Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania itakavyovuna Sh5.25 trilioni za uwekezaji kutoka Russia

Muktasari:

  • Katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutapata uwekezaji na biashara wa thamani inayozidi dola 2 bilioni za Marekani. Huu utakuwa uwekezaji mkubwa utakaoifanya Russia kuwa miongoni mwa washirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania

Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kuvutia uwekezaji na biashara zenye thamani ya zaidi ya Dola 2 bilioni za Marekani (Sh5.2 trilioni) kutoka Russia katika kipindi cha miaka mitano ijayo huku sekta ya afya ikitarajiwa kunufaika kupitia uzalishaji wa dozi milioni 20 za chanjo nchini.

Matarajio hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga wakati akitoa taarifa ya matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Russia ambapo alishiriki Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) pamoja na kufanya ziara ya kitaifa.

Balozi Ulanga pamoja na mawaziri, Profesa Kitila Mkumbo wa Mipango na Uwekezaji na Balozi Mahmoud Thabit Kombo wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo Jumapili, Juni 7, 2026 wamekutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuzungumzia ziara hiyo.

Mkutano huo umeratibiwa na kuongozwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Bakari Machumu. Ziara hiyo ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais wa Russia,

ilianza Juni 2  kwa Rais Samia kuondoka nchini na kurejea jana Jumamosi, Juni 6, 2026.

Balozi Ulanga amesema ziara hiyo imefungua milango mipya ya uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Russia huku kampuni kubwa za nchi hiyo zikionyesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali za kimkakati nchini.

“Ukiangalia mazungumzo yote yaliyofanyika kwenye maeneo ya uwekezaji na biashara, tunaamini katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutapata uwekezaji na biashara wa thamani inayozidi Dola 2 bilioni za Marekani. Huu utakuwa uwekezaji mkubwa utakaoifanya Russia kuwa miongoni mwa washirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania,” amesema.

Amesema moja ya maeneo yaliyovutia wawekezaji ni sekta ya afya, ambapo kampuni za Russia zimeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa dawa na chanjo.

“Kampuni hizo zimetueleza ndani ya miaka mitano ijayo zina uwezo wa kushirikiana na Tanzania kuzalisha dozi milioni 20 za chanjo za magonjwa mbalimbali hapa nchini, si kwa ajili ya Tanzania pekee bali pia kwa soko la kikanda,” amesema.

Amesema mafanikio hayo yametokana na ushawishi wa Rais Samia aliyelitumia jukwaa hilo kuitangaza Tanzania kama kitovu cha uwekezaji, biashara na utalii.

Amesema hotuba ya Rais Samia iliyoanza kwa kuitambulisha Tanzania kupitia Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti na visiwa vya Zanzibar ilivutia washiriki wengi waliotaka kupata taarifa zaidi kuhusu nchi.

“Dakika chache za mwanzo za hotuba yake zilitosha kuamsha hamasa kubwa. Banda la Tanzania lilianza kupokea wageni wengi waliotaka kujua zaidi kuhusu vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilizopo na kampuni 20 za utalii zilitaka taarifa za kina,” amesema.


Maeneo ya kimkakati

BaloziUlanga amesema sekta ya madini ya kimkakati ilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyovutia kampuni nyingi za Russia hususan katika miradi ya uranium, nikeli na madini mengine muhimu ya kimkakati sambamba na maendeleo ya teknolojia za kisasa.

Katika madini hayo pia kampuni zimeonesha nia ya kuwekeza katika uchimbaji na uongezaji thamani badala ya kuuza madini ghafi.

Ametaja pia sekta ya nishati hususan mafuta na gesi kuwa imevutia kampuni kubwa za Russia ikiwamo Gaspo ambayo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa gesi duniani.

“Kampuni hizo zimeonyesha nia ya kushiriki katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi nchini Tanzania,” amesema.

Katika sekta ya kilimo amesema wawekezaji wameonesha nia ya kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kilimo, usindikaji wa mazao na kuongeza thamani ya mazao ya Tanzania kabla ya kuuzwa katika masoko ya Russia sambamba na kilimo smart.

Mazao yaliyotajwa kuwa na fursa kubwa ni pamoja na korosho, kahawa, chai na bidhaa nyingine za kilimo zinazozalishwa kwa wingi nchini.

“Sekta ya teknolojia na uchumi wa kidijitali nayo imevutia makampuni ya Russia hasa yale yanayojihusisha na ubunifu wa kidijitali na kampuni change zinazotafuta fursa za kushirikiana na Tanzania katika kukuza uchumi wa kidijitali,” amesema.

Mbali na uwekezaji pia wafanyabiashara wa Tanzania walipata fursa ya kufanya majadiliano ya moja kwa moja na kampuni kubwa kupitia kongamano la biashara lililoandaliwa sambamba na jukwaa hilo.

Ulanga amesema baadhi ya kampuni tayari zimeanza mazungumzo ya kuingiza nchini bidhaa mbalimbali ikiwemo mbolea kutoka Russia, huku yakitafuta pia masoko ya bidhaa za Tanzania katika soko la nchi hiyo.

Amesema hatua inayofuata ni kuanza kufuatilia utekelezaji wa makubaliano na mazungumzo yaliyofikiwa ili kuhakikisha fursa zilizopatikana zinageuka kuwa uwekezaji halisi wenye manufaa kwa uchumi wa Tanzania.


Alichokisema Kitila

Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema manufaa ya ziara hiyo hayaishii kwenye uwekezaji pekee, bali pia yamefungua fursa mpya katika elimu, sayansi na teknolojia.

“Mikataba iliyosainiwa itarahisisha kutambuliwa kwa sifa za wahitimu wa Tanzania na Russia huku wanafunzi wakipata nafasi ya kusoma kwa mfumo wa shahada mbili katika taasisi za nchi hizo,” amesema.

Amesema ushirikiano katika maeneo ya akili bandia, ujifunzaji wa mashine na sayansi ya takwimu pia unatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi katika kukuza uchumi wa kidijitali, wakati makubaliano kati ya taasisi za uwekezaji yatasaidia kuimarisha maandalizi ya miradi, ubia wa kibiashara na ushawishi wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa ya uwekezaji.


Kipindi muhimu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo amesema ziara ya Rais Samia imefanyika katika kipindi muhimu ambacho Russia inaongeza ushirikiano wake wa kiuchumi na kidiplomasia na nchi za Afrika.

Amesema hatua hiyo imeipa Tanzania nafasi ya kujiweka katika mkondo wa nchi zinazolengwa na Russia katika kupanua biashara, uwekezaji na ushirikiano wa maendeleo, huku ikiimarisha nafasi ya nchi katika diplomasia ya uchumi na majukwaa ya kimataifa.

“Mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuongezeka kwa fursa za elimu kwa Watanzania baada ya Russia kuendelea kutoa nafasi za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Tanzania katika ngazi mbalimbali za elimu ya juu. Ushirikiano huo utaongeza idadi ya wataalamu wa Tanzania katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na taaluma nyingine muhimu kwa maendeleo ya taifa,” amesema.