Sita Mahakamani kwa uhujumu uchumi, utakatishaji fedha

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imemfikisha mahakamani mjasiliamali, Caroline Magafu na wenzake watano wakikabiliwa na kesi ya uhujumu Uchumi yenye mashitaka sita likiwemo la utakatishaji wa zaidi ya Sh1.4 bilioni.

Dar es Salaam. Watu sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka sita likiwemo la utakatishaji wa fedha  zaidi ya sh1.4 bilioni.

Washtakiwa hao ni  Watanzania Caroline Magafu, Raymond Richard na Grace Sureshi; wengine ni raia wa Nepal Bhusal Govinda na Emanuel Gaudios , Mkameruni mmoja Takoounga Anselme.

Wakili wa Serikali kutoka Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akisaidiana na wakili wa Serikali Gloria Mwenda, wamewasomea hati ya mshtaka walidai, washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Agosti na Septemba mwaka 2022  jijini Dar es Salaam.

Wakili Groria alidai katika tarehe hizo, jijini Dar es Salaam washitakiwa hao kwa pamoja  kwa nia ovu waliungana mtandao wa kiharifu  na kujipatia Dola za Kimarekani 623,000 sawa na Sh1.449 bilioni kutoka kampuni ya Zhejiang Afol Import and Export Co. ltd.

Imedaiwa kuwa kati ya Agosti 19 na Septemba 29 mwaka 2022 jijini Dar es Salaam, Caroline na Govinda walijipatia Sh449 milioni kutoka kampuni hiyo kupitia akauti yao iliyopo benki ya Stanbick kama malipo ya kuuza madini aina ya shaba tani 100, kupitia kampuni ya Steca Export and Import Company, wakati wakijua si kweli.

Alidai kuwa kati ya Agosti na Septemba mwaka 2022, Dar es Salaam, mshitakiwa Gaudios, Richard na Grace; walikula njama ya kutenda kosa la kugushi.

Katika shtaka lingine inadaiwa kuwa Septemba 16 mwaka 2022 mtaa wa Nkuruma, mshitakiwa Gaudios aligushi hati ya kusafirishia mzigo (bill of lading), akionesha kwamba, kampuni ya Stecas Export and Import, imesafirisha tani 44 za madini ya shaba kwenda kampuni ya Zhejiang Afol Import and Export Co.Ltd wakati akijua siyo kweli.

Inadaiwa kwamba katika tarehe hizo, na eneo hilo, mshitakiwa huyo aligushi hati ya kusafirishia mzigo, akionesha kampuni ya Stecas Export and Import, imesafirisha tani 66 za madini ya shaba kwenda kampuni ya Zhejiang Afol Import and Export Co.Ltd wakati akijua siyo kweli.

Iliendelea kudaiwa kuwa,  Septemba 2, mwaka 2022 eneo hilo, mshitakiwa huyo akiwa mwajiriwa wa kampuni ya  Glob Vest Group Ltd , alijipatia sh 12, 964,000 kutoka kampuni ya Zhejiang Afol Import and Export Co LTD kama malipo ya kusafirisha mzigo tani 44 za madini ya shaba.

Katika shitaka la utakatishaji fedha, ilidaiwa kwamba, kati ya Agosti 19 na Septemba 29 mwaka 2022 jijini Dar es Salaam,  washitakiwa wote walijihusisha katika miamala ya zaidi ya Sh1.4 bilioni wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya makosa ya jinai.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio alisema  washitakiwa hao hawakuruhusiwa  kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kesi iliahirishwa hadi Mei 25 mwaka huu.