Simba anayedaiwa kula mifugo auwawa

Mbeya. Wananchi wa Mtaa wa Itezi Magharibi jijini Mbeya, wameshirikiana na Askari wa Wanyamapori Wilaya ya Chunya mkoani hapa; kumuua Simba dume aliyekuwa tishio kwenye makazi ya watu huku akirarua na kuu mifugo.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi June 3, 2023 wamesema kuwa kwa kipindi cha wiki moja Simba huyo amekuwa akionekana kwa nyakati tofauti na kuzua taharuki kwa jamii, jambo lililosababisha wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo.

“Licha ya kuzua taharuki, Simba huyo alifanikiwa kuua mifugo kadhaa wakiwepo ng'ombe wawili na Punda mmoja, katika kijiji cha Ilowelo Kata ya Lwanjilo Wilaya ya Mbeya,” imeelezwa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilowelo, Wilaya ya Mbeya vijijini Yona Mbalila amesema kwa kipindi cha siku sita zilizopita baada ya kubaini uwepo wa Simba huyo walitoa taarifa kwa maofisa wanyamapori.

“Huku hofu ikiwa imetanda walianza msako kwa kushirikiana na maofisa hao ndipo walipofanikiwa kumkuta Simba huyo akiwa kwenye moja ya korongo akila mabaki ya mzoga wa punda,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Itezi Magharibi, Mario Paul amesema eneo ambalo Simba huyo amekuwa akionekana ni pori la hifadhi ambapo wanyama wakali wamekuwa wakipita katika njia zake.

“Tuombe maofisa wanyamapori kuendelea kutoa elimu ya kuonyesha mipaka ambayo jamii haipaswi kutumia kwa malisho ya wanyama ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza,” amesema.

Naye Ofisa wanyamapori Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Jacob Mpinga, amesema kuwa kuna changamoto kwa baadhi ya wanyama kutoroka hifadhi kufuata ushoroba maeneo mengine.

“Kimsingi tunashukuru alikuwa bado hajaleta madhara kwa jamii hivyo badaa ya kumuua mzoga wake wake tumeuhifadhi ofisi za maliasili ikiwa kama ni nyara za Serikali,” amesema.

Aidha amewataka wananchi hususan wafugaji kuangalia mazingira rafiki ambayo wanaweza kupeleka mifugo kwaajili ya malisho na siyo mapori hifani hapo, kama njia ya kuepukana na madhara ya wanyama wakali wanaotoroka na kuvamia makazi ya watu na kufanya uharibifu.

Mkazi wa Itezi, Julian Joseph amesema kuwa baada ya kuzuka kwa taharuki ya uwepo wa Simba dume shughuli za kiuchumi zilisimama kwa kuhofia kuliwa ikiwepo kuzuia watoto kuhudhuria masomo.