Taasisi yatoa mafunzo kudhibiti vifo vya watoto

Naibu Waziri wa Elimu, Omar Kipanga akizungumza baada ya kupata maelezo kuhusu matumizi ya vifaa hivyo vya kuhudumia watoto wachanga.
Muktasari:
- Taasisi ya afya Ifakara imetoa mafunzo kwa wataalamu wa vifaa tiba na kukabithi vifaa vya Sh80 milioni.
Arusha. Taasisi ya Afya ya Ifakara ya kupitia Mpango wa imetoa mafunzo kuhusu vifaa tiba kwa wataalamu wa idara na kukabithi vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia watoto wachanga vyenye thamani ya Sh80 milioni katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).
Akizungumza baada ya kutoa mafunzo hayo ya siku tano jana Oktoba 23 jijini hapa, kiongozi wa Teknolojia Muhimu za Kuhudumia Watoto Wachanga (NEST360) kutoka taasisi ya Ifakara, Donat Shamba amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wataalamu wanaotumia umeme na vifaa tiba na hatimaye ili kupunguza vifo vya watoto.
Amesema vifaa hivyo vitawarahishia wataalamu hao kwa kufundishia wanafunzi hao kwa vitendo na hata watalaamu wengine kunufaika na huduma hiyo ili kupata wataalamu waliobobea katika fani hiyo.
“Tayari tumeshatoa mafunzo kama hayo na kutoa vifaa tiba katika Chuo kikuu cha Mbeya na Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.
“Lengo ambapo lengo ni kuisaidia juhudi za serikali kupunguza vifo vya watoto wachanga, kwani wataalamu hao watakuwa mabalozi wazuri kwa wengine ambao hawajanufaika na kupata mafunzo haya," amesema Shamba.
Naye Naibu Waziri wa elimu, Omar Kipanga ameipongeza taasisi ya Afya ya Ifakara akisema wanapaswa kuigwa kwani Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa viwanda, hivyo vifaa hivyo vitasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo ya NEST, Josephat Mutakyamilwa ametaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni pamoja na mashine ya kuvuta maji machafu yaliyoziba njia ya hewa kwa mtoto, mashine ya kupimia sukari kwa watoto, mashine ya kupimia ugonjwa wa manjano, na mashine ya kutibu ugonjwa huo.
Ametaja vifaa vingine ni pamoja na mashine ya kutunza joto kwa watoto wanaohitaji joto ambayo inasaidia kupumua kwa watoto wachanga pamoja na mashine ya kutoa Oxygen.
Naye mwalimu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Masood Mbelwa, amesema baada ya kupata mafunzo hayo watawafundisha wanafunzi wao namna ya kutengeneza vifaa tiba hivyo ili wanapohitimu mafunzo yao wawe na elimu ya vitendo na kuweza kuajiriwa kwa urahisi.