Takukuru yamuomba CAG kukagua Sh900 milioni Shinyanga

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari.

What you need to know:

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Shinyanga imemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua mkopo wa Sh900 milioni uliotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Halmashauri ya Shinyanga kwa ajili ya kupima viwanja.

Shinyanga. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Shinyanga imemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua mkopo wa Sh900 milioni uliotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Halmashauri ya Shinyanga kwa ajili ya kupima viwanja.

Akitoa taarifa ya kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2022/23 leo Alhamisi Mei 25, 2023, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy amesema uchunguzi wa awali umebaini fedha hizo zimewekwa kwenye akaunti tofauti zenye matumizi mbalimbali.

Amesema kutokana na kubaini changamoto hiyo wamemuandikia barua CAG, Charles Kichere kuomba ukaguzi maalum wa fedha hizo.

“ Tumeanza kufanyia kazi suala hili na tukabaini fedha hizo zimeingizwa akaunti tofauti ambazo zinamatumizi mbalimbali, niwahakikishie kwamba tumeomba ukaguzi maalumu kwa Halmashauri hiyo kutoka kwa CAG. Tumeshapeleka maombi, akishafanya uchunguzi na sisi tunakamilisha uchunguzi wetu,”amesema Kessy

Akizungumzia miradi mingine, Kessy amesema wamebaini dosari ndogo ndogo kwenye miradi 44 yenye thamani ya Sh5.1 bilioni iliyochunguzwa kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu na kuagiza  kufanyiwa kazi.

 Amesema miradi ya maendeleo iliyofuatiliwa ni  Sekta ya Afya, Elimu, Maji, Ujenzi na mikopo ya asilimia 10 ambapo miradi miwili yenye thamani ya Sh86 milioni ilionekana kuwa na mapungufu na hatua mbalimbali zilichukuliwa.

Miradi hiyo ni pamoja na vyumba viwili shule ya sekondari Bunambiyu na vyumba viwili shule ya sekondari Ikonda ambavyo baadhi ya madirisha yalikuwa na nyufa na mikanda ya bodi kuachia nyufa.