Tanzania, Rwanda na Burundi zaanza kupata umeme wa Rusumo

Muktasari:

  • Hatimaye mataifa matatu ya Tanzania, Rwanda na Burundi yameanza kunufaika na mradi wa maporomoko ya umeme wa Rusumo wa megawati 80.

Dar es Salaam. Hatimaye mataifa matatu ya Tanzania, Rwanda na Burundi yameanza kunufaika na mradi wa maporomoko ya umeme wa Rusumo wa megawati 80.

Mradi huo unaotekelezwa kwa pamoja na nchi hizo umefikia asilimia 99.9 na unatarajia kuzinduliwa Machi mwaka 2024 huku kila nchi husika ikipata megawati 27 za umeme.

Mradi unahusisha ujenzi wa mtambo wa uzalishaji umeme, bwawa, eneo la kupokea umeme kabla haujasambazwa na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kutoka eneo la mradi hadi Nyakanazi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 18, 2023 jijini Mwanza wakati akiongoza kikao cha ngazi ya Mawaziri wa Nishati katika mataifa hayo.

"Tumeridhishwa na maendeleo mazuri ya mradi, tunawapongeza Bodi na watendaji kutoka kampuni ya umeme ya Rusumo na wakandarasi kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huu,” amesema Biteko ambaye ni Mwenyekiti wa Mawaziri wanaosimamia mradi huo.

Dk Biteko amesema mradi huo una umuhimu kwa nchi zote tatu zinazokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa uhakika wa umeme, hivyo mradi huo utaongeza uimara kwenye gridi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mafuta, Nishati na Migodi wa Burundi, Mhandisi Seleman Khamissi amesema  megawati 27 zitakazoanza kutumika nchini humo zitapunguza changamoto za upatikanaji umeme.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati Tanzania, mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha BENACO kitakachotoa umeme kutoka mradi huo na kuusafirisha kwa msongo wa KV 220 kwenda Kyaka mkoani Kagera ili mkoa huo upate umeme kutoka gridi ya Taifa badala ya Uganda.

Mradi huo ulianza kujengwa Mwaka 2017 kwa thamani ya mkopo wa Dola 340 milioni (Sh850 bilioni) za Benki ya Dunia na ulitarajiwa kukamilika mwaka 2020 lakini ulikwama kutokana na changamoto za Ugonjwa wa Uviko-19.

Kuhusu manufaa ya mradi huo kwa upande wa Tanzania, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga akizungumza na Mwananchi Digital amesema megawati 27 zitasaidia kupunguza ukali wa mgao wa umeme unaoendelea nchini kwa sasa.

Luoga amesema megawati hizo zitaingizwa zote katika gridi ya Taifa kupitia njia ya msongo wa kusafirisha umeme kutoka Rusumo-Nyakanazi. Amesema kiwango hicho kinaweza kuhudumia mikoa mitatu ya Simiyu, Lindi na Mtwara kwa pamoja.

“Pili, mradi huo unaendana na manufaa ya kijamii katika Wilaya ya Ngara itakayonufaika na ujenzi wa mradi wa maji unaohudumia wakazi wote wa wilaya yote, shule za Sekondari tano, shule msingi tatu, vituo vya afya viwili. Pia itaunganisha nchi hizo kwa kusudio la kuuziana umeme,” amesema Luoga.

“Kila megawati 27 inatumia mashine moja, mashine ziko tatu. Kwa sasa ziko mashine mbili, mashine moja itaingia Januari ili kila nchi ianