Shahidi asimulia mtoto alivyouawa, adai mshtakiwa alisema hajamzaa yeye

Ahemas Anold (28) mshtakiwa kwa kosa la kumuua mtoto wake mwenye umri wa mwezi mmoja akiwa katika  Mahaka Kuu Kanda ya Geita. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

  • Mume anakabiliwa na kesi ya  mauaji, akidaiwa kumuua kwa makusudi mtoto wake Anna Shemas, Oktoba 19, 2021 katika Kijiji cha Kakumbi Kata ya Masumbwe wilayani Mbogwe.

Geita. Shahidi wa nane wa upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja anayedaiwa kuuawa na baba yake, amesoma maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya mshtakiwa, ambapo mtuhumiwa ameeleza namna alivyomuua mtoto huyo kwa kumyonga.

Shahidi huyo Koplo Alex ambaye ni askari wa upelelezi Wilaya ya Mbogwe, ametoa ushahidi huo leo Aprili 16, 2024 katika Mahakama Kuu Kanda ya Geita.

Kesi hiyo ya jinai namba 53 ya mwaka 2022 dhidi ya Shemas Anold Juma, inasikilizwa na Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Kelvin Mhina.

Shemasi anakabiliwa na kesi ya  mauaji, akidaiwa kumuua kwa makusudi mtoto wake Anna Shemas, Oktoba 19, 2021 katika Kijiji cha Kakumbi, Kata ya Masumbwe wilayani Mbogwe, kinyume na kifungu 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Godfrey Odupoy, shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa yeye ndiye aliyemhoji mshtakiwa na katika mahojiano hayo alikiri kutenda kosa na akaeleza sababu zilizomfanya atekeleze mauaji hayo.


 Maelezo ya shahidi

Kwa mujibu wa maelezo hayo ya onyo, mshtakiwa alikuwa akiishi na mkewe aliyemtaja kwa jina la Kulwa James.

Amedai Oktoba 18, 2021 saa 12 jioni akiwa katika Kitongoji cha Kakumbi, alimwomba mkewe ampeleke mtoto wake hospitali (ambaye kwa sasa ni marehemu) kwa kuwa alikuwa anaumwa tumbo.

Akiwa njiani kwenye pikipiki, alimwambia dereva ampeleke Logito na wakati wako njiani alimkaba mtoto kwenye shingo huku akiwa amemziba mdomo na pua.

Alipofika Lugito alimtaka dereva bodaboda asimame amsubiri na yeye alikwenda hadi sehemu yenye shimo lililokuwa na maji na kumfunika mtoto kwa kitenge kisha kumtupa kwenye shimo.

“Niliporudi dereva aliniuliza mbona sina mtoto, nikamwambia nimemuacha kwa bibi yake (mama yake mshtakiwa) na kurudi nyumbani.

Baada ya kurudi nyumbani, mkewe alimuuliza kuhusu mtoto na yeye alimweleza kuwa amepelekwa Hospitali ya Bugando na bibi yake.

Kuhusu sababu za kumuua, alisema ni baada kugundua si wake kutokana na mtoto huyo kutofanana wala mama yake.

Shahidi wa tano katika kesi hiyo, Kulwa James ambaye ni mama wa marehemu, ameieleza Mahakama kuwa siku ya tukio mtoto alikuwa akilia ndipo baba yake alimbeba na kumpeleka hospitali, lakini aliporudi hakuwa na mtoto na alipohoji alidai amepelekwa hospitali na bibi yake.

Alidai baada ya majibu hayo alianza kulia kwa sauti, ndipo watu akiwemo mwenyekiti wa kitongoji walifika na akawaeleza kuwa mumewe amerudi bila mtoto ndipo mtuhumiwa huyo alitakiwa kumpeleka mama wa mtoto kwenye hospitali aliyolazwa mtoto.

“Kesho yake tulianza safari ya kwenda Bugando tukiwa njiani, alidai mama yake amemtumia ujumbe na kumweleza kuwa mtoto amezidiwa wanapelekwa Muhimbili, akamwambia asubiri lakini aliambiwa mtoto amezidiwa hivyo wanamuwahisha,” amedai James.

Akiendelea kutoa ushahidi wake, James amedai baada ya kufika Mwanza, walikaa nyumba ya wageni kwa siku tatu na kurudi Masumbwe lakini hawakufikia kwenye nyumba waliyokuwa wamepanga na alipohoji sababu ya mumewe kumwambia wasirudi, akamjibu kuwa majirani ndio waliomloga mtoto, wakirudi hata yeye kidonda chake cha operesheni ya uzazi hakitapona.

“Tulishukia gesti hapo Masumbe, kesho yake nikamwambia sasa kwa nini tuendelee kukaa gesti tukitumia hela, nikamshauri atafute chumba na akatafuta tukahamia eneo lingine.”

Amedai baada ya miezi miwili akiwa Masumbwe mume wake hakurudi nyumbani, naye akapata taarifa kuwa amekamatwa na polisi kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Alisema Novemba 22, 2021 alienda Kahama kwa mjomba wa mume wake, alipofika alipokewa kwa pole ya msiba na alipohoji msiba wa nani, alielezwa kuwa mume wake alipiga simu akisema mtoto wao amefariki dunia.

“Nilimjibu mjomba sina taarifa, ninachojua mtoto wangu yupo na bibi yake hospitali. Kesho yake tulirudi hadi Masumbe na kwenda Kituo cha Polisi Masumbe kutoa taarifa ya mtoto wangu kuchukuliwa na baba yake na sijui aliko.”

“Mjomba wake alipiga simu kwa mama mkwe wake ambaye alidai hajawahi kupewa mtoto na hata hamjui,” alisimulia shahidi huyo.

Alipoulizwa na Wakili wa utetezi, Elizabeth Msechu kama walifanya uchunguzi wa vinasaba kubaini kama mtoto aliyetolewa kwenye shimo ni wake, shahidi huyo alidai hawakufanya.

Baada ya ushahidi huo, upande wa mashtaka umefunga ushahidi wake na Mahakama imesema mshtakiwa anakesi ya kujibu na atatakiwa kuanza kujitetea.

Hata hivyo, akijitetea, Shemasi amedai kuwa hajawahi kuoa wala kuwa na mtoto.

Amedai kuwa alikamatwa akiwa mnadani Bukombe kama mhamiaji haramu na kufikishwa Kituo cha Polisi Masumbwe, lakini baada ya siku tatu alipandishwa mahakamani akishtakiwa kwa kosa la mauaji.

Upande wa utetezi umefunga ushahidi wake na kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 30, 2024 itakapokuja kwa ajili ya uamuzi.