Shahidi akutwa na ‘diary’, simu kizimbani kesi kina Mbowe

New Content Item (1)
Shahidi akutwa na ‘diary’, simu kizimbani kesi kina Mbowe

Muktasari:

  •  Shahidi wa pili upande wa mashtaka katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amekutwa na ‘diary’, kalamu na simu kizimbani.


Dar es Salaam. Shahidi wa pili upande wa mashtaka katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amekutwa na ‘diary’, kalamu na simu kizimbani.

Shahidi huyo aliyejitambulisha kama askari H4323 DC Msemwa anayefanya kazi kituo Cha Polisi Oyster bay amekutwa na vifaa hivyo leo Ijumaa Novemba 12, 2021 katika Mahakama Kuu ya Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Awali, Wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala alisimama mahakamani hapo na kuieleza kuwa shahidi huyo ana simu, diary na karatasi

Hivyo Wakili Kibatala aliiomba mahakama hiyo uuondoe katika kumbukumbu za Mahakama  ushahidi alioutoa akiwa chini ya kiapo.

Kibatala: Vifaa anavyo tena mbele ya mabenchi mawili ya mawakili wa Serikali.

 Baada ya kueleza hayo, shahidi alitoa simu na diary  na kisha vitu hivyo  kuchukuliwa na karani wa Mahakama.

Jaji: Umeona hivyo vifaa anavyo?

Kibatala: Nimeona.  Tangu zamani shahidi  alikuwa na emotion (mhemko) na alikuwa anaandika, hivyo akaguliwe.

Jaji: Unataka akaguliwe sasa hivi  au tuache kwanza upande wa mashtaka wamalize kutoa hoja zao?

Kibatala: Hivyo vitu akabidhi kwa ofisa wa Mahakama,  halafu awe chini ya ulinzi kama tunaweza kufanya hivyo.

Jaji: Sawa.

Shahidi tayari akakabidhi vifaa hivyo kwa karani wa Mahakama, huku upande wa mashtaka ukiendelea kutoa hoja za kupinga maelezo ya upande wa utetezi kuhusu  barua ya Naibu Msajili iliyotolewa na DC Msemwa, kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi.

Jaji: Nimekusikia bwana Kibatala ulisimama na kuomba Mahakama kuhusiana na shahidi kuwa na diary kizimbani.

Kibatala: Tunaomba maelekezo yako kuzingatia na muda kutokana na pingamizi diary ya shahidi iwekwe hadi pale utakapotolewa uamuzi au wenzetu kama wanao,  kwa kuwa amekiuka kiapo cha mahakama.

Wakili Kidando: Hata kama hilo lilitokea…Hatujasikia sehemu yoyote vitu hivi vikilalamikiwa  vimetumiwa wakati shahidi anatoa ushahidi wake. Hicho alichosema Kibatala tukianza kuingia kwenye zoezi hilo tu nahitaji kuwa waangalifu kitu kama simu ni kitu binafsi. Kwa nini nasema ni eneo hatari anataka kuchukua kwenye simu kuna nini na kwenye diary kuna nini.

Jaji: Ulisema shahidi ana simu na diary hujasema kama alikuwa anatumia, tukumbushane sheria kabla shahidi hajaingia afanyiwe upekuzi.

Jaji: Diary inaweza kupekuliwa lakini kwenye simu tunaenda mbali

Kibatala: Niliarifiwa mapema na Profesa J kuwa  shahidi anasoma hasa wakati anataja majina ya askari lakini wakati tunabishana hapa alikuwa na peni.

Jaji: Kwenye simu naona ugumu arudishiwe lakini kwa weekend hii nendeni mkafanye research katika maeneo hayo halafu Jumatatu tutaona namna gani ya kufanya ila simu arudishiwe diary itabaki kwa mahakama.

Wakili Kidando: Nina angalizo tunapofanya zoezi hili, sio kila ombi linaloletwa mahakamani sio lazima likubaliwe.

Jaji: Naona kuna vifungu vya sheria vimetajwa lakini kafanyeni research Jumatatu mkija tuangalie linafanywa kwa sheria ipi hapa Kibatala hukuzungumza chochote.

Jaji : Naahirisha kesi hadi Jumatatu Novemba 15 kwa ajili kutolea uamuzi. Shahidi nakuonya uje kuendelea na ushahidi na washtakiwa wataendelea kubaki chini ya uangalizi wa Magereza.