Shule kujengwa kukuza vipaji
Muktasari:
- Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde amesema mpango wa Serikali uliopo kwa sasa ni kujenga shule kwenye kanda 8 nchi nzima kuhakikisha wanakuza na kuibua vipaji mbalimbali kwa vijana ikiwemo michezo.
Rombo. Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde amesema mpango wa Serikali uliopo kwa sasa ni kujenga shule kwenye kanda 8 nchi nzima kuhakikisha wanakuza na kuibua vipaji mbalimbali kwa vijana ikiwemo michezo.
Silinde ameyasema hayo wakati wa mchuano wa mashindano ya fainali ya mpira wa miguu ya "Mkenda Cup" yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.
Michuano hiyo ambayo ilikutanisha timu zaidi ya 63 kutoka wilaya hiyo imemalizika kwa kuzikutanisha timu za Motamburu Kitendeni(Rongai FC) na Ubetu Kahe FC ambapo Rongai FC iliibuka mshindi wa mashindano hayo kwa mwaka 2022 kwa mkwaju wa penalti 6 kwa 5 baada ya kufungana bao 1-1 ndani ya dakika 90 na kujinyakulia kitita cha Sh2milioni pamoja na kombe.
"Mashindano yenu yamedhihirishia umma wa Watanzania kuwa Rombo ni imara kweli kweli na kuna vipaji vikubwa, niseme Profesa Mkenda hiki alichokifanya umefanya kazi kubwa sana na yenye baraka kubwa mbele ya mwenyezi Mungu na bahati nzuri wananchi wa Rombo mmepata mbunge mzuri na mchapakazi,"amesema amesema na kuongeza.
"Mpango wa Serikali ni kujenga shule kwenye kanda 8 nchini, kwa hiyo shule hizo zitakapokuwa zimekamilika maana yake tutaibua vipaji mbalimbali, kwa hiyo mashidano kama haya ya "Mkenda Cup" itakuwa ni rahisi serikali kutambua vipaji kwa urahisi zaidi, niwapongeze sana timu zote hasa timu ya Rongai kwa kuchukua ubingwa huu ,"amesema Silinde
Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu nchini, Profesa Adolf Mkenda amesema mashindano hayo ya mechi za kirafiki kwa ajili ya kumpongeza mama Samia Suluhu Hassann ambayo yataitwa "Mashindano ya kirafiki ya mama Samia"yatafanyika katika shule zote na Kata zote za Wilaya hiyo.
"Tunaendelea na mechi za kirafiki kwa kata zote ambazo zitaitwa mashindano ya kirafiki ya Samia"kwa kumshukuru mama yetu Samia kwa mambo mengi aliyoyafanya hapa Rombo,ikiwemo suala la maji ambapo tumepata Sh10 bilioni kwa ajili ya kumaliza changamoto ya maji,"