Tanesco yadaiwa kutoa zabuni ya Sh53.71 bilioni kwa kampuni isiyo na vigezo

Muktasari:

  •  Licha ya kasoro zilizobainika, timu ya tathmini ilipendekeza mzabuni apewe tuzo kufuatia mazungumzo kuhusu hitilafu zote za kiufundi zilizotajwa.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetoa zabuni kwa Kampuni ya TBEA CO LTD kwa ajili ya kusanifu, kuleta, kusimika na kuzindua kituo kidogo cha umeme wakati kampuni hiyo haina vigezo.

Hayo yameelezwa katika Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya Mkaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23 iliyowasilishwa bungeni jana Aprili 15, 2024.

Alipoulizwa na Mwananchi jana, Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Kenneth Boymanda alisema kilichomo ndani ya ripoti hiyo ni hoja za CAG na kwamba shirika hilo linaandaa majibu yake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanesco iliingia mkataba na kampuni hiyo Juni 2, 2023 kwa ajili ya kusanifu, kuleta, kusimika na kuzindua kituo kidogo cha umeme Dundani cha 220/33Kv, 2x120MVA kwa bei ya mkataba ya Sh53.71 bilioni.  

Hata hivyo, katika ripoti hiyo, CAG amesema alibaini kamati ya tathmini ilipendekeza tuzo kwa Kampuni ya TBEA CO LTD Loti Na. 2, mzabuni hakukidhi baadhi ya mahitaji ya kiufundi.

“Kuhusu transfoma, mzabuni alikuwa na uzoefu wa ugavi wa miaka 26 kinyume na mahitaji ya miaka 30, kuhusu kivunja saketi, hakuwa amefikia mahitaji ya uzoefu wa miaka 30, kuhusu transfoma ya mkondo na transfoma ya volti, hakuwa amefikia mahitaji ya uzoefu ya miaka 30.

“Kuhusu mfumo wa KV 33 GIS, mzabuni aliwasilisha thamani ya mkondo wa hitilafu kama KA16 badala ya mahitaji ambayo ni KA40 na kiwango cha juu cha mzunguko mfupi wa KA16 badala ya KA25.

“Licha ya kasoro zilizobainika, timu ya tathmini ilipendekeza mzabuni apewe tuzo kufuatia mazungumzo kuhusu hitilafu zote za kiufundi zilizotajwa hapo juu,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo, CAG amesema pamoja na kwamba Bodi ya zabuni kuona kasoro zote za kiufundi zilizobainishwa kuwa ni ndogo zinazoweza kurekebishwa na mzabuni, jambo hilo ni kinyume na Kanuni ya (204) (1) (2) (f), 205 na 206 (2) za ununuzi wa umma za mwaka 2013.

“Ni maoni yangu kuwa, kasoro zote za kiufundi zilizobainishwa wakati wa tathmini zilikuwa ni kasoro kubwa na muhimu kwa mujibu wa mwongozo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma.

“Hivyo, kukubaliwa kwa kasoro hizo kunaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa wigo, ubora au utendaji wa kazi zilizoainishwa kwenye mkataba. Hii inaweza kuathiri nafasi ya ushindani ya wazabuni wengine waliowasilisha zabuni zenye mwitikio mkubwa.