Tanroads, Tarura kukarabati miundombinu Hanang

Muktasari:

  • Kazi ya kuondoa tope katikati ya barabara, mitaroni na maduka yaliyopo pembeni mwa barabara wilayani Hanang mkoani Manyara imeendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa chini ukihusisha taasisi za Serikali na wananchi.

Hanang. Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), wameunganisha nguvu kukarabati miundombinu ya barabara katika Mji Mdogo wa Katesh, wilayani Hanang.

Itakumbukwa kuwa Desemba 3, 2023, mvua kubwa iliyonyesha wilayani hapa na kusababisha maporomoko ya matope kutoka katika Mlima Hanang yaliyosababisha vifo vya watu 69, majeruhi zaidi 116,uharibifu wa mali na miundombinu

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatano Desemba 6, 2023, mjini Katesh, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema wameamua kuungana ili kuhakikisha mawasiliano ya barabara ikiwemo barabara kuu ya Babati - Singida inasafishwa ili safari ziendelee bila changamoto.

"Jana na leo hata nyie mnaona tofauti, mnaona watu wameanza kufungua maduka na kufanya biashara, haikuwa hivi na tuaamini wafanyabiashara wengi, wataendelea kufungua maduka na biashara nyingine na hivyo kuruhusu maisha kuendelea," amesema na kuongeza:

"Baada ya kufungua barabara ikiwemo barabara kuu ya Singida hadi Babati tutahakikisha inapitika na kwa kushirikiana na Tanroads na Tarura tumetengeneza timu ya pamoja kusafisha barabara kubwa na zile za ndani."

Tanroads na Tarura, wanashirikiana na vikosi vya uokoaji ikiwemo Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) na wananchi  kuondoa tope lililojaa kwenye barabara, mitaro ya barabara na maduka yaliyopo pembeni mwa barabara.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, maafa hayo yalisababishwa na miamba dhoofu ya Mlima Hanang’.

Matinyi amesema, miamba hiyo ilinyonya maji ya mvua hiyo na hivyo kusababisha mgandamizo huku sehemu ya mlima huo ikishindwa kuuhimili na hivyo kumeguka, na kutengeneza tope lililoporomoka.

Kwa mujibu wa Matinyi,tope hilo lilifuata mkondo wa Mto Jorodom, ambapo lilizoa mawe na miti na kuipeleka katika makazi ya watu ambayo yako pembezoni mwa mto huo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hadi jana Desemba 5, 2023 watu 65 walipoteza maisha, 116 wakijeruhiwa na wengine wakipoteza makazi yao ambapo yamefunikwa na tope, mawe makubwa na magogo ya miti.