Siri mwanafunzi anayesoma  Veta kupatiwa ajira na mbunge

Mwanafunzi wa fani ya ufundi bomba katika Chuo cha Veta Mwanza, Leticia Charles (aliyeshikilia maiki katikati) akitoa maelezo kuhusu mafunzo ya ufundi bomba wanayopatiwa chuoni hapo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Leticia amepatiwa ajira na Mbunge wa Kwimba mkoani Mwanza, Shanif Mansoor baada ya kuonyesha weledi wa kufafanua nadharia na vitendo wanachofundishwa. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Mbunge wa Kwimba, Shanif Mansoor ametangaza ajira kwa mwanafunzi Leticia Charles wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilipofanya ziara katika chuo cha Veta Mwanza, kukagua utekelezaji wa ‘mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa njia ya uanagenzi’.

Mwanza. “Mungu hamtupi mja wake.” Ndiyo msemo unaoweza kuutumia kuelezea kisa cha Leticia Charles (25), mwanafunzi wa fani ya ufundi bomba katika Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) kilichopo Nyakato jijini Mwanza aliyepewa ajira na Mbunge wa Kwimba (CCM) Shanif Mansoor.

Mansoor ametangaza ajira kwa Leticia leo Jumanne Machi 19, 2024, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilipofanya ziara Veta Mwanza kukagua utekelezaji wa ‘Mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa njia ya uanagenzi’ yanayotekelezwa na Veta kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu.’

 Huku akionekana mwenye kujiamini, Leticia alikabidhiwa jukumu la kuwasilisha mbele ya kamati hiyo walichojifunza kwa kipindi cha mwezi mmoja kwa niaba ya wenzake 24, ambapo amewaelezea wajumbe wanachofundishwa kwa nadharia na vitendo jambo lililomvutia Mansoor na kumpatia ajira hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital baada ya kupewa ajira hiyo, Leticia ambaye ni mtoto wa pili kati ya watatu waliozaliwa katika familia ya marehemu, Charles Ng'waya na Sophia Ladislaus waliofariki mwaka 1998 na 2005, amesema pamoja na kusoma ufundi huo hakutarajia kupata ajira akiwa bado masomoni.

Anasema baada ya wazazi wake kufariki dunia, familia yake ilibaki chini ya uangalizi wa mama yake mdogo aliyemtaja kwa jina la Leonida Ladislaus ambaye alibeba jukumu la kumsomesha hadi kidato cha sita.

Hata hivyo, amesema fedha za kumfanya atimize ndoto ya kusoma kozi anayoipenda ya Sayansi ya Chakula, haikupatikana. 

“Nilihitimu darasa la saba Shule ya Msingi Ng'wamagoli (2012), nilijiunga na Sekondari ya St Joseph iliyoko Kata ya Pamba jijini Mwanza mwaka 2016, nikafaulu na kwenda kusoma kidato cha tano Mwanza Sekondari na kuhitimu mwaka 2019. Baada ya kuhitimu nilipata daraja la tatu. 

“Nilipomaliza kidato cha sita nilikaa nyumbani kwa miaka minne nikipambana na maisha kwa sababu mama mdogo hakuwa na uwezo wa kunigharamia masomo. Niliposikia Waziri ametangaza nafasi ya mafunzo Veta, nikaomba kujiunga na Veta Mwanza Februari 22, mwaka huu,” amesema.

Kwa mwezi mmoja aliosoma kozi yake ya fundi bomba, amesema ameweza kufunga na kufungua mabomba, kutengeneza mita za maji, usalama wa kazi na utengenezaji wa vipuli vinavyotumiwa katika miradi ya maji. 

“Sikutarajia kupata ajira baada ya kuhitimu japo nilitegemea kupata ujuzi utakaoniwezesha kujiajiri mtaani. Namshukuru Mungu na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa nafasi kwa vijana na mbunge Mansoor kwa kunipa ajira. Itanisaidia kupata kipato na kuisaidia familia yangu ambayo inanitegema,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge Mansoor alipoulizwa kama alikuwa anafahamu mwanafunzi huyo ni yatima, amesema alikuwa hafahamu chochote.

