Simulizi waliofunga ndoa uzeeni

Muktasari:
- Mwishoni mwa mwaka jana ndipo Kiwia alimfahamu Christina, lakini stori iko tofauti upande wa mwanamke huyo. Yeye alianza kumfahamu mwaka 1975 akiwa mwanafunzi wa Sekondari Kazima iliyopo mkoani Tabora. Wakati huo Kiwia alishaanza kutoa huduma ya mahubiri hivyo, alikwenda shuleni hapo katika mkutano wa injili.
Dar es Salaam. “Mimi naona kama Mungu amenipa mke mzuri hata kwa sura na umbo nafikiri ‘nimewin’ kweli kweli lakini hilo sio tu lililonivuta kwake, bali ni mwanamke wa aina yake.”
Hivyo ndivyo Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Pugu Kajiungeni, Dk Christian Kiwia (72) alivyoanza kumzungumzia mkewe Christina Teemba (66).
Wawili hawa ni wanandoa wapya ambao wameingia kwenye taasisi hiyo Februari 6 mwaka huu, ikiwa ni ndoa ya kwanza kwa Christina na ya pili kwa mchungaji Kiwia.
Dk Kiwia na mkewe wa kwanza walikuwa wakiishi Marekani kwa zaidi ya miaka 20 na hata kifo cha mwenza wake huyo kilitokea wakiwa huko hivyo, alilazimika kusafirisha kurejea nchini kwa mazishi yaliyofanyika Moshi.
Mchungaji huyo ambaye ni baba wa watoto watatu anasema alivutiwa kumuoa Christina (aliyekuwa akiishi Moshi) baada ya kusikia taarifa zake kuwa amekulia kanisani na anazeeka ikiwa hajawahi kuolewa wala kupata mtoto. Habari hizo alizipata ikiwa ni miezi michache baada ya kwenda Moshi kwenye shughuli mazishi ya mkewe wa kwanza aliyedumu naye kwa miaka 48.
“Nilijiuliza huyu atakuwa mtu wa aina gani yaani ni mcha Mungu, anahudumia kanisani hajawahi kuolewa wala kupata mtoto. Wenzake wanaolewa wanazaa. “Kanisa alilokuwa anahudumia ndipo ilipofanyika ibada ya kumuaga aliyekuwa mke wangu, ikabidi niombe kibali cha kuzungumza naye kutoka kwa mchungaji wake,” anasema.
Ombi hilo lilikubaliwa na hatimaye Kiwia na Christina wakakaa chini kuzungumza, hata hivyo mambo hayakuwa rahisi, lakini mchungaji hakukata tamaa alimfuata tena na tena.
Christina alikuwa amejiwekea nadhiri kuwa hatoolewa, maisha yake amejitoa kwa kanisa na kumtegemea Mungu kama kiongozi wake maishani.
Kwanini aliweka nadhiri hiyo
Hili ndilo linaweza kuwa swali kubwa kwanini aliamua hivyo na aliwezaje kufanikisha lengo lake hadi kufikia kuolewa akiwa na miaka 66.
Christina anasema akiwa mwanafunzi wa sekondari aliokoka jambo ambalo lilipingwa vikali na familia yake hadi kufikia hatua ya kutengwa. Pamoja na nguvu kubwa ya familia alisimamia uamuzi wake na kujikuta akitofautiana na baba yake.
Alipomaliza alirejea nyumbani na wachumba wakaanza kujitokeza kwa lengo la kumuoa. Kama ilivyo tamaduni za kiafrika washenga walipita kwa baba yake ila mambo yakawa tofauti.
“Unajua mimi nilikuwa nimeokoka kwahiyo hata wale wachumba waliokuwa wanakuja nilishindwa kuwakubali kwa kuwa hawakuwa karibu na Mungu. Mara zote nilikataa hadi baba yangu akakasirika, ikafika hatua hata waliokoka walikuwa wanakuja, ila nikaendelea kushikilia msimamo wangu. Nikaona nisimyumbishe baba yangu, nikamwambia wazi mimi sitoolewa,” anasema Christina.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa na akaishi kwa miaka 65 hatimaye maneno hayo yamefutika mwaka huu baada ya kutua mikononi mwa Mchungaji Kiwia.
Kama ilivyo tamaduni za kiafrika hususan Wachaga, Christina alitolewa posa kisha mahari kwa sherehe ya kitamaduni ilifanyika mjini Moshi. Pamoja na umri wake kuwa mkubwa familia yake ilimfanyia sherehe ya kumuaga (Sendoff)na siku ikawadia akiwa ndani ya shela alifunga ndoa iliyofuatiwa na sherehe iliyofanyika katika Kanisa la TAG Pugu Kajiungeni.
Baada ya sherehe hiyo wawili hawa walikwenda fungate na hata mahojiano haya yamefanyika ikiwa ni siku ya tano tangu wafunge ndoa.
