SUGU: Tumepitia mazingira magumu

SUGU: Tumepitia mazingira magumu

Muktasari:

  • Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameanza kazi vizuri, huku akiomba mambo yaliyotokea kabla ya kiongozi huyo kushika wadhifa huo yasirudiwe na waliyoyafanya wakeweme.

Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameanza kazi vizuri, huku akiomba mambo yaliyotokea kabla ya kiongozi huyo kushika wadhifa huo yasirudiwe na waliyoyafanya wakeweme.

 Alieleza hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi aliyoyafanya hivi karibuni mkoani Mbeya. Kuna mambo gani hutoyasahau? Nchi ilikuwa katika mazingira magumu, wanasiasa tulizuiwa kufanya siasa, katika chaguzi mbalimbali tulishuhudia wizi wa kura, mfano yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali ya mitaa.

Ninajisikia vibaya nikitafakari. Ninajua watu wangapi wamefungwa chini ya..., binafsi nilifungwa nadhani unakumbuka, nilikata rufaa na nilishinda na Mahakama Kuu ilishangaa hata nilifungwaje? Watu walifungwa wengi, mtu anashushwa kwenye jukwaa anahutubia na kuambiwa amemtukana mtu, anawekwa ndani siku nne na mkitaka apewe dhamana anahamishwa na baadaye anapewa kesi yoyote.

Hayo yanafanyika mtu ana watoto, familia na wazazi yaani mtu kwa ajili ya kulinda nafasi yake anakupa kosa ambalo si lako, hayo ndio mambo ambayo tunayakumbuka.

Mfano Nape (Nnauye-mbunge wa Mtama-CCM) alitishiwa bastola, wale watu waliomtishia wako wapi..., watu walivamia maeneo mbalimbali na bunduki, tukiyasahau haya yatajirudia lazima yasemwe ili yasirudiwe, lazima wahusika waelezwe ubaya walioufanya waone na waogope.

 Wakati nikiwa mbunge, nilinunua kompyuta kwa hela zangu nikapeleka shule na wakati nazungumza na walimu, wananchi na wanafunzi, wakaja watu wakanikamata naambiwa nimeitisha mkutano bila kibali na shule nzima ikahojiwa..., sijui hata ilikuwaje mpaka tukafikia kule.

Nimempoteza mama yangu kwa sababu ya siasa..., kwa hiyo ukiniuliza najisikiaje nitakwambia siwezi kulia wala kucheka kwa kuwa najisikia vibaya kwa hapo tulipofika, sifurahii wala sihuzuniki ila najiuliza ilikuwaje tukafika hapa.

Unawazungumziaje wabunge 19 wanaoendelea na nafasi zao licha ya kufukuzwa uanachama Chadema? Wale wabunge ni batili, walipatikana kibatili na katika aibu za utawala wa awamu ya tano na uspika wa Ndugai (Job) ni rafu ya wabunge hawa.

Wamekataa kutumia akili na maarifa kuendesha mambo, sasa wanatumia nguvu na ubabe. Watu wanasema Ndugai ni rafiki yangu, lakini principal is the principal, wanasahau Ndugai alimrejesha Mwambe (Cecil) wakati akijua Mwambe alihama chama (Chadema) mwenyewe akapokewa na Dk Bashiru (Ally-katibu mkuu wa zamani wa CCM) na kisha alikwenda Ndanda kuendelea na shughuli zake.

Bungeni kuna siku Mnyika (John-sasa katibu mkuu wa Chadema) akaomba mwongozo sijui wa nini na Spika akaagiza Mwambe aje na (Mwambe) akarudi bungeni akitokea Ndanda. Akawa anaingia bungeni bila kuapa na tulimuona, lakini ilipokuja ishu watu wanakwenda mahakamani ndio akapotea..., ukisema ilikuwa unaitwa na kamati ya Bunge na kuambiwa umelidharau Bunge.

Juzi Rais Samia amesema Bunge halifanyi kazi inayopaswa kufanya, hiyo maana yake ameona kuna kitu pale. Najua kama chama tuna fursa ya kukutana na Rais Samia, maana Mnyika alieleza kuwa kiongozi amekubali kuonana na sisi tutalisema hili.

Rais Samia aligusia suala la diplomasia unadhani kwa nini? Kwa sababu anajua mahusiano hayakuwa mazuri, nikupe mfano, hivi unaweza kukamata vifaranga vya jirani yako mathalani Kenya hapo ukavichoma moto badala ya kuvirudisha vilipotoka.

Ile ni bidhaa mbona wao (Kenya) waliposema mahindi yetu hayafai hawakuyachoma moto waliyarudisha.

Lazima tutengeneze mazingira ya kwenda mataifa ya nje tujifunze mambo na pia kutengeneza wigo wa ukusanyaji kodi, Mama Samia anajua ukitaka kufika mbali nenda na wenzako, anajua lazima twende na wenzetu na ndio maana katika Wizara ya Mambo ya Nje alimteua Balozi Liberata Mulamula kuwa waziri, huyu waziri tunayo rekodi yake alipokuwa America,

Watanzania na jumuiya ya kimataifa inamuheshimu, ni mtu mwenye funguo na atafungua loki za kimat Diplomasia ni uchumi, huwezi kusema uchumi halafu unakandamizia diplomasia na demokrasia utakwama kwa sababu utafanya biashara na nani?

Nini ushauri wako kwa Serikali kuhusu uhaba wa ajira kwa vijana? Tumezungumza kwa miaka mingi kuitaka Serikali ibadili mitalaa na ndio maana kwa sasa mtazamo wa watoto wa shule binafsi ni tofauti na wa shule za Serikali.

Tubadilishe mfumo wa elimu yetu ili watoto wetu wasiwe na wazo la kusoma ili kuajiriwa, huo ni mfumo wa mkoloni kusomesha watu ili wakafanye kazi, tulitakiwa tubadili na tuje na mfumo tofauti mtu atarajie akimaliza elimu yake aajiri zaidi.

 Tukiwa na wasomi wa namna hiyo tutakuwa na wabunifu wengi. Hiyo ni long term lakini short term, biashara irudi watu wafanye biashara ya kujiingizia kipato.

Mfano mimi nikiajiri watu watano na wengine wakaajiri kama mimi maana yake mzunguko wa fedha unakuwa mkubwa. Tumefika hapa kwa sababu ya sheria za kubana na kuzuia..., sheria zinatakiwa kubadilishwa ili isiwe tu kauli ya kiongozi iwe sheria ili wafanyabiashara wajisikie wapo salama. Masuala ya uchumi yanatakiwa kuwa katika level moja bila kujali nani atakuwa rais.

Unazungumzia Tanzania ya kiutawala, kisiasa na maendeleo? Sasa hivi tunafanyia kazi nia yake njema aliyoionyesha (Samia)..., tufanyie kazi ile nia yake njema ambayo anaionyesha.

Hata anavyosema yeye na aliyemtangulia ni kitu kimoja watu wanamkataa kwa sababu mambo mengi ameyabadilisha kwa muda mfupi. Ndani ya wiki mbili alikuwa amebadili mtazamo kwa kiasi kikubwa sana mpaka confidence ya nchi ipo juu.

 Unavizungumziaje vyama vya siasa nchini? Katika vitu ambavyo ni faida kwa Taifa na Watanzania wameweza kujua kwa sasa ni kipi chama halisi cha upinzani na kipi ni chama kanjanja. Sitaki kurushiana sana madongo lakini ukiniuliza kuhusu vyama vya siasa, nitakujibu katika miaka mitano iliyopita Watanzania watakuwa wamejua kipi ni chama pinzani na kipi si chama pinzani.

Mbeya itakukumbuka kwa lipi? Sipendi sana kusema nimejenga barabara au mambo mengine kwa sababu huo ni wajibu..., wananchi wao watasema ila kitu ninachojivunia ni kuwa mbunge kwa miaka 10 lakini bado nipo mioyoni mwa wana Mbeya na hivyo inatokana na sababu mbalimbali.

Bado natembea kwa miguu mitaa ya Mbeya labda pale nione mkusanyiko unakuwa mkubwa zaidi na ninakuwa na haraka na shughuli nyingine.

Mimi na watu wa Mbeya hakuna kilichobadilika. Watu wa Mbeya ni suala la muda tu kuona kwamba tunarudi pale tulipokatizwa. Wewe ni mwanamuziki, una mipango gani kwa sasa? Ninapenda sana muziki, ila tatizo ni muda maana nimejikita zaidi katika biashara, unajua kwenye biashara kuna maeneo unatakiwa kujifunza, kusafiri na kuangalia fursa mbalimbali.

 Hata vikao nikiwa Mbeya pale kujadili masuala mbalimbali nikitaka niende kwenye muziki ninaweza kurekodi, ila nikashindwa kurekodi video, kufanya media tour.

Mtu anakupigia simu anataka akuhoji na wewe unajikuta unazungumzia masuala ya nchi. Majukumu yameingia kwenye life. Sasa hivi si kama zamani ukitoa muziki lazima ufanye video, wapo niliofanya nao wimbo, lakini nashindwa kufanya nao video kwa sababu ya kutokuwa na muda. Napenda sana muziki na nitatoa kwa ajili ya mashabiki zangu.