Somalia yatambuliwa rasmi EAC, viongozi kuvalia njuga migogoro

Waziri wa Viwanda wa Somalia (kushoto), Jibril Abdirashid Haji Abdi akikabidhi nyaraka za kukubaliana na masharti ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa Katibu wa Jumuiya hiyo, Peter Mathuki ndani ya makao makuu ya jumuiya hiyo iliyoko jijini Arusha

Muktasari:

  • Somalia yajitolea kufuata sheria na kuchangia maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki baadaya kutambuliwa rasmi mwanachama wa nane.

Arusha. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeipokea rasmi Somalia kama mwanachama wa nane leo, Machi 4,  2024,.

Somalia, inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, imefanikiwa kukabidhi nyaraka za kukubali kufuata sheria za EAC, ikithibitisha nia yake tangu mwaka 2012.

Baada ya kukubaliwa tangu Novemba 24, 2023, Somalia imetimiza masharti na kusaini hati ya makubaliano leo.

Katibu wa EAC, Peter Mathuki amesema Somalia sasa inatambulika rasmi kama mwanachama na viongozi wa EAC wameahidi kushirikiana kutatua changamoto za kiusalama nchini humo.

Somalia inakuwa mwanachama pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Tanzania, DRC na Sudan Kusini.

Miongoni mwa daida za kujiunga na EAC ni pamoja na upanuzi wa soko katika nchi wanachama na ukuaji wa uchumi.

Somalia sasa inatakiwa kuteua wabunge na jaji kutoka nchi hiyo wa kushiriki katika shughuli za EAC.

Kufuatia hatua hiyo, viongozi wa nchi wanachama za EAC, wanatarajia kuanza safari ya kusaka suluhu ya changamoto za kiusalama zinazoikabili Somalia.

Novemba 24, 2023 kwenye mkutano wa 23 wa mwaka uliofanyika jijini Arusha, ilipewa masharti ya kufuata na kusaini hati ya makubaliano ya kuridhia ndani ya miezi sita.

Nchi hiyo imefanikiwa kuwasilisha hati ya makubalino ya kuridhia masharti na sheria za EAC, iliyosainiwa Desemba 15 mjini Kampala, Uganda kati ya Rais wa Somalia Sheikh Hassan Mohamud na mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Salva Kiir Mayarditi ambaye ni Rais wa Sudani Kusini, ikishuhudiwa na mwenyeji wao, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Mathuki amesema baada ya kukabidhi nyaraka hizo za kukubaliana na masharti waliyopewa na kuahidi kuyafuata, wanaingizwa rasmi kwenye mipango na mikakati yote ya jumuiya hiyo, ikiwemo majadiliano ya bunge lao.

Amesema wanatambua changamoto za kiusalama zinazoikabili nchi hiyo na rasmi viongozi wa juu wa Jumuiya watalibeba kama ajenda za mikutano yao na kuona namna gani wanaweza kurudisha amani nchini humo.

“Wakuu wa nchi za jumuiya hii wako tayari kushirikiana katika changamoto zinazowakumba wenzetu za kiusalama, kama wanavyobeba mgogoro wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuona jinsi wanarudisha amani ili biashara iweze kufanyika na jumuiya iweze kunufaika nao,” amesema Mathuki.

Akizungumzia faida kwa Somalia kujiunga na EAC, Mathuki amesema imepanua soko la bidhaa za wanajumuiya ambayo sasa imefikia wateja milioni 350.

Waziri wa Habari wa Somalia, Daud Aweis amesema haikuwa kazi rahisi kutimiza masharti ya kujiunga na EAC lakini wanamshukuru Mungu wametimiza na wamekubaliwa kuwa wanachama.

Amesema wanatarajia kutoa michango yao na kupokea maoni kwa ajili ya uimara wa umoja huo na kwa manufaa ya nchi wanachama.

“Leo ni siku kubwa sana kwetu, na muhimu kufanikiwa kuwa wanachama rasmi wa jumuiya hii, tulipewa sheria na kanuni hizi mwaka jana na tulizifikisha kwa Bunge letu wakajadili na Rais wetu kukubaliwa na wabunge kusaini, leo wametutuma kuleta hati hizi kwamba tuko tayari kufuata masharti yote na kanuni zake” amesema Awes.

Awali, Waziri wa Viwanda kutoka Somalia, Jibril Abdirashid Haji Abdi alisema nchi hiyo bado ina fursa nyingi za biashara licha ya kukabiliwa na changamoto ya amani.

“Tumefurahi kuwa familia moja sasa tunaahidi kuwa wawazi katika fursa zetu za kibiashara zilizopo maeneo mbalimbali nchini kwetu, lakini pia tunawakaribisha wageni kutoka nchi hizi kutembelea Somalia kutengeneza mnyororo mpya wa mahusiano na ushirikiano,” amesema Haji Abdi.

Amesema licha ya kupewa miezi sita ya kufanikisha taratibu zote, lakini kutokana na uhitaji, umuhimu na nia ya kujiunga EAC walifanya kama ajenda yao ya kwanza na kwa haraka wamefanikisha.

Mbali na nyaraka za makubaliano, Somalia pia imewasilisha bendera yake katika makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha na ikapandishwa rasmi leo.