Taka ngumu bado tatizo, wadau washauri upandaji miti

Afisa mtendaji wa Benki ya Standard chartered Tanzania, Herman kasekende, aliyevalia kofia ya bUluu akifanya usafi katika ufukwe wa kibo, Picha na Emmanuel Msabaha

What you need to know:

  • Wadau watakiwa kutunza mazingira kwa kupunguza taka ngumu huku wakishauriwa kupanda miti.

Dar es Salaam. Takwimu za mtandao wa Statista zinaonyesha kiwango cha taka ngumu kinazidi kuongezeka duniani na kinatarajiwa kufikia tani za ujazo bilioni 3.4 hadi kufikia mwaka 2050.

Ongezeko hilo la taka ngumu ni sawa na asilimia 70 ikilinganishwa na zile zilizokuwepo hivi sasa, huku takwimu hizo zikionyesha pia ni asilimia 20 tu ya taka ngumu duniani zinafanyiwa urejeleshwaji.

Afisa Mwendeshaji wa kampuni ya ‘Recycler Limited’, Javan Jerome amesema kampuni yao inafanya kazi ya kuzirudisha taka ambazo zinaharibu mazingira katika mzunguko wa matumizi.

Hayo ameyazungumza katika maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani waliyofanya sambamba na Benki ya Standard Chartered, Tanzania kwa kusafisha ufukwe wa bahari, kibo jijini Dar es Salaam.

“Tunachofanya ni kuhakikisha taka ambazo zinapaswa kurejeleshwa, zinachukuliwa ili kutumika katika matumizi mengine,’’amesema.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi katika fukwe za kibo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Herman Kasekende amesema benki yao inatambua umuhimu wa kutunza mazingira hivyo, wamedhamiria kuendeleza utamaduni wa utunzaji wa mazingira katika jamii.

“Benki yetu siku zote tumekuwa tukiongozwa na azma yetu ya kuwa na mifumo ya kibishara yenye uendelevu. Tunatambua kwamba mafanikio yetu yanahusiana sana na ustawi wa jamii ambazo tunafanya kazi,”amesema Kasekende.

“Kama taasisi ya kifedha, tuna fursa ya pekee ya kuleta athari chanya kwa kuwekeza katika suluhisho endelevu na kusaidia jitihada zinazokabiliana na changamoto za mazingira,”ameongeza.

Aidha katika jitihada hizo za kutunza mazingira Kasekende amesema kuwa benki yao imepanda miti zaidi ya 3,000 hadi sasa, huku akieleza kuwa watajitahidi kubuni huduma za kifedha zinazounga mkono nishati mbadala, kuchochea uwekezaji wa kijani.