Simulizi tamu, chungu za vijana wanaopambana kujiinua kiuchumi

Beatrice Mwaringo aliyepewa cherehani na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ofisini kwake Kivule Bombambili jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Ukiacha simulizi ya milima na mabonde aliyopitia Beatrice Mwalingo, mbunifu wa mavazi aliyepewa cherehani na Rais Samia Suluhu HassanaH, kuna simulizi nyingi za vijana wanaopambana kujiinua kuichumi na hatimaye kufanikiwa.

Miongoni mwa vijana hao ni Wilfred Kalunju, aliyejiajiri kwa kufanya biashara za kuuza bidhaa ndogondogo kwenye viunga vya eneo la kupumzikia jijini Dodoma maarufu kama Nyerere Square, huku akiwa na mtaji wa Sh17,000 na sasa kufanikiwa kumuingiza zaidi ya Sh500,0000 kwa mwezi.

Wilfred Kalunju, aliyejiajiri kwa kufanya biashara za kuuza bidhaa ndogondogo kwenye viunga vya eneo la kupumzikia jijini Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Wilfred anasema alipata wazo la kufanya biashara hiyo kutokana na hali ya maisha, baada ya kukatisha masomo yake akiwa kidato cha sita kutokana na ukosefu wa ada na changamoto za kifamilia.

Simulizi ya Kijana aliyejiajiri kwa biashara ya pipi na kupata zaidi ya laki tano

“Ilikuwa mwaka 2020 nilipotakiwa kumaliza elimu ya kidato cha sita, lakini kutokana na kukosekana ada na baadhi ya changamoto za familia ilinilazimu kukatisha masomo na kuanza kufanya biashara, ili kuisaidia familia yangu” anasema Wilfred.

Hivyo, alianza kuuza mitumba, biashara aliyoifanya katika soko la Kariakoo, Mnazi Mmoja na Lumumba, jijini Dar es Salaam. Baada ya kuona biashara hiyo inafanywa na watu wengi na inampa ugumu,  alifikiria kurudi kwao Dodoma na kuanzisha biashara ya tofauti katika eneo alilolikusudia ambalo ni maarufu kama Nyerere Square kwa kuuza chocolate, lipstick na mzani wa kupima uzito.

Anasema biashara yake ina kama miezi tisa sasa, lakini imemuwezesha kufanya kilimo cha biashara ya mahindi na alizeti wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara kwa mtaji aliouwekeza kwa heka tano na kugharimu kama Sh800,000.

Matarajio yake katika biashara ya kilimo kupata mtaji utakaozalisha biashara nyingine ya duka la nguo mkoani Dodoma, pia kununua kiwanja na kufanya mambo mengine ya maendeleo.

Biashara anayoifanya imegeuka kuwa ajira kuu kwake kiasi cha kumuwezesha kuwa na mchango mkubwa kwenye kuwatunza wazazi wake pamoja na kutoa ushauri kwa vijana juu ya fursa ambazo haziitaji mtaji mkubwa, lakini zinaingiza kipato kuliko kukaa kusubiri ajira.

“Vijana wanapaswa kuwa wabunifu wa biashara kulingana na mazingira yanayowazunguka, wasiake bila kujishughulisha,” anasema.

Wilfred anasema biashara anayoifanya haiitaji fremu na mtaji alioanza nao ni mdogo kuliko faida anayoiingiza, katika biashara yake kwa siku anapata faida ya Sh15,000.

Kijana mwingine, Robert Mrema, mwanafunzi wa shahada ya Biashara katika Chuo cha Mwenge Catholic (MWECAU) wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, anajishughulisha na biashara ya kuuza mtumba ya nguo za kike na kiume anazozinunulia katika soko la Memoria lililopo Moshi.

Anasema mtaji wa biashara yake wakati anaanza ulikuwa Sh20,000 ambapo alinunua nguo za kike na kiume kwa Sh1,000 na kisha kuuza kwa Sh2,000,  hivyo kumzalishia Sh20,000 kama faida kwa kila siku. Faida anayoipata inamwezesha kujikimu kimaisha akiwa chuoni na kulipa ada.

Anasema anatumia muda wa jioni kufanya biashara yake, japo nguo huzichukua asubuhi kwa wafanyabiashara wanapofungua mabalo.

“Baada ya masomo napita katika mabweni ya wanafunzi kuuza nguo hizo ambazo huchukua saa mbili kumalizika.

“Mtaji wa biashara yangu ni mdogo, lakini unaniletea faida nzuri, nilianza kuuza nguo nikiwa na Sh 20,000 na kuizalisha hiyo fedha mara mbili kwa kila siku,” anasema.

Robert anaeleza vikwazo anavyokutana katika biashara yake ni kukamatwa na walinzi wa mabweni na wakati mwingine kuzuiwa kufanya biashara ndogondogo kwa sababu za kulinda usalama wa mali za wanafunzi ambao huibiwa na watu kwa kigezo cha kufanya biashara.

Ndoto zake kupitia biashara yake, ni kufungua duka la nguo ili kupata wateja wengi na kukuza mtaji wa biashara yake na hata kutoa ajira kwa watu wengine.

Anawashauri vijana kuwa na uthubutu na kuacha kuona haya kwa watu watamuonaje ukiwa anafanya biashara hiyo.

Kwa upande wake, Anna Joseph maarufu kama ‘Gugu’ mmiliki wa Gugu Beauty Saloon yenye matawi yake Mwananyamala na Kinondoni, jijini Dar es Salaam anasimua safari ya biashara yake.

Mmiliki na mwanzilishi wa Gugu Beauty Saloon, Anna Joseph

Akizungumza na Mwananchi Digitala, anaeleza safari yake ya utafutaji ilianza akiwa anasoma shahada ya biashara katika chuo cha CBE, jijini Dar es Salaam mwaka 2018.

Anasema alianza kufanya kazi za promo, ilikuwa kama masihara kutokana na kujaribu biashara mbalimbali ikiwemo kuuza nguo, mkaa, kilimo na ufugaji bila kupata matokeo yoyote zaidi ya hasara.

Hakukata tamaa, japokuwa familia yake ilimtaka kwenda kujiunga na Jeshi la Ulinzi, kitu ambacho hakuwa tayari na ndipo karata yake ya mwisho akaamua kuitupa katika ususi wa nywele baada ya kupata vifaa kwa gharama ya 2,000,000 ambayo aliilipa kidogo kidogo.

“Haikuwa rahisi kufanya biashara hiyo kwa kuwa sehemu niliyofungua fremu ya ususi kulikuwa na saluni nyingine,” anasema.

Hali hiyo ilimfanya kuja na mbinu ya kusuka kwa gharama ya chini akiwana kaulimbiu ya ‘kila kitu kwake’ kitu kilichowavutia wateja wengi.

Njia hiyo imemuwezesha kukuza biashara yake inayotoa ajira za wasusi wasiopungua 40 ambao nao wana wasusi wasaidizi wanaowalipa.

Anawashauri watu kutoogopa pale wanapotaka kufanya biashara, wajaribu kutumia mbinu zinazoweza kuwapa matokeo chanya, japo yanaweza kuwa si ya haraka kama wanavyotarajia na pia uvumilivu unahitajika.

Kupitia simulizi hizo, baadhi ya wasomi na wanasaikolojia wameeleza njia ambazo mtu anaweza kuzitumia kufikia mafanikio katika maisha.

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude anasema simulizi ya Beatrice Mwalingo jambo kubwa linalodhihirisha mafanikio yake imetokana na uthubutu kuanzia kusafiri kutoka Tunduma hadi Dar es Salaam, pia kwenda nchini Japan bila kuwa na uhakika kama atafanikiwa.

Lakini kwa sababu aliona hiyo ni njia ya kufikia mafanikio alitubutu na kuamua kutafuta ujuzi kwa kujifunza kupitia mtandao na ujuzi huo kuufanya kuwa biashara.

Ushauri anaoutoa kwa vijana wa Tanzania wanaojaribu lakini wanakwama, wazingatie mambo yatakayowawezesha kufikia mafanikio ya kiuchumi na kimaisha ikiwamo kwanza watafute ujuzi kwa kuingia darasani au viwandani wakiwa na uthubutu.

Mtaalamu huyo anasema watu wengi wanafikiri ili uweze kufanya biashara lazima upate fedha nyingi, jambo ambalo halina uhalisia,  bali wanapaswa wawe wabunifu katika kutimiza ndoto zao.

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya (MZRH) kitengo cha saikolojia tiba, idara ya afya ya akili, Yisambi Mbuwi anaeleza katika hali ya kawaida mwili wa binadamu unaweza kuvumilia shuruba na changamoto za aina yoyote, lakini ni ngumu kuishawishi akili kukubali hizo changamoto, hali inayosababisha watu kushindwa kufikia ndoto zao.

Yisambi anaeleza uthubutu ni silaha kufikia mipango ya mafanikio, akitolea mfano wa Beatrice aliyeonyesha uthubutu kwa kumtumia Rais Samia ujumbe katika mtandao wa kijamii bila kujua kama atajibiwa.

Pia uthubutu alioana wa kufanya ubunifu wa mavazi unaomuwezesha kufikia ndoto alizojiwekea.

Anasema kisaikolojia ili ufanikiwe ni lazima uwe na uthubutu wa kufanya kile unachokusudia, jitihada, ujasiri na uvumilivu pale inapotokea mtu akakutana na changamoto mbalimbali.

Yisambi anashauri pia malezi kuwa sehemu tiba ya kisaikolojia kwa watoto, kwani itawaandaa vyema kukabiliana na changamoto mbalimbali.