Sugu awataka wanaume kufunguka ukatili wanaofanyiwa

Aliyekuwa mbunge wa Mbeya, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 24, 2022 wakati akitoa taarifa ya kuwepo kwa kongamano la siku ya Wanaume lanye kauli mbiu “Bro Funguka”.

Muktasari:

  • Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amewataka wanaume kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa katika ndoa ili kupata msaada wa kisheria na kisaikolojia.

Mbeya. Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amewataka wanaume kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa katika ndoa ili kupata msaada wa kisheria na kisaikolojia .

Sugu amesema hayo leo Jumatatu, Oktoka 24, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kuwepo na Kongamano la Siku ya Wanaume lenye lengo la kusikiliza changamoto zao, hususan katika suala la biashara na uchumi.

“Wanaume wanapaswa kuwa na amani ya moyo muda wote ili familia iweze kwenda na kitendo cha usiri wa kuficha vitendo vya ukatili ndio vinasababisha kuwepo kwa matukio ya mauaji au mtu kufikia kujiua “amesema.

Amesema kuwa Kongamano hilo ambalo limendaliwa na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Empower Youth Prosperity (EYP) ambapo yeye ameteuliwa kuwa mjumbe wa bodi huku kauli mbio ikiwa ni“Bro Funguka”.

Sugu amesema kuwa ufike wakati wanaume kufunguka ili kuweza kupata msaada wa kisheria na kisaikolojia na kuachana na dhana za kufanya maamuzi magumu.

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi hiyo, Ipyana Mwakyusa amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwajengea uwezo wanaume wa kukabiliana na changamoto ya afya ya akili, kiuchumi, kijamii pamoja na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanaume walio kwenye mahusiano.

 “Tunaamini kupitia Kongamano hilo changamoto za kiuchumi, afya ya akili na ukatili wa kijinsia kwa wanaume zinazuilika ikiwa sote tutashirikiana kuzibaini na kuzitafutia suluhu ya kudumu katika jamii”amesema.

Mwanasaikolijia na Mkurugenzi wa Taasisi ya Nasaha hub, Silvester Mwasyuya amesema kuwa kupitia kongamano hiko wanaume wanapaswa kupaza sauti ili kuepuka athari za kisaikolojia wanazokumbana nazo na kutimiza kauli mbio ya “Bro Funguka ”.

Mkazi wa mjini Mbeya, Amos Joel amesema changamoto ya ukatili wa kijinsia katika ndoa ni kubwa jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa matukio ya mauaji kutokana na kuchoshwa na matusi, dharau zinazotokana na ukosefu wa kupato kwa wanaume.