Tanswift yazindua huduma ya usafirishaji mtandaoni

Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanswift, Japhet Tesha akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Mei 13, 2023 baada ya uzinduzi wa Swiftcabb jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kampuni ya usafirishaji ya Tanswift imezinndua huduma ya usafirishaji mtandaoni huku ikilenga kutoa ajira kwa vijana na wanafunzi wa vyuo.

Akiyasema hayo leo Jumamosi Mei 13, 2023 Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanswift, Japhet Tesha katika hafla ya uzinduzi wa bidhaa mpya ya Swiftcabb inayomilikiwa na kampuni ya usafirishaji ya Tanswift. Amesema huduma hiyo imetoa fursa kwa vijana hasa wanafunzi kuwa mabalozi na kupata kipato wakiwa bado wapo vyuoni huku ikilenga kutoa huduma ndani ya mkoa na nje ya mkoa. 

"Kwa kuzindua tumeanza na Mkoa wa Dar es Salaam lakini tutaendelea katika maeneo ya Arusha, Mwanza, Dodoma na Zanzibar. Mabalozi ni wanafunzi wa vyuo vikuu kwa sababu tumelenga kuwapa maarifa ya kupata kipato wakiwa bado vyuoni," amesema.

Huduma hiyo imelenga kutoa huduma ya usafiri kwa gharama nafuu na ya uhakika kwa Watanzania.

Pia wasafirishaji Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kufuata sheria za barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Miongoni mwa mambo mengine muhimu, pia wametakiwa kufuata michoro na alama za barabarani ili kuepuka kusababisha ajali kwao, abiria na watembea kwa miguu.

Rai hiyo imetolewa na Inspekta Faustina Ndunguru kutoka Makao Makuu Kitengo cha Usalama Barabarani, Dawati la Elimu kwa Umma.

Inspekta Ndunguru amesema watumiaji wa huduma hiyo wanapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani na kutambua kwamba haziruhusu kupakia watoto wenye umri chini ya miaka tisa katika bodaboda.

"Tumewakumbusha umuhimu wa kupakia abiria mmoja kwa waendesha bodaboda bila kusahau kufuata sheria za usalama barabarani hasa kutofuata sheria ya kupakia watoto katika bodaboda chini ya umri wa miaka tisa," amesema Inspekta Ndunguru.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,   Florah Mgonja amesema kampuni hiyo itachangia kutoa ajira kwa vijana na kukuza pato la nchi.

Mgonja amesema maofisa usafirishaji wanatakiwa kuwa mabalozi kwa madereva wengine na kuacha tabia ya kukiuka sheria za barabarani.

"Maofisa usafirishaji mmemepewa fursa ya kupata elimu ya kuwa mabalozi wa kutumia vyema usafiri wa mtandaoni na kujiongezea kipato ili muacha kukaa kijiweni," amesema Mgonja.