Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri Jimbo Katoliki Moshi kupata mapadri 18

Muktasari:

  • Wakati mapadri 18 kutoka Jimbo Katoliki la Moshi wakipata daraja la upadri, maadili, malezi imara ya familia, elimu na sala vimetajwa kuwa siri ya mafanikio ya kanisa hilo kuendelea kuvuna mapadri wengi zaidi.

Moshi. Jimbo Katoliki la Moshi mkoani Kilimanjaro limepokea mapadri 18 waliopanda daraja kutoka kuwa mashemasi, huku ikielezwa kuwa maadili, malezi imara ya familia, elimu na sala ndio siri ya mafanikio ya kanisa hilo kuvuna mapadri wengi zaidi.

Viongozi hao ambao 15 ni wa jimbo hilo na watatu ni wa shirika, walipata daraja la upadri Januari 9, mwaka huu katika Parokia ya Kristo Mfalme katika misa takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo pamoja na Askofu wa jimbo hilo, Askofu Ludovick Minde.

Idadi hiyo ya viongozi 18  waliopata daraja la upadri kwa mwaka huu inaonekana kuwa kubwa ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo waliopata daraja hilo walikuwa 12 na mwaka 2023 walikuwa wanane.

Akizungumzia siri ya jimbo hilo kuendelea kupata mapadri wengi zaidi, Padri Aidan Msafiri ametaja mambo manne yaliyowezesha mafanikio hayo.

Amesema mchakato wa kuwapata mapadri unatokana na msingi imara kuanzia kwenye malezi ya familia.

"Kuwapata mapadri ni mchakato mkali wa sala na kiimani na ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kwamba anatengenezwa na familia iliyo imara kiimani na kimaadili," amesema Padri Msafiri

Amesema viongozi wa kanisa hilo wanatengenezwa katika msingi imara wa elimu bora kuanzia wakiwa darasa la awali mpaka seminari kuu, hivyo kwao maadili ni jambo muhimu.

"Mapadri hutengenezwa na walezi katika elimu na wanakuwa wamesoma sana, shule ambazo hazitoi elimu nzuri haziwezi kutoa mapdri wa baadaye, hivyo tunawapatia elimu bora na sio bora elimu, maana  elimu ikiharibiwa pia usitegemee kupata mapadri bora, maadili ni jambo muhimu," amesema Padri Msafiri.

Ameitaka jamii kuendelea kuwasaidia wale wenye wito katika jamii na hawana msaada ili baadaye jamii iweze kuwa na mapadri wengi na wema.

"Mapdri wanatokana na matoleo ya watu wengi, kuna vijana wengi wana miito lakini hawapati watu wakuwasomesha, ni wakati wa wale wenye mapenzi mema kuangalia wale ambao hawana uwezo wa kifedha wa kuweza kwenda kusoma seminari ili baadaye tuweze kuja kuwa na iwengi na wema," amesema.

Akizungumza na mapdri hao wapya, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka mapdri vijana kuwa tayari wakati wowote kwenda kufanya kazi za kitume katika vituo vya kazi wanavyopangiwa.

Aidha, amewataka mapadri hao kuwa mfano mzuri wa kanisa na kutenda sawa sawa na utume wao ili kuondoa malalamiko katika jamii au wanakopangiwa.

Pamoja na mambo mengine, alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wachaga kwa moyo wa kujitolea katika shughuli mbalimbali za kanisa ambazo zimeliwezesha kanisa hilo kusimama na kujitegemea.

"Nimeishi na nimefurahi sana kuwa na Wachaga kule Dar es salaam na hao wamenisaidia sana kusimamisha jimbo kule kwa mpango huu mnaoufanya wa kusaidia kwa kila hali ili kanisa letu lijitegemee.

"Kama Askofu wa Dar es Salaam kwa karibu ya miaka 30 sijawahi kusikitika kuwa na Wachaga, ninaowaamini wanaoendesha kanisa kule Dar es salaam," amesema.