Siri katika maombi ya kujivika silaha za Mungu
Mwalimu Tuntufye Mwakyembe.
Bwana Yesu asifiwe. Mungu ametupa nafasi tena kutafakari neno la Mungu. Somo hili ni mwendelezo wa Jumapili wiki iliyopita na tunahitimisha leo. Tunapaswa kumshukuru na kumtegemea yeye peke yake kwa njia mojawapo kama kutafakari neno lake. Tafakari yetu itatuongoza kwenye mstari unaosema;
“Kwa maana kushindana kwetu si juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa Roho.” Waefeso 6:12
Zipo aina mbalimbali za maombi katika maisha ya Mkristo, lakini leo tunaangazia maombi ya kushindana, yaani maombi ya vita vya kiroho. Haya ni maombi yanayomfanya mwamini asimame dhidi ya kazi za giza na kuutetea ufalme wa Mungu katika maisha yake. Mtume Paulo katika Waefeso 6:12 anatumia neno “kushindana,” akionyesha kuwa maisha ya kiroho yana mapambano. Pia katika Waefeso 6:13 anaendelea kusisitiza umuhimu wa kuvaa silaha zote za Mungu ili kuweza kushindana siku ya uovu. Kadhalika, Ufunuo 12:11 unasema, “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo, na kwa neno la ushuhuda wao.” jambo linaloonyesha kuwa kulikuwa na mapambano na ushindi ulipatikana kupitia nguvu za Mungu.
Maana ya kushindana
Neno kushindana lina maana ya kupambana, kuvutana, kwenda kinyume na kutokukubaliana. Katika ulimwengu wa roho, Mkristo amewekwa katika nafasi ya kupinga kazi zote za adui zinazolenga kuharibu maisha yake. Biblia inaeleza kuwa tunashindana na falme, mamlaka, wakuu wa giza pamoja na majeshi ya pepo wabaya.
Hizi ni ngazi za kiroho zinazotawala upande wa giza, huku chini yake kukiwa na mawakala wao wanaotekeleza kazi hizo duniani kama wachawi, washirikina, waganga, waaguzi, wapiga ramli na wengineo.
Sababu za kufanya maombi ya kushindana
Maombi haya yanafanyika kwa lengo la kuzuia uharibifu, mauti, magonjwa pamoja na utendaji wa nguvu za giza katika maisha ya watu. Yohana 10:10 inasema, “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Hivyo basi, maombi ya kushindana ni maombi ya kupinga, kukataa, kwenda kinyume, kutokukubaliana na kuzuia mipango yote ya adui dhidi ya maisha ya Mkristo.
Ufalme wa Mungu na nguvu ya maombi
Mathayo 11:12 inasema, “Tangu siku za Yohana mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.” Waamini ni wana wa ufalme wa Mungu na baraka zao zimefungwa katika namna ya kifalme. Mungu anatarajia watoto wake walete mambo ya ufalme wa mbinguni katika mifumo yao ya maisha ya kawaida. Kwa sababu hiyo Mungu ametupatia funguo za ufalme wa mbinguni. Mathayo 16:19 inasema, “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa na mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Kupitia maombi, Mkristo anaweza kufunga na kufungua mambo katika ulimwengu wa roho na kuona matokeo yake katika maisha ya kawaida.
Kwa nini Mkristo anahitaji nguvu za Mungu?
Kuna ufalme wa giza ambao kazi yake ni kupambana na ufalme wa Mungu. Ndiyo maana Mkristo anahitaji nguvu za Mungu kwa njia ya maombi ili kuwazuia wanaomzuia, kuwabatilisha wanaompinga, kuwapiga wanaompiga, kuwavuruga wanaomvuruga, kuwapangua wanaompangua pamoja na kuwateketeza wanaomteketeza. Haya yote yanafanyika kwa mamlaka ya Mungu dhidi ya kazi za ufalme wa giza.
Maombi ya kushindana ni maombi ya aina gani?
Haya ni maombi ya kujivika nguvu za Mungu na kuziachilia ili kuleta matokeo, maombi ya kutangaza vita dhidi ya ufalme wa adui, maombi ya kuzuia adui kutawala maisha ya mtu pamoja na maombi ya kulinda maendeleo na mifumo ya kiuchumi ya mwamini.
Mamlaka ya Mkristo katika vita vya kiroho
Yeremia 1:10 inasema, “Angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa na kubomoa na kuharibu na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.” Mungu amempa kila aaminiye mamlaka ya kung’oa mapando ya adui, kubomoa yaliyojengwa na adui, kuharibu kazi za ibilisi, kujenga ufalme wa Mungu na kupanda vitu vya ufalme wa Mungu mahali alipo.
Maombi ya kushindana ni sehemu muhimu ya maisha ya Mkristo. Ni maombi yanayompa kila anayeamini uwezo wa kusimama dhidi ya nguvu za giza na kuleta ushindi wa Mungu katika maisha yake. Mkristo anatakiwa kuwa na nguvu za Mungu kupitia maombi ili kuweza kufunga na kufungua, kushinda vita vya kiroho na kuona ufalme wa Mungu ukidhihirika katika maisha yake ya kila siku.
Mungu Mwenyezi akubariki na kukutunza uishi katika misingi hii kwa kumaanisha ili uweze kushinda mitego ya audi. Kwa kufanya hivyo utastawi kiroho, kiimani hata kiuchumi. Amen
Kwa maombi na ushauri Mwalimu Tuntufye Mwakyembe anapatikana jijini Arusha kwa simu 0767629562