Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tamu, chungu kufungwa kwa Ziwa Tanganyika

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa wauzaji hao, bei ya dagaa hao maarufu wa Kigoma, ilianza kupanda baada ya tangazo la kufungwa kwa ziwa hilo mapema mwaka huu kutoka Sh20,000 hadi Sh50,000 kwa kilo.

Kigoma. Zikiwa zimepita siku tatu tangu Ziwa Tanganyika lifungwe kwa shughuli za uvuvi, dagaa wamepanda bei hadi kufikia Sh70,000 kwa kilo, huku wauzaji wakilalamikia makali ya maisha.

Kwa mujibu wa wauzaji hao, bei ya dagaa hao maarufu wa Kigoma, ilianza kupanda baada ya tangazo la kufungwa kwa ziwa hilo mapema mwaka huu kutoka Sh20,000 hadi Sh50,000 kwa kilo.

Wanasema ilipofika Mei 14, bei ilipanda hadi Sh60,000 na jana ilifikia Sh70,000 ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Leo Ijumaa Mei 17, 2024, Mwananchi ilitembelea soko la Kibirizi mkoani Kigoma na kushuhudia wauzaji wa dagaa wakisubiri wateja, ambao wengi waliishia kuulizia bei na kuondoka.

Mustafa Mohamed, mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, amesema baada ya ziwa kufungwa bei ya dagaa imepaa na kuwafanya wakose wanunuzi.

“Mfumo tunaoenda nao kimaisha kwetu umekuwa mgumu sana kulingana na bidhaa tulizonazo na kazi tulizonazo. Tangu asubuhi ukifika hapa unaishia kukaa tu, huuzi chochote hadi jioni unaondoka hata mia mfukoni huna,” amesema Mohamed.

Amesema wanunuzi wakiuliza bei wakaelezwa ni Sh70,000 kwa kilo wanaondoka na hali hiyo inawaweka kwenye wakati mgumu kibiashara.

Mwenyekiti wa Wavuvi Mkoa wa Kigoma, Bakari Almasi amesema bei hiyo imepanda kuanzia kwa wavuvi na wafanyabiashara wanaokusanya dagaa mwaloni wanauziwa Sh50, 00 kisha wenyewe kuwauzia wajasiriamali Sh70, 000, zikijumuisha gharama za usafirishaji.

“Bei ya dagaa inategemea upatikanaji wa dagaa ulivyo, zikiwa adimu bei inapanda, zikiwa nyingi inashuka,” amesema.

Si wauza dagaa pekee wanaolia, Shabani Kazuba, anayefanya biashara ndogondogo pembezoni mwa mwalo wa Kibirizi, amesema kusimamishwa kwa uvuvi kumefanya shughuli zake kukwama kwa kuwa wateja wengi ni wavuvi, ambao haijulikani wametawanyikia wapi.

“Serikali itufikirie, ifikirie jambo, labda kuna mbinu mbadala, lakini kwa hivi sasa hali ni ngumu, mambo hayaendi kabisa. Hakuna wateja, maana yake wateja wengi hapa kwetu ni wavuvi, sasa wavuvi hawaeleweki wameenda wapi, kwa hiyo hali ni ngumu kwa kifupi,” alisema.

Aisha Kibiza, anayefanya biashara ya chakula, ameiambia Mwananchi Digital kuwa amefunga biashara yake kwa sababu hakuna wateja.

Wavuvi katika mwalo wa Katoga mkoani Kigoma wakihamisha nyavu zao za kuvulia mazao ya samaki kutoka mwaloni hapo kupeleka pasipo julikana baada ya Ziwa Tanganyika kufungwa Mei 15 na kutarajiwa kufunguliwa Agosti.

“Nilikuwa napika chakula kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane kwa sababu kazi hii ya uvuvi ipo muda wote, lakini sasa hivi hapa hakuna wa kumuuzia. Si unaona hakuna mvuvi hata mmoja, inabidi nigeukie biashara nyingine ambayo mpaka sasa hivi sijui ni ipi,” amesema Aisha.


Bei ya dagaa mikoani

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini baadhi ya mikoa dagaa wa Kigoma hawapatikani na sababu ikitajwa ni bei na upatikanaji wake.

Mikoa ambayo dagaa hao hawapatikani ni Mara, Geita, Kagera, huku Mwanza kilo moja ikiuzwa Sh70,000, Tabora kati ya Sh30,000 na Sh40,000 na Shinyanga wakiuzwa kwa mafungu kati ya Sh1,000 hadi Sh5,000.

“Kufikia siku ya leo dagaa hao katika Soko kuu la Mwanza wanauzwa Sh70,000 kwa kilo. Wamekuwa adimu,” amesema Meshack Katambi.

Mkazi wa Mabatini mkoani Tabora, Shella Adam amesema tangu mwaka huu uanze, dagaa wa Kigoma hawapatikani mkoani humo.

“Mara ya mwisho nimeenda kuwanunua sokoni nilikuta fungu la dagaa kama watano Sh1,000… kwetu dagaa hao wana gharama sana,” amesema.


Wavuvi waondoa zana

Kama ambavyo Serikali ilielekeza shughuli za uvuvi zisimame itakapofika Agosti 15, mwaka huu, wavuvi wametii amri hiyo na Mwananchi Digital imeshuhudia wakisogeza mitumbwi katika mwalo wa Katonga na kuipanga vizuri pembeni, huku nyavu wakizifunga, kuzipakia na kuzihamisha pasipojulikana.

Mwandishi alipotaka kuzungumza nao, walikataa wakidai wameshazungumza sana, lakini hawasikilizwi.

“Hatuna cha kuongea, Serikali imeshaamua sisi tuseme nini,” amesema mmoja wa wavuvi hao katika mwalo wa Katonga.


Sababu ziwa kufungwa

Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdalah Ulega alisema Serikali imefikia hatua ya kufunga ziwa hilo baada ya makubaliano na nchi zinazozungukwa na ziwa hilo – Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ili kuruhusu samaki kuzaliana kwa wingi na kudhibiti uvuvi haramu, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Chini ya makubaliano hayo, ziwa hilo litapumzishwa kwa miezi mitatu kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 kila mwaka; kwa kipindi cha miaka mitatu.

Katika kipindi hicho, nchi zinazoshirikiana ziwa hilo zitafanya utafiti wa kiwango cha samaki, utafiti wa kibaolojia na matokeo ya kiuchumi kwa watu wanaolitegemea kimaendeleo.