“Sikujua kwamba yule binti ni yatima niliona ana sifa, bidii, alivyochangamka na alivyojitambulisha kwetu pale nimevutiwa, nikaona anastahili kupata kazi, akishapata ujuzi atakuja kwenye kampuni yangu kupatiwa uzoefu kisha tutamuajiri jumla,” amesema Mansoor.

Kutokana na hilo, amesema akihitimu mafunzo yake Julai 27, mwaka huu, atamuajiri kwenye Kampuni yake ya uchimbaji madini huku akidokeza kuwa amevutiwa na mafunzo yanayotolewa chuoni hapo kwa kile alichodai wanafunzi wanatengenezwa kwa weledi wa nadharia na vitendo.

Hivyo, mbunge huyo ameitaka Serikali kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kutengeneza ajira, vifaa na mtaji kwa vijana wanaosomea ujuzi mbalimbali katika vyuo vya Veta.

Amesema kupitia mafunzo hayo, Serikali itapunguza kundi kubwa la vijana wanaohitimu na kukosa ajira.

“Leo nimetoa ajira kwa vijana wawili akiwemo huyo binti ambaye nimemtaja moja kwa moja, hiyo nyingine tutaangalia namna ya kumpata mwingine. Pia nimeongea na Mkuu wa Chuo cha Veta Mwanza tuwasiliane kwa sababu ninatarajia kutoa ajira 70 kabla ya Oktoba mwaka huu, naamini wengi nitawatoa hapa,” amesema.

Mwalimu wa fani ya Bomba chuoni hapo, Julius Ndagani amesema uamuzi wa Mansoor kutangaza ajira kwa mwanafunzi huyo siyo tu unaonyesha namna Veta inavyoaminika, pia unaashiria kuthamini wanafunzi wanaosoma katika taasisi za Serikali. 

“Nimejisikia furaha na amani na nimeamini leo kwamba kumbe wanafunzi wanaelewa kile tunachowafundisha. Vyuo vyetu vya Serikali vinatoa elimu bora ukishuhudia wanafunzi wamefundishwa kwa mwezi mmoja tu lakini ukiwaangalia wanaweza kuajiriwa,” amesema Ndagani.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Veta Mwanza, Lupakisyo Mapamba ameishukuru kamati ya Bunge kwa kufanya ziara katika chuo hicho,  huku akisema imeacha neema kwa wanafunzi wake na amewaomba waajiri wa sekta binafsi kuwatumia wanafunzi wanaosoma fani mbalimbali chuoni hapo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Taufiq amesema kamati hiyo itaenda kuishawishi Serikali kutoa mtaji na vifaa kwa vijana wanaohitimu fani mbalimbali, kupitia programu hiyo ya mafunzo ya uanagenzi.

“Tutaishauri Serikali kama bajeti itatosheleza mtakapokuwa mnamaliza mafunzo basi muwe mnapatiwa vifaa vitakavyowawezesha kwenda kujiajiri. Yawezekana msipatiwe wote lakini angalau kwa uchache wenu,” amesema Taufiq. 

Awali, akizungumza kwa niaba ya Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Cyprian Luhemeja amesema kupitia programu hiyo, Serikali imetoa Sh2.7 bilioni kufadhili mafunzo kwa wanafunzi 6,000 katika vyuo 43 nchini mwaka 2023/24.

Pia Luhemeja amesema Chuo cha Veta Mwanza kimepokea Sh59 milioni kugharamia mafunzo kwa wanafunzi 132 wakiwemo wenye ulemavu sita waliodahiliwa mwaka huu wa masomo, huku akidokeza kuwa vijana 141,968 wamenufaika na fani mbalimbali kupitia programu hiyo tangu mwaka 2016 nchi nzima.