Spika Ndugai yuko njiapanda

Muktasari:

 Utendaji kazi wa Spika wa Bunge Job Ndugai sasa uko njiapanda baada ya kutofautiana kimtazamo na Rais Samia Suluhu Hassan, juu ya mikopo inayochukuliwa na Serikali, wasomi na wadau wa siasa wamesema.


Dar/mikoani. Utendaji kazi wa Spika wa Bunge Job Ndugai sasa uko njiapanda baada ya kutofautiana kimtazamo na Rais Samia Suluhu Hassan, juu ya mikopo inayochukuliwa na Serikali, wasomi na wadau wa siasa wamesema.

Siku chache zilizopita Ndugai alishauri Serikali ijielekeze katika kusaka fedha za ndani ikiwemo tozo badala ya kwenda kukopa na kuifaanya nchi ilemewe na mzigo wa madeni unaoweza kuifanya ipigwe mnada.

Siku moja baada ya kauli hiyo, Rais Samia aliwesisitiza Serikali yake itaendelea kukopa ili kuchochea kasi ya maendeleo, huku makada mbalimbali wa CCM kumshambulia Spika Ndugai.

Kwa hatua hiyo Ndugai hakuwa na njia nyingine zaidi ya kumuomba radhi Rais Samia na Watanzania kutokana na kauli hiyo iliyozua mtafaruku na kuonekana wakuu wa mihimili miwili ya dola wametofautiana.

Hata baada ya kuombwa radhi, Rais Samia juzi alitumia muda mrefu kukemea kitendo cha Spika ambaye ni mkuu wa mhimili kukosoa mikopo ya Serikali, hasa ya mashatri nafuu, huku akihusisha kitendo hicho na harakati za kusaka urais mwaka 2025.

Njia ni moja

Kufuatia sakata hilo, wakizungumza na Mwananchi jana, wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa walisema kwa hali ilivyo Spika Ndugai ni vema akajiuzulu wadhifa huo kwa kuwa ameshapoteza imani kwa kiongozi wa chama chake, Rais Samia.

Hata hivyo jana Ndugai hakupatikana kupitia simu kuzungumzia maoni hayo ya wachambuzi

Miongoni mwa wadau wa siasa waliozungumzia suala hilo ni baadhi ya wabunge wa CCM, waliotumia mitandao ya kijamii, hasa Instagram kueleza ugumu atakaokabiliana nao Spika.

Catherine Magige, mbunge wa viti maalumu alisema mazingira ya kazi yatakuwa magumu kwa Spika kwa kuwa hataungwa mkono na wanachama wa CCM, chama kilichomwezesha kufika alipo.

Munde Tambwe, yeye hakuuma maneno akisema kwa masilahi mapana ya nchi, ni vema Ndugai akajiuzulu kwa kuwa hakuna namna nyingine.

Naye Ester Charles alisema baada ya kusikiliza hotuba ya Rais juzi, inaonekana msamaha aliuomba Ndugai haujakubalika, hivyo mazingira ya kazi yatakuwa ni magumu kwake.

Kwa upande wake Neema Rugangira, pia wa viti maalumu alisema ni dhahiri hakuna umoja na ushirikiano kati ya wakuu wa mihimili miwili (Serikali na Bunge) hivyo kazi hazitaendelea.

Wabunge hao wanaungwa mkono na Anna Henga, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), aliyesema kwa mataifa yaliyoendelea, tayari Spika Ndugai angekuwa ameshajiuzulu kwa kuzua taharuki.

Si Anna Henga pekee, hata Agustino Mrema, mwenyekiti wa TLP, alisema hivi Rais Samia hana, amani naye na hali ikiendelea hivyo kuna uwezekano utendaji wa Bunge au Serikali ukalegalega.

“Kuomba radhi pekee hakutoshi. Ndugai amemkosea heshima Rais Samia, amemvunja moyo na nguvu; ni vema ajiuzulu ili kikao kijacho cha Bunge kimchague Spika mwingine. Hii italeta umoja, ushirikiano na kuaminiana ndani ya CCM na Serikali yake,” alisema.

