Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania, Misri zakubaliana kuongeza biashara, kuunganisha bandari

Muktasari:

  • Misri ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini, ikishika nafasi ya nane kati ya nchi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania, ikiwa na miradi 61 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.5, ambayo imezalisha ajira kwa Watanzania zaidi ya 4,000 katika sekta za nishati, viwanda, ujenzi, kilimo, utalii na huduma nyingine.

Dar es Salaam. Tanzania na Misri zimekubaliana kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kwa kukuza biashara na uwekezaji, kuunganisha bandari, kuwekeza katika kilimo na mifugo pamoja na kuimarisha usafiri wa anga na baharini, hatua inayotarajiwa kufungua masoko mapya ndani na nje ya Afrika.

Makubaliano hayo yamewekwa wazi leo Julai 18, 2026 na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya mazungumzo rasmi na Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi, ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Samia amesema viongozi hao wamebaini kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Misri bado ni kidogo ikilinganishwa na fursa zilizopo, hivyo wamekubaliana kuongeza ushirikiano huo.

"Tumekubaliana sote kwamba kiwango cha biashara kati yetu bado kiko chini, lakini kuna fursa kubwa za kukikuza. Kwa hiyo tumekubaliana kukuza biashara, lakini pia uwekezaji kati ya nchi zetu," amesema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fattah El-Sisi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais Samia amesema Misri ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini, ikishika nafasi ya nane kati ya nchi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania.

Amesema kwa sasa wawekezaji kutoka Misri wana miradi 61 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.5, ambayo imezalisha ajira kwa Watanzania zaidi ya 4,000 katika sekta za nishati, viwanda, ujenzi, kilimo, utalii na huduma nyingine.

"Licha ya takwimu hizi kutia moyo, bado tunaona kuna nafasi kubwa zaidi ya kuongeza biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu," amesema Rais Samia.


Kilimo na mifugo

Katika sekta ya kilimo, Rais Samia amesema wamekubaliana kutumia uzoefu wa Misri katika teknolojia za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.

Amesema Afrika bado hutumia kati ya Dola za Marekani bilioni 70 hadi 100 kila mwaka kuagiza bidhaa za chakula, hali inayoonyesha umuhimu wa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani.

"Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na pia tunashika nafasi ya pili Afrika kwa idadi ya mifugo. Misri imepiga hatua kubwa katika teknolojia za umwagiliaji na uzalishaji wa mbegu. Tumeamua kushirikiana ili kukuza sekta hii," amesema.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Misri pia imeonyesha nia ya kuwekeza katika sekta ya mifugo nchini, ambapo pande hizo zimekubaliana kutumia Ranchi ya Ruvu kwa uwekezaji wa pamoja.

Amesema pia amewaalika wawekezaji wa Misri kushirikiana na taasisi za Tanzania zenye maeneo makubwa ya kilimo na mifugo, ikiwemo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Magereza na Shirika la Taifa la Ranchi (Narco).


Safari za ndege

Katika sekta ya usafiri wa anga, Rais Samia amesema viongozi hao wamekubaliana kuongeza ushirikiano kati ya mashirika ya ndege ya nchi hizo.

Amesema kwa sasa shirika la EgyptAir linafanya safari tatu kwa wiki kwenda Tanzania, huku Serikali ikilitaka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kujiandaa kuanzisha safari za kuelekea Misri.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo rasmi na ujumbe wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, uliongozwa na Rais wa nchi hiyo, Abdel Fattah El-Sisi, leo Julai 19, 2026 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Aidha, amesema mazungumzo yataendelea kuhusu kuanzisha ushirikiano wa usafiri wa baharini utakaounganisha bandari za Dar es Salaam, Bagamoyo, Safaga na nyingine za Misri ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kupanua masoko kati ya nchi hizo.

Mbali na makubaliano ya kuongeza biashara, uwekezaji na ushirikiano katika kilimo, Tanzania na Misri zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika diplomasia, nishati, viwanda vya dawa na vifaa tiba, maendeleo ya bandari, usafiri wa baharini pamoja na kubadilishana utaalamu ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi ya nchi hizo mbili.

Rais Samia amesema wamekubaliana pia kuendelea kuratibu misimamo yao katika masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Rais El-Sisi amesema Misri iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mipya ya kimkakati.

Katika hatua nyingine, Rais El-Sisi amesema nchi yake imejitolea kuongeza programu za kubadilishana wataalamu na kuwajengea uwezo maofisa wa Tanzania katika sekta mbalimbali.

"Tutatumia uwezo wetu wote kuhakikisha tunaongeza programu za kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo maofisa wa Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo," amesema.

Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fattah El-Sisi akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa Kikwete leo Julai 19, 2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uwezo wa kitaalamu na kuongeza tija katika utekelezaji wa miradi ya pamoja.

Amesema pamoja na kuendelea kuendeleza Bandari ya Dar es Salaam, kutakuwa pia na ushirikiano katika huduma za usafiri wa baharini kati ya bandari za Tanzania na Misri.

"Tumeelezea utayari wetu wa kushirikiana katika maendeleo ya bandari, huduma za lojistiki na kuanzisha usafiri wa baharini kati ya Misri na Tanzania ili kurahisisha biashara na usafirishaji wa bidhaa," amesema.


Msimamo wa pamoja wa kikanda

Katika mazungumzo yao, viongozi hao pia walijadili hali ya usalama na maendeleo katika Afrika na Mashariki ya Kati.

Rais El-Sisi amesema Misri inaithamini Tanzania kwa msimamo wake wa kuendeleza ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

"Misri inaipongeza Tanzania kwa msimamo wake chanya katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu. Pia tumebadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yanayohusu Afrika na Mashariki ya Kati," amesema.

Amesema ushirikiano huo wa kisiasa utaendelea kuwa msingi wa kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kukuza maendeleo ya kiuchumi kati ya Tanzania na Misri.


Jukwaa la Wafanyabiashara

Rais El-Sisi aliambatana na jopo la wafanyabiashara 35 kutoka Misri walioshiriki katika Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Misri, lililowakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi hizo mbili.

Katika jukwaa hilo, nchi hizo zilifikia uamuzi wa kuanzisha kituo cha kimkakati cha usafirishaji wa mizigo kati ya Dar es Salaam na Cairo, kitakachounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Ain Sokhna kupitia Bahari ya Hindi, Bahari Nyekundu na Bahari ya Mediterania.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Tanzania na Misri zimedhamiria kukuza biashara baina yao kupitia fursa zilizopo, ikiwemo sekta ya uchukuzi ambayo ndiyo inarahisisha biashara.

"Kituo hiki kitafungua njia mpya ya biashara kati ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, Afrika Kaskazini, Mashariki ya Kati, Ulaya na masoko mengine ya dunia.

"Nina furaha kubwa kutangaza kuwa, chini ya wataalamu wa Wizara ya Uchukuzi, Tanzania itatembelea Misri mwezi huu wa Julai ili kuhakikisha majadiliano yote kuhusu mradi huu yanakamilika rasmi," amesema Profesa Mbarawa.

Kwa upande wake, Waziri wa Uwekezaji na Biashara za Kimataifa wa Misri, Hassan El Khatib amesema Tanzania na Misri ni viungo muhimu vya biashara, wakati Tanzania ikiunganisha dunia na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Misri nayo inaunganisha dunia na bara la Afrika na Ulaya.

Amesema wawekezaji wa Misri wanakuja kuwekeza Tanzania katika sekta saba tofauti, jambo ambalo limechochewa na kuimarika kwa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

"Tumepiga hatua katika ushirikiano wetu, lakini tunahitaji kwenda mbele zaidi katika biashara na uwekezaji kwa manufaa ya wananchi wetu," amesema waziri huyo.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Misri inaisaidia sekta binafsi ya Misri kuja kuwekeza na kufanya biashara Tanzania, hivyo amewaalika wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kufanya biashara nchini kwake.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Tanzania na Misri zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mbalimbali, akitolea mfano kampuni ya Arab Contractors iliyofanya utafiti wa namna ya kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, hatua iliyosaidia kujengwa kwa madaraja ya juu (flyover) yaliyopo sasa.

Amesema kufikia mwaka 2030, Dar es Salaam itakuwa na hadhi ya jiji kubwa (mega city), ikiwa na watu milioni 10, hivyo maandalizi yameanza, hususan katika kuboresha miundombinu ili kukidhi mahitaji yanayotarajiwa.

"Tutakwenda kujifunza kwenye majiji kama Cairo ili kujifunza namna ya kupangilia mji wetu. Tumedhamiria kutumia mfumo wa PPP (ubia kati ya Serikali na sekta binafsi), tunawakaribisha wawekezaji mbalimbali waje tushirikiane," amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza), Gilead Teri amewatambulisha wafanyabiashara kuhusu mamlaka hiyo, akisema wana Kituo cha Huduma kwa Pamoja (OSC) kinachojumuisha taasisi zote za Serikali zinazohusika na huduma kwa wawekezaji, lengo likiwa ni kurahisisha mchakato wa uwekezaji.

"Yapo mengi ambayo ni bure yamewekwa kwa ajili yenu. Wale wenye ardhi, wenye leseni za madini, tutatumia fursa hizo kuwaunganisha na wawekezaji. Huduma zote hizi tunazitoa bure," amesema.