Tacaids kukusanya Sh1 bilioni Kili challenge 2022
Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania(TACAIDS), Dk Leonard Maboko akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikiana na Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGM) imesema inatarajia kukusanya Sh500 milioni hadi Sh1 bilioni kupitia kampeni yake ya "Kili challenge 2022" itakayo itazinduliwa mkoani Kilimanjaro Julai 14 mwaka huu.
Moshi. Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) kwa kushirikiana na Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGM) imesema inatarajia kukusanya kiasi cha Sh500 milioni hadi Sh1bilioni kupitia kampeni yake ya ‘Kili challenge 2022’ ambayo itazinduliwa mkoani Kilimanjaro Julai 14 mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo Julai 5 na Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk Leonard Maboko wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoa wa Kilimanjaro kuelekea tukio la uzinduzi wa harambee ya uchangiaji wa fedha kwa ajili ya shughuli za udhibiti wa Ukimwi Julai 14, mwaka huu.
Dk Maboko amesema mwaka huu wameendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, hivyo kwa kushirikiana na GGM wanatarajia kuanza kampeni ya kupanda mlima Kilimanjaro ifikapo Julai 15 hadi 21.
"Fedha zitakazopatikana zaidi ya nusu zinaenda kwenye NGO's ambazo mara nyingi zinakuwa zinaendeshwa na watanzania kutusaidia kwenye jamii katika mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi.
"Kupitia hizi shughuli za kupanda mlima kwa miaka 20 fedha zilizopatikana katika kipindi hicho ni takribani Sh12 bilioni na kila mwaka kipindi cha nyuma tulikuwa tukipata Sh500 hadi 700milioni na mwaka huu tunaamini hatutakosa Sh500milioni hadi Sh1 bilioni na ndio lengo letu hili," amesema Dk Maboko.
Pamoja na mambo mengine amesema takwimu zinaonyesha kuwapo kwa ongezeko la maambukizi mapya ya Ukimwi hususani kwa makundi maalum yaliyo katika hatari kubwa ya mambukizi ambapo hadi kufikia mwaka 2020 idadi ya Watanzania wanaioshi na virusi vya Ukimwi imefikia watu milioni 1.7 na maambukizi mapya kwa mwaka ni watu 68,000.
"Makundi yaliyo katika hatari ya kupata maambukizi ya VVu ni vijana, wanaotumia madwa ya kulevya, wanaofanya biashara ya ngono, madereva malori yaendayo masafa marefu, wafanyakazi wa kwenye mashamba makubwa na jamii za wavuvi na wafanyakazi wa migodini," amesema na kuongeza
"Vifo vinavyotokana na Ukimwi ndani ya miaka 10 iliyopita tumepunguza karibu asilimia 50 ya vifo, mwelekeo ni mzuri maana maambikizi yanapungua, vifo navyo vinapungua kwasababu watu wanapima, wanaanza dawa na wengine wanaendelea kunywa dawa," amesema Dk Maboko.
Naye Mkuu wa Mkoa huo Stephen Kagaigai amesema lengo la kufanya harambee hiyo ni uchangiaji wa fedha kwa ajili ya mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini kwa kulenga zaidi jamii zilizoko kwenye mazingira hatarishi ya maambukizi ya VVU na kupunguza ayhari za Ukimwi.
"Kupitia tukio hili tunatarajia kupata fedha zitakazosaidia katika mwitikio wa VVU na Ukimwi nchini na kuwafikia walengwa wengi zaidi wakiwemo watoto yatima ambao waliondokewa na wazazi wao kwa janga la Ukimwi waliopo ndani na nje ya shule," amesema Kagaigai