Alisema akijiuzulu hali ya kuaminiana miongoni mwa viongozi wakuu wa mihimili ya dola itarejea na itakuwa funzo kwa viongozi wengine kuhusu umuhimu wa kuchunga ndimi zao na kuchagua maneno.

Hata hivyo, mtazamo tofauti ulitolewa na Dk Kaanaeli Kaale, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino aliyeshauri suala la Ndugai lijadiliwe na kuamuliwa na vikao vya juu vya CCM kutokana na nafasi yake ya kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho tawala.

“Nafasi za kisiasa siyo za kudumu. CCM ina mfumo, misingi na utamaduni wake katika kushughulikia mambo yake, nadhani suala hili lijadiliwe na kuamuliwa kupitia vikao vya chama ikiwemo kamati ya maadili,” alisema Dk Kaale.

Katiba na nafasi ya Spika

Kwa mujibu wa ibara ya 84 (1) hadi (7) ya Katiba, umewekwa utaratibu wa kumpata na kumwondoa madarakani Spika madarakani, ikiwemo kujiuzulu au kulazimishwa kufanya hivyo au kwa kupoteza unachama wa chama kilichomdhamini.

Makada CCM wafunguka

Akizungumzia suala hilo, Dk Abel Kinyondo alirejea chanzo cha suala hilo akisema mawasiliano baina ya viongozi na muktadha wa hoja ndiyo tatizo.

“Spika ni kiongozi wa Bunge linalopokea na kujadili bajeti ya Serikali, kwa nini asitoe maoni yake kwa Wizara ya Fedha? Kama angezungumzia ndani ya Bunge lile angekuwa na kinga na muktadha ungeonekana wazi kasemea wapi hoja yake na huenda malengo yangeonekana ya ukosoaji,” alisema D kKinyondo.

“Pili, Ndugai na Rais Samia ni viongozi wa mihimili, angeweza kumwambia chemba (faragha), sasa kutoa kauli ile hadharani tena bila muktadha wa nafasi yake bungeni, ni tatizo.”

Dk Kinyondo alisema tofauti hizo za viongozi zinaleta afya kwa jamii baada ya mkuu wa nchi kubaini maadui zake ni wanaovaa kijani na si vyama vya upinzani. Alisema tofauti hizo zitamfanya Rais kuongeza umakini katika maamuzi yatakayokuwa chanya kwa wananchi.

Naye Dk Frank Kimario wa Chuo Kikuu cha Iringa alisema Rais Samia alilazimika kutoa ufafanuzi ule ili kueleza anachoamini kufichika nyuma ya kauli za Ndugai.

Alisema Ndugai kwa nafasi yake alikuwa na nafasi ya kufuata utaratibu wa kupima uzito wa hoja yake na kuiwasilisha katika Serikali au chama.

Msomi huyo alisema katika mazingira ya ukomavu wa kisiasa na uwajibikaji, Ndugai alitakiwa kujiuzulu mara moja nafasi yake katika kiti cha spika wa Bunge hilo.

Kwa mtazamo huohuo, Professa Mohamed Makame Haji, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) alisema ufafanuzi wa Rais Samia, licha ya Ndugai kukiri makosa yake, umepunguza hofu ya Watanzania juu ya mikopo inatotafutwa na Serikali.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu bara wa Chama cha Demokrasia Makini, Cecilia Mmanga alishauri Spika Ndugai kutafuta nafasi ya kukaa meza moja na Rais Samia ili kumaliza tofauti hizo.

“Mtoto akikunyea huwezi kukata mkono wako, ni kweli Ndugai aliteleza ulimi lakini Rais akubali kumsamehe kama mzazi, kila mtoto ana tabia zake na mama lazima ajue namna ya kushughulika nazo, amsamehe,” alisema Cecilia.

Akitoa maini yake mwanazuoni wa siku nyingi na mtaalamu wa falsafa, Dk Azaveri Lwaitama alisema ni jambo la kushangaza kwamba watu wanaanza mbio za urais miaka minne kabla ya muda wa uchaguzi badala ya kuwatumikia wananchi.

Alisema kauli ya Rais Samia inaonyesha kwamba kuna watu ndani ya chama wanajipanga kugombea urais wakati wana majukumu makubwa ya kutatua kero za Watanzania.

“Mimi ukiniuliza nitakwambia hiki ni chama cha ajabu sana, wakati wananchi wanahangaika na tozo na kupanda kwa bei za bidhaa, wao wanahangaika kupanga safu za mwaka 2025,” alisema Dk Lwaitama.

Akizungumza na Mwananchi Mbunge wa Mtera mkoani Dodoma, (CCM), Livingstone Lusinde alisema anawaombea kwa Mwenyezi Mungu, Spika Ndugai na Rais Samia ili waweze kufikia muafaka.

Alisema ni ngumu kuzungumza chochote kwa sababu msuguano huo unahusisha viongozi wakuu, hivyo maombi yake Mungu awape busara.

“Hawa ni viongozi wetu wakuu, kwa hiyo ni ngumu kueleza chochote. Ila mimi nawaombea kwa Mungu wapate busara na kuweza kufikia muafaka,” alisema Lusinde.

Alipoulizwa kuhusu msamaha ambao Spika Ndugai aliomba, Lusinde alisema msamaha una mambo mawili ambayo ni kukubaliwa au kukataliwa.

“Unapoomba msamaha uwe tayari kwa vitu viwili, kukubaliwa au kukataliwa. Anayeombwa ndiye anachagua kati ya hayo mawili,” alisema mbunge huyo.

Haijapata kutokea

Historia ya Tanzania haionyeshi kuwa mhimili wa Bunge uliwahi kugombana na mhimili wa Serikali. Spika wa kwanza wa Tanganyika huru, Abdulkarim Yusufali Karimjee ambaye alikuwa Spika wa Bunge wakati wa ukoloni kuanzia Januari mosi 1956 hadi Desemba 26, 1962 Tanganyika ilipokuwa Jamhuri.

Adam Sapi Mkwawa alikuwa Spika wa Bunge kuanzia Aprili 26, 1962 hadi Novemba 19, 1963 akiwa na Mwalimu Nyerere.

Akafuatia Erasto Mang’enya aliyeingia  Novemba 20, 1973 na alikaa na Nyerere hadi Novemba 5, 1975.

Baada ya muda, Adam Sapi Mkwawa akarudi kwenye nafasi hiyo kuanzia Novemba 6, 1975 hadi alipostaafu rasmi Aprili 25, 1994 na mambo yalikwenda vyema.

Aprili 28, 1994 aliingia Pius Msekwa ambaye kwa muda fulani alikaa na Mwalimu Nyerere na muda mwingine akakaa na Ali Hassan Mwinyi na baadaye Benjamin Mkapa. Yeye alikaa hadi Novemba 28, 2005. Mambo yalikuwa shwari.

Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 14, 2005, Samuel Sitta alichaguliwa kuwa spika Desemba 28, 2005.

Wakati anakaribia kuingia kipindi cha pili, inaelekea kulikuwa na mvutano fulani ndani ya chama chake na hivyo hakuweza tena kugombea kipindi kingine baada ya uhai wa bunge la wakati wake kumalizika.

Ndipo akaja Anne Makinda Novemba 10, 2010 na kukaa hadi Novemba 16, 2015 muhula wa pili wa Kikwete ulipomalizika. Ndipo Job Ndugai akaingia Novemba 17, 2015 hadi sasa.

Katika historia ya Tanganyika na baadaye Tanzania, haijawahi kutokea viongozi wa mihimili miwili ya dola—kama Serikali na Bunge—kugombana.

Nje ya Bunge, Januari 26 – 29, 1967 Nyerere alizozana na Waziri wa Ulinzi, Kambona katika mkutano wa kuanzishwa Azimio la Arusha. Baadaye Kambona alijiuzulu nyadhifa zake zote na kuondoka nchini.

Mgogoro mwingine mkubwa wa viongozi ulikuwa wa Januari 29, 1984 pale Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe Mwinyi alipolazimika kujiuzulu baada ya “kuchafuka hali ya kisiasa”.

Jumbe alilazimika kujiuzulu katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM mjini Dodoma. Hata hivyo, huo haukuwa ukinzani wa mihimili ya dola bali ni viongozi wa chama na Serikali.