Ilikuwaje akamkubali mchungaji
Christina ambaye kwa umri wake tunaweza kumuita bibi, anasema wakati wote wa usichana wake alikuwa akishuhudia wenzake wakiolewa na kupata watoto lakini yeye hakutamani.
“Tangu nilipomtamkia baba yangu kuwa siolewi, sikuwahi kutamani kuolewa wala kupata mtoto. Nilikuwa nafurahia rafiki zangu wakiolewa ila binafsi sikuwa na matamanio hayo.”
Anasema Mchungaji Kiwia alimfuata mara tatu kumueleza dhamira yake ya kumuoa, lakini msimamo wake ulikuwa ule ule kwamba hataki kuolewa.
“Siku moja nikiwa nimelala nikasikia sauti ikiniambia kwamba nimemtuma mtumishi wangu kwanini hutaki kuelewa, nilishtuka nikajiuliza hiki nini, nikagundua ni sauti ya Mungu. “Kulipokucha nilimpigia simu baba mchungaji, nilimuomba anisahemehe na kukubali ombi lake kisha taratibu zikaanza hadi tulipofikia hatua hii amekuwa mume wangu,” anasema Christina.
Mchungaji Kiwia anasema ni kusudi la Mungu kumkutanisha na mwanamke huyo, ambaye maisha yake yote amekuwa akimtumikia.
“Nimetafakari sana ukuu wa Mungu juu ya mwanamke huyu, katika umri wa miaka 66 hajawahi kuzaa wala kuguswa na mwanaume ni kitu cha aina yake na ninachoshukuru zaidi ndiye mwanamke nitakayemaliza naye safari yangu ya maisha hapa duniani,” anasema huku akionyesha tabasamu kwa mkewe.
Walikutana vipi
Mwishoni mwa mwaka jana ndipo Kiwia alimfahamu Christina, lakini stori iko tofauti upande wa mwanamke huyo. Yeye alianza kumfahamu mwaka 1975 akiwa mwanafunzi wa Sekondari Kazima iliyopo mkoani Tabora. Wakati huo Kiwia alishaanza kutoa huduma ya mahubiri hivyo, alikwenda shuleni hapo katika mkutano wa injili.
Christina alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliohudhuria mkutano huo na ndio ikawa mara yake ya kwanza kumuona mwanaume huyo, ambaye kwa sasa ni mume wake.
Haikuishia hapo miaka ya 80 Dk Kiwia alikwenda kununua dawa kwenye duka la dawa, muuzaji alikuwa Christina, hilo pia halikuwafanya wawe karibu kwani mchungaji alikuwa na mkewe na bibie alikuwa akiendelea na nadhiri yake.
Familia zimepokeaje ndoa hii
Kwa Christina ndugu zake wamepokea kwa mikono miwili wakifurahia hatua hiyo kwa kuwa hakuna aliyetegemea kwamba, kuna siku bibi huyo angeolewa tena kwa sherehe.
Mambo yapo nusu nusu kwa upande wa Mchungaji Kiwia kwani, kati ya watoto wake watatu ni mmoja ndiye ameelewa na kushirikiana nao bega kwa bega katika maandalizi ya harusi hiyo.
“Mtoto wangu wa kwanza ana miaka 47, ameelewa na kushirikiana nami, hawa wengine wadogo kuna wa miaka 27 na 23 bado wanamlilia mama yao na kiukweli nawaelewa ila hawana tatizo tunazungumza,” anafichua Mchungaji Kiwia.
Anasema aliamua kuoa kwa sababu ya huduma anayofanya, kwani aliona si sawa kwa mchungaji kuishi bila mama mchungaji. Baada ya kifo cha mkewe aliyemuuguza kwa miaka 27 na kutafakari kuhusu umri wake, aliona kuna haja ya kupata mwenza ambaye atakuwa akimsaidia kwa mambo mbalimbali kuanzia kwenye kazi yake hadi maisha ya kila siku. “Niliona umri niliofikia nahitaji kumaliza vizuri maisha yangu kwa kuwa najua kama nimeishi sana ni miaka 80, sikutaka miaka yangu iliyobaki duniani iende hovyo, nilihitaji mtu wa kunihudumia na huyu ni mwanamke sahihi,” anasema Dk Kiwia.
Ushauri wao kwa vijana
Christina anawataka mabinti kutafakari kwa kina kabla ya kufikia uamuzi wa kuolewa na sio kukurupuka. “Sijui shida ni nini watoto wa siku hizi hawashauriki, wanakurupuka kwa kuangalia vitu kama fedha au hata uonekane tu umeolewa. Kuolewa kunahitaji neema ya Mungu,”
Dk Kiwia yeye anasema na watoto wa kiume, “Mungu hawai wala hachelewi, msiangalie umbo wala sura, mshirikishe Mungu katika kufanya maamuzi hususan haya muhimu ya kwenda kuchagua mwenza wa maisha.”
Itaendelea kesho