Prime
Sintofahamu kujengwa ukuta kuzingira nyumba, kuzibwa barabara
Muktasari:
- Kwa mujibu wa wananchi hao, nyumba zao zimejumuishwa ndani ya ukuta uliojengwa na mmiliki wa shule binafsi, huku barabara ya umma nayo ikizibwa
Kahama. Maswali yasiyo na majibu yanaumiza vichwa vya wananchi kadhaa wa Mtaa wa Kitwana, Kahama mkoani Shinyanga, baada ya kukuta nyumba zao zimezungushiwa ukuta, huku baadhi wakitakiwa kuzihama.
Kwa mujibu wa wananchi hao, nyumba zao zimejumuishwa ndani ya ukuta uliojengwa na mmiliki wa shule binafsi, huku barabara ya umma nayo ikizibwa.
Wananchi hao wanasema yote hayo yanafanyika bila kupewa taarifa wala kufuatwa taratibu za kisheria, jambo lililoibua mgogoro kati yao na mmiliki wa shule hiyo inayojengwa, Steven Nyeriga.
Jana, Julai 3 2026 akizungumzia madai hayo, Nyeriga amesema kabla ya kuanzishwa kwa shule hiyo kulikuwa na majirani waliomiliki maeneo yanayozunguka eneo hilo.
Msingi wa nyumba wa Emanuel Godfrey uliozungushiwa ukuta na mmiliki wa shule ya kibinafsi Steven Nyeriga katika mtaa wa Kitwana kata ya Busoka Manispaa ya Kahama, wakati akiendelea na ujenzi.
Amesema baadhi ya maeneo hayo yaliuzwa baadaye kupitia madalali, ndipo changamoto mbalimbali zilipoanza kujitokeza.
Mgogoro huo ulianza kufukuta mwanzoni mwa mwaka huu, ukihusisha wakazi wa eneo hilo na Nyeriga, ambaye pia ni Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Neema Magoti, ni miongoni mwa waathirika amesema nyumba yake imo ndani ya ukuta na anapata hofu kama atanyang’anywa au vinginevyo.
Amesema nyumba hiyo, ameijenga kwa fedha alizozipata kupitia biashara ya mbogamboga.
Magoti amesema aliamua kuwekeza katika nyumba hiyo baada ya miaka mingi ya kujituma, akiamini eneo alilonunua lilikuwa salama na halikuwa na mgogoro wowote wa umiliki.
Hata hivyo, wakati akiendelea na ujenzi, amedai alifuatwa na mtoto wa Nyeriga aliyemtaka ahame ili kupisha eneo la shule.
“Alinipeleka kunionesha eneo lingine lakini sikuridhika nalo. Ni majaruba ya mpunga, liko mbali na thamani yake haiwezi kulinganishwa na eneo langu,” amesema Magoti.
Amesema eneo alilooneshwa halikuwa na miundombinu wala mazingira yanayofanana na kiwanja chake cha sasa alichokinunua kwa gharama kubwa.
“Hapa nilinunua kiwanja kwa Sh2 milioni. Kule thamani yake hata haifiki hapo. Haiwezekani mtu akupangie tu mahali pa kuishi bila makubaliano,” amesema.
Magoti, amesisitiza kuwa hakupinga kuondoka iwapo taratibu za kisheria na haki vingezingatiwa na kila upande kuheshimiwa.
“Sikukataa kuondoka. Nilichotaka ni haki. Kama wanataka nichukue eneo lingine, basi nifanyiwe tathmini na nilipwe stahiki zangu,” amesema.
Boma na nyumba za wakazi wa mtaa wa Kitwana zilizozungushiwa uzio wa ukuta bila ridhaa yao na mmiliki wa shule ya kibinafsi Steven Nyeriga.
Amesema kama angekubali kujengewa nyumba nyingine, angependa apewe nafasi ya kushiriki katika uamuzi unaohusu mali yake.
“Lakini sasa tumewekwa ndani ya uzio wao na barabara imefungwa. Hilo ndilo linatuumiza zaidi,” amesema Magoti.
Yohana Umoja, mwalimu wa Shule ya Sekondari Malunga amesema alijenga nyumba kwa ajili ya familia yake, lakini nayo kwa sasa ipo ndani ya ukuta wa shule hiyo.
Amesema alinunua kiwanja baada ya kuoneshwa mipaka na barabara zilizotengwa kwa matumizi ya wananchi, jambo lililompa uhakika wa kuanza ujenzi.
Wakati akikamilisha nyumba yake, amesema hakukuwa na uzio wowote katika eneo hilo wala dalili za kuwepo kwa mgogoro wa ardhi.
