Tanzania, Msumbiji kuongeza ushirikiano kiuchumi

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi gwaride likitoa heshima mbele yao.
Muktasari:
- Rais wa Msumbiji, Felipe Nyusi yupo nchini Tanzania kwa ziara ya siku nne kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan. Leo Jumanne, wamefanya mazungumzo Ikulu ya Dar es Salaam na kesho atafungua Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam maarufu Sabasaba.
Dar es Salaam. Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi kwa kuongeza wigo wa biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili ya kusini wa jangwa la Sahara.
Hatua hii ni matokeo ya ziara ya siku nne ya Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi nchini Tanzania iliyofanikisha mazungumzo ya kuimarisha uhusiano na utiwaji saini hati mbili za makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya afya na uwekezaji.
Leo Jumanne, Julai 2, 2024, Rais Nyusi amekutana na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo kwa pamoja walifanya mazungumzo yaliyolenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa mataifa hayo ambayo yana historia ndefu ya uhusiano wa kidiplomasia.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Rais Samia amesema ya uimara wa mataifa hayo katika uhusiano wa kidiplomasia bado ushirikiano wao wa kibiashara uko chini, hivyo wakuu hao wa nchi wamefikia makubaliano ya kuimarisha hali hiyo.
Amesema takwimu zinaonesha thamani ya biashara kati ya Tanzania na Msumbiji zimeshuka kutoka dola 57.8 milioni mwaka 2022 hadi dola 20.1 milioni mwaka 2023.
Rais Samia amesema mdodoro huo umewashtua hivyo wamekubaliana kufuatia kwa kina kubaini kiini chake ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo cha kuhamasisha biashara eneo la Mtambaswala kwa upande wa Tanzania na Msumbiji ikitajiwa kufanya hivyo kwa upande wa pili wa mpaka.
“Tukiangalia rekodi tunaona bado hatujafanya vizuri kwenye ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, hapa Tanzania kuna wawekezaji wawili tu kutoka Msumbiji, halafu kule Msumbiji wawekezaji kutoka Tanzania ni 16 hii namba iko chini tumekubaliane tuweke nguvu katika eneo hili,” amesema.
Kufanikisha hilo mataifa hayo yamesaini hati ya makubaliano ili kupanua mawanda ya biashara na uwekezaji kuwezesha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi moja kwenda kuwekeza nchi nyingine.
Rais Samia ameeleza pia katika mazungumzo yake na Rais Nyusi wamekubaliana kuziunganisha nchi zao kwenye eneo la usafirishaji ili kuwezesha mchakato wa kuzifanya nchi za Afrika kufikika.
“Msumbiji wana mradi wanateleza kwenye sekta ya miundombinu ambao unalenga kuziunganisha na Zambia, Zimbabwe kama ilivyo sisi tunavyotaka kuungana na Burundi, Rwanda na Congo kupitia reli,” amesema.
Pia tutaenda kushirikiana kwenye eneo la uchumi wa buluu, nishati ya umeme na gesi na ulinzi na usalama kwenye mipaka kukabiliana na uharamia.
Katika sekta ya kilimo wakuu hao wa nchi wamekubaliana wazo la kuhamasisha nchi nyingine zinazozalisha korosho kuanzisha umoja wao utakaoratibu biashara ya zao hilo.
Akizungumzia hilo, Rais Nyusi amesema uwepo wa umoja wa wazalishaji korosho utasaidia kuwa na sauti moja kwenye soko na kukabiliana na changamoto ya wanunuzi wakubwa wa zao hilo kujipangia bei.
“Miongoni mwa vitu vingi tulivyobarikiwa ni zao la korosho, ni muhimu tuwe na umoja utakaotufanya tuwe na sauti moja. Pia tuangalie namna gani tunaweza kuongeza thamani ya zao hili, tunahitaji tafiti ambazo zinaweza kutuonesha tija zaidi kwenye korosho,” amesema Rais Nyusi.
Eneo lingine alilosisitiza ni ushirikiano huo kuelekezwa katika maeneo ya vijijini ambayo ndiyo hasa yanahitaji huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji, umeme, afya na miundombinu bora.
Kuhusu usalama nchini kwake Nyusi amesema hali inaendelea kuimarika ikiwa ni matokeo ya kupata msaada kutoka katika mataifa mengine ya Afrika na kusisitiza kuwa siku zote Msumbiji itakuwa na shukurani jitihada hizo.
“Hali ya usalama inaendelea kuimarika na tunafahamu majirani zetu wamechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha hili amani imerejea Msumbiji. Tuna kila sababu ya kuimarisha uhusiano huu na vijana wa sasa wanapaswa kutambua wana jukumu katika kuhakikisha tunaendelea kuwa pamoja,” amesema Rais Nyusi.
Rais Nyusi aliwasili nchini jana Jumatatu Julai 1, kwa ziara ya siku nne kwa mualiko wa ziara ya kikazi kutoka kwa mwenyeji wake Rais Samia na kesho Jumatano, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonesho ya 48 Kimataifa ya Biashara Dar es salaam maarufu sabasaba.
Sambamba na matukio hayo, ujio wa Rais Nyusi nchini unalenga pia kuwaaga Watanzania kwa kuwa anakaribia kumaliza muhula wake wa pili wa urais katika nchi hiyo.
Rais Nyusi ameiongoza Msumbiji kwa miaka 10 hadi sasa na Oktoba 2024 taifa hilo linatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa kumpata Rais mpya.