Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Veta kuwakutanisha vijana 4,000

Mshauri wa ufundi kutoka Veta Leah Dotto (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la vijana waliopata mafunzo kupitia program ya kukuza ajira na ujuzi (E4D) litakalofanyika Jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi  nchini  (VETA) imeandaa kongamano la vijana waliopata ujuzi kupitia Programu ya Kukuza Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo Afrika (E4D), litakalofanyika Agosti 24 mwaka huu, jijini Dodoma.

Dodoma. Vijana 4,000 waliomaliza mafunzo ya ujuzi kupitia programu ya kukuza ajira na ujuzi kwa maendeleo Afrika (E4D) watashiriki katika kongamano la kuwakutanisha na fursa za ajira.

Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo Stadi (VETA), Abdalah Ngodu ameyasema hayo leo Jumanne, Agosti 22, 2023 Jijini Dodoma.

Amesema kongamano hilo, litatoa fursa kwa vijana hao kuonyesha kazi zao walizozifanya kupitia mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.

Amesema kongamano hilo litawakutanisha vijana hao na waajiri ili waweze kushirikishana kuhusu taarifa za soko la ajira pamoja na kuonyesha umahiri wa ujuzi wao katika bidhaa walizotengeneza na miradi yao wanayotekeleza.

"Hivyo kwenye kongamano hilo wananchi watapata fursa ya kujionea shughuli zinazofanywa na wahitimu wa mradi wa kukuza ajira na ujuzi pamoja na kupata taarifa juu ya fursa za mafunzo ya ufundi stadi zinazopatikana kwenye vyuo vya Veta nchini," amesema Ngodu.

Kwa upande wake mkuu wa chuo cha Veta Dodoma, Stanslaus Ntibara amesema programu hiyo imewanufaisha jumla ya vijana 4,000 huku Dodoma ikiwa na vijana 2,200 na wengine waliobaki wametoka Mikoa ya Manyara, Lindi na chuo cha Kipawa kilichopo Jijini Dar es salaam.

Amesema vijana hao wamepata mafunzo ya ufundi bomba wa majumbani na viwandani, ufundi wa uchomeleaji vyuma viwandani na ufundi Mekatroniki.

Naye Mshauri wa Ufundi kutoka chuo hicho, Leah Dotto amesema kuna vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Sh418 milioni ambavyo vimenunuliwa kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa vitendo kwa vijana wote watakaosoma programu hiyo.