Amesema baadaye alipigiwa simu na kuambiwa nyumba yake imezungushiwa ukuta huku njia ya kuingia na kutoka ikiwa imefungwa.
Amesema alipohoji sababu za hatua hiyo, alishauriwa kukubali kuhamia eneo mbadala ambalo hakuridhika nalo.
“Mimi nilisema kama wanahitaji eneo langu, basi wanilipe fidia ili nikatafute sehemu nyingine. Sikukubaliana na eneo walilonionesha,” amesema.
Umoja amedai alipinga hatua hiyo kwa sababu aliamini alikuwa amepata eneo lake kwa kufuata taratibu zote zinazotakiwa.
Amesema baada ya kulifikisha suala hilo kwa viongozi wa mtaa na kata, vikao vya usuluhishi vilifanyika lakini havikufikia mwafaka.
Mwananchi mwingine, Emmanuel Godfrey, amesema alinunua kiwanja chake mbele ya viongozi wa eneo na kupewa nyaraka za umiliki.
Amedai baada ya muda aliporejea kukagua eneo lake, alikuta limezungushiwa uzio wa ukuta bila yeye kupewa taarifa yoyote.
Godfrey amesema kilio kikubwa cha wananchi ni kuona watu waliopata maeneo yao kihalali wakikosa uhakika wa hatima ya mali zao.
“Mtu amenunua kiwanja kwa fedha zake na ana nyaraka za umiliki. Kama kuna sababu ya kuchukua eneo hilo, basi taratibu za kisheria zifuatwe,” amesema.
Amesema wananchi walijaribu kutafuta suluhu katika ngazi mbalimbali lakini walikata tamaa baada ya kuona hakuna hatua ya haraka iliyokuwa ikichukuliwa.
Hatimaye waliamua kufikisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama wakiamini ofisi hiyo ingeweza kusaidia kutatua mgogoro huo.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kitwana, Clement Steven amekiri kupokea malalamiko hayo na kuanza kuyafanyia kazi.
Amesema kwa muda mrefu eneo la shule halikuwa na mgogoro wa umiliki kwa mujibu wa taarifa zilizokuwa zikifahamika katika ofisi ya mtaa.
Amesema changamoto ilijitokeza baada ya kuanza kwa ujenzi wa uzio unaodaiwa kuingia katika eneo la barabara ya wananchi.
“Mimi nilimwelekeza kwamba mbele pale kuna barabara. Nilimwambia akijenga uzio wake aache nafasi ya wananchi kupita kuelekea makazi yao,” amesema.
Kiongozi huyo amesema ushauri huo haukuzingatiwa na kusababisha malalamiko kuendelea kuongezeka.
“Akajenga tu akaziba barabara na nyumba za wengine kazijengea humu ndani. Hapo ndipo mgogoro ulipoanza kuwa mkubwa,” amesema.
Amesema vikao vilivyowashirikisha viongozi wa kata na maofisa wa ardhi viliitishwa ili kutafuta ukweli wa jambo hilo.
Licha ya jitihada hizo, amesema hakukuwa na mwafaka wa haraka uliofikiwa kati ya pande zinazohusika.
Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kahama, Evarist Lameck amesema Nyeriga anamiliki viwanja namba tatu na nne vilivyopimwa rasmi.
Amesema kama alinunua maeneo mengine nje ya hayo, alipaswa kuwasilisha nyaraka zake katika idara ya ardhi kwa ajili ya uhakiki na upimaji.
“Hakuna utaratibu unaoruhusu kufunga barabara ya umma, na sisi Manispaa ya Kahama hatujatoa kibali cha kujenga ukuta huu,” amesema.
Akizungumza na wakazi wa eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amemwagiza mmiliki wa shule hiyo kuondoa ukuta uliokuwa umejengwa katika eneo la barabara.
“Ndani ya saa nane kuanzia sasa (juzi) ukuta huo uwe umeondolewa. Ikifika muda huo na haujaondolewa, tutakuja tubomoe wenyewe,” amesema.
Nkinda amesema wananchi waliopata maeneo yao kwa kufuata taratibu za kisheria hawapaswi kubugudhiwa wala kulazimishwa kuondoka.
“Wananchi hawa hawakuiba maeneo haya, bali wamenunua kwa kufuata taratibu. Kama kuna mtu anataka waondoke, basi afuate sheria,” amesema.
Ameonya kuwa uwezo wa kifedha wa mtu hauwezi kuwa sababu ya kuwaonea wananchi au kuwanyang’anya haki zao.
Amesisitiza kuwa, migogoro yote ya ardhi inapaswa kutatuliwa kwa kuzingatia sheria, ushahidi na maelekezo ya wataalamu husika.