Soko la Karume lateketea kwa moto

Wafanyabiashara na wananchi wakiangalia mabaki ya mali zilizoteketea baada ya Soko la Karume, Mchikichini lililopo jijini Dar es Salaam kuungua juzi usiku. Picha na Silvan Kiwale
Muktasari:
- Umuteketeza mali zote zilizohifadhiwa katika mabanda ya wafanyabiashara.
Dar es Salaam. Soko la Karume (soko la mchikichini) limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana. Chanzo cha moto kinadaiwa ni hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye ghala la kuhifadhia bidhaa.
Imeelezwa kuwa moto huo ulioteketeza sehemu kubwa ya soko hilo lenye wafanyabiashara zaidi ya 3,500, ulianza usiku wa saa 4:00 usiku na uliendelea kuwaka usiku kucha na juhudi za zimamoto na uokoaji kuudhibiti hazikufua dafuhibiti.
Akizungumza baada ya kukagua athari za moto huo, meya wa manispaa ya Ilala, Jerry Slaa alisema ajali hiyo ni kubwa katika ajali za moto ambazo zimewahi kutokea sokoni hapo na kuahidi kushirikiana na mamlaka zinazohusika kubaini chanzo chake na hatua za kuchukua.
Silaa alisema wafanyabiashara zaidi ya 2,700 wamepoteza mali zao zinazokadiriwa kuwa zaidi ya Sh1 bilioni. Alisema wahusika wanatakiwa kuwa na subira wakati mamlaka zikitafuta chanzo cha moto huo.
Hata hivyo, aliwahadharisha wafanyabiashara hao kutoeneza ujumbe usiokuwa sahihi kwamba moto huo ni hujuma kama inavyodaiwa na baadhi yao. Alisema Serikali haiwezi kufanya hujuma kwa watu wake.
Mmoja wa wafanyabiashara ya mkaa ndani ya soko hilo, Deo Mtei alidai kushuhudia moto huo ukianza kutokana na hitilafu ya umeme kwenye mabanda ya stoo saa 3.30 usiku na kusambaa kwa kasi.
“Moto ulianza kusambaa kwa kasi ya ajabu kutokana na mabanda mengi kuunganishwa umeme kienyeji,” alisema Mtei.
Kamanda wa polisi Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema wanafanya uchunguzi kwa kushirikiana na Tanesco ili kubaini chanzo cha moto huo.
Mwenyekiti wa soko hilo, Jumanne Kongogo alisema mabanda ya zaidi ya wafanyabiashara 4,000 yameteketea.
Kongogo aliziomba taasisi za kifedha zilizowakopesha baadhi ya wafanyabiashara hao, kutafuta njia mbadala ya kuwaongezea muda wa marejesho ya mikopo hiyo.
Alisema mitaji ya asilimia kubwa ya wafanyabiashara hao ni mikopo.
Imeandaliwa na Beatrice Moses, Andrew Msechu na Pamela Chilongola.