Sungusia achaguliwa kuwa Rais TLS

Wakili Harold Sungusia.

Arusha. Wakili maarufu nchini, Harold Sungusia amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) katika uchuguzi uliofanyika leo Jumamosi Mei 13, 2023.

Sungusia ambaye mwaka jana pia aligombea nafasi hiyo na kushindwa na Rais aliyemaliza muda wake Profesa Edward Hosea. Jana ametangazwa kushinda baada ya kupata kura  748.

Mpinzani wake Wakili Reginald Shirima alipata kura 77 licha ya kuibuka katika uchuguzi huo na sera ya kuifanya TLS  kuendelea kuwa chama cha kitaaluma na siyo chama cha kiharakati.

Akitangaza matokeo hayo mwenyekiti wa kamati ya uchuguzi TLS, Wakili Mwandamizi Charles Rwechungura alisema kura zilizopigwa katika uchuguzi huo zilikuwa 825 na hakuna ambayo imeharibika.

Rwechungura amesema katika nafasi ya makamu wa Rais Wakili Aisha Sinda ameshinda  baada ya kupata kura 527.

Amesema Wagombea wengine Revocatus Kuuli alipata kura 32 na Emmanuel Agostino kura 261.

Baada ya kutangazwa matokeo hayo shangwe ilitawala ukumbini na mawakili kumbeba juu juu Sungusia.

Akizungumza baada ya kutangazwa kushinda Sungusia aliwashukuru mawakili kwa kumchagua kwa kura nyingi na kuahadi atatekeleza yote ambayo aliahidi.

Miongoni mwa ahadi zake TLS kushirikiana vyema katika mchakato wa katiba mpya, kuongeza mapato ya chama na kukabiliana na changamoto za kimaadili kwa mawakili.

Baadhi ya mwakili wamepongeza ushindi wa Sungusia na kueleza wanaimani atairejesha TLS kuwa mshauri wa serikali na umma katika masuala ya kisheria.

Wakili Shilinde Ngalula amesema hawana hofu na Sungusia kwani ni wakili makini, mzoefu na anauwezo mkubwa kuongeza TLS.