Sita washikiliwa kwa kufanya utapeli wa ajira Moshi

Sita washikiliwa kwa kufanya utapeli wa ajira Moshi

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia wafanyakazi sita wa Kampuni ya Allience Motion In Global kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya utapeli.


Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia wafanyakazi sita wa Kampuni ya Allience Motion In Global kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya utapeli.

Wafanyakazi hao wamekamatwa baada ya agizo lililotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Said Mtanda baada ya kupokea taarifa ya zaidi ya watu 50 kuitwa na kampuni hiyo kwa ajili ya kupata ajira.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 8, 2021 Mkuu huyo wa wilaya amesema kwa kushirikiana na Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu walifanya mtego na kuweza kuwakamata watu hao sita waliokuwa wakitapeli wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania.

"Hii kampuni imekuwa ikitoa watu kutoka mikoa mbalimbali kwa kuwadanganya kuwapatia ajira lakini wanapofika mjini Moshi hawapewi ajira zaidi ya kupewa semina ambayo kila mshiriki hulipia kwa gharama ya Sh220,000," amesema.

Mtanda amelitaka Jeshi la Polisi kuchunguza uhalali wa kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kurejesha kwa kila mwananchi fedha aliyotoa Sh220,000 ili waweze kurudi walikotoka.

Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu ameeleza kusikitishwa na utapeli unaofanywa na kampuni hiyo na kuwatahadharisha wananchi  kujiepusha na watu wanaowapiga simu kuwa watapatiwa ajira.


"Nimesikitishwa sana na utapeli ambao umekuwa ukifanywa na kampuni hiyo, na kuanzia sasa sitaki kusikia kampuni yoyote inakuja kufanya shughuli ndani ya Manispaa ya Moshi bila kufuata taratibu husika ikiwamo kupata vibali toka mamlaka husika," amesema Meya Raibu.

Kampuni hiyo inafanya shughuli zake jijini Dar es Salaam.