa hizo alienda kituoni hapo akiwa na Inspekta Sultan. Walipofika alijitambulisha kwa Mkuu wa Upelelezi akieleza wanahitaji kumuona Baraka Mukama kwa ajili ya kumsaidia.

"Baraka alichukuliwa kule mahabusu, kisha nikajitambulisha kwake kuwa natoka TLS nataka kumsaidia, hivyo nilitaka anitajie jina kamili, alidai anaitwa Wakili Baraka Mukama na namba ya uwakili ni 4696," amedai.

Amedai alichukua hatua ya kuingia kwenye mfumo wa Mawakili wa Tanganyika kisha aliandika jina kamili na namba ya uwakili ambayo alitaja likatokea jina la Nyando Nashon na si Mukama.

"Baada ya kuona jina tofauti na ambavyo amenitajia nilienda kujiridhisha katika mfumo wa Mahakama ambao unatambuliwa na TLS jina halikutokea, kisha nilienda kumweleza akanijibu ni suala la mtandao," amedai.

Baada ya hapo amedai alimtaka Mukama aonyeshe kitambulisho chake cha uwakili.

"Mukama alidai hana, Polisi waliamua kumrudisha mahabusu kwa upelelezi zaidi kwani mfumo wa TLS haukumtambua," amedai.

Amedai siku iliyofuata walipata barua kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kuwa inahitajika taarifa na uhakiki wa wakili Mukama.

Ameeleza ofisa aitwaye Rose Salvator aliwaandikia barua kuwajibu kuwa Mukama si wakili.

Amedai changamoto anazokabiliana nazo ni kuwa wakili ambaye si taaluma yake ambapo anaweza kusababisha wananchi kukosa haki zao za msingi.

Amesema mawakili wanaaminiwa, hivyo tasnia ya mawakili iheshimiwe na watu wote.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, Hakimu Swallo aliahirisha kesi hadi Aprili 24, 2024 itakapoendelea. Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.