Shule ya msingi Bunazi Green Acres yapaa

Shule ya msingi Bunazi Green Acres yapaa

Muktasari:

Shule ya Bunazi Green Acre ambayo iko Wilayani Misenyi mkoani Kagera, imeshika nafasi ya pili kitaifa katika mitihani ya darasa la saba baada ya mwaka jana kushika nafasi ya 48 kwa shule ambazo zina  wanafunzi chini ya 40.

Bukoba. Shule ya Bunazi Green Acre ambayo iko Wilayani Misenyi mkoani Kagera, imeshika nafasi ya pili kitaifa katika mitihani ya darasa la saba baada ya mwaka jana kushika nafasi ya 48 kwa shule ambazo zina  wanafunzi chini ya 40.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) nchini Tanzania, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Geofrey Moses amesema licha kupitia changamoto kubwa ya ugonjwa wa Covid-19, wanafunzi walivyorejea baada ya likizo hawakuruhusiwa kurejea nyumbani kkwa mapumziko ya aina yoyote hadi walipomaliza mitihani ya Taifa.

“ Wakati mwingine unakuta wanaamka saa 12:00 asubuhi wanaingia darasani hadi saa 1:00 asubuhi, tumejitahidi sana kuwaandaa wanafunzi tuliwafanyisha mitihani tofautitofauti na tulikuwa tunaitoa maeneo tofauti ya mikoa hapa nchini ikiwemo Arusha, Dar es Salaam, Mara  na tulikuwa na mawasiliano mazuri na walimu wa taaluma wa  hizo shule,” alisema Mwalimu Moses.

Alisema hata walimu pia waliongoza midahalo mbalimbali na wanafunzi ya namna ya kujibu maswali wawapo ndani ya chumba cha mtihani, hali iliyowajengea matumaini ya ufaulu.

Akizungumzia ufaulu huo, Mwalimu wa taaluma shuleni hapo, Derison Deus alisema wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 41 na wote wamepata daraja la kwanza.

Mkoa wa Kagera una shule tatu zilizoingia kwenye kumi bora ya shule zenye mchepuo wa Kiingereza.

Miongoni mwa shule hizo ni pamoja na  Kaizirege iliyopo Manispaa ya Bukoba ambayo imeshika nafasi ya sita, Rweikiza  ya Halmashauri ya Bukoba imechukua nafasi ya saba.