Tanzania, EU zajiwekea mkakati nishati safi ya kupikia
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba wakati akizungumza katika uzinduzi wa Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia Juni 10, 2026
Muktasari:
- Takwimu zinaonesha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 16 mwaka 2022 hadi asilimia 28.6 kufikia Machi 2026
Arusha. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), wameweka mikakati ya kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ili kufikia lengo la asilimia 80 ya kaya kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
Mikakati hiyo imejadiliwa katika kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia la siku mbili lililoanza jijini Arusha, likiwakutanisha wadau wa sekta ya nishati, taasisi za Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na watafiti.
Akizindua kongamano hilo leo Jumatano Juni 10, 2026, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema Serikali imejipanga kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaongezeka kwa kasi ili kufikia malengo ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034.
“Nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kulinda afya za wananchi, kuwawezesha wanawake na vijana pamoja na kuhifadhi mazingira. Kongamano hili limetuwezesha kuoanisha sera, mifumo ya ufadhili na mikakati ya ushirikishwaji wa jamii ili kuharakisha utekelezaji,” amesema Makamba.
Amesema juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, zimechangia kuongeza uelewa wa wananchi na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa za kupikia.
Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christine Grau amesema Umoja wa Ulaya umetenga Euro 30 milioni (Sh92 bilioni), kusaidia upanuzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Amesema fedha hizo zitatumika kuimarisha masoko ya nishati endelevu, kulinda mazingira na kuchochea fursa za kiuchumi kupitia uwekezaji katika sekta hiyo.
“Huu ndio uwekezaji mkubwa zaidi wa Umoja wa Ulaya katika sekta ya nishati safi ya kupikia katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ufadhili huu unalenga kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na kuharakisha matumizi ya nishati safi barani Afrika,” amesema.
Hata hivyo, takwimu zinaonesha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 16 mwaka 2022 hadi asilimia 28.6 kufikia Machi 2026.
Mafanikio hayo yamechangiwa na ruzuku ya mitungi ya gesi ya LPG, kupunguzwa kwa gharama za umeme, kuondolewa kwa baadhi ya kodi kwenye vifaa vya nishati safi ya kupikia pamoja na uwekezaji wa sekta binafsi.
Lakini matumizi ya kuni na mkaa bado yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwa kaya nyingi nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Ufundi wa UNCDF, Peter Malika amesema kupitia programu ya CookFund, taasisi hiyo imeendelea kusaidia biashara na wabunifu wanaotoa suluhisho za nishati safi ya kupikia.
Amesema tangu kuanzishwa kwa programu hiyo, Dola 11.2 milioni za Marekani (Sh29.4 bilioni) zimetolewa kupitia ruzuku 102 kwa biashara ndogo na za kati, hatua iliyochangia kuzalisha ajira takribani 27,000 nchini.
Amesema zaidi ya kaya 413,000 zimewezeshwa kupata huduma za nishati safi ya kupikia, zikiwanufaisha karibu watu milioni 1.94 nchini kote.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), za watu bilioni 2.3 duniani bado hawana huduma za nishati safi ya kupikia.
Hivyo, wadau walioshiriki kongamano hilo wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wafadhili na sekta binafsi ili kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinapata nishati safi, salama na nafuu ifikapo mwaka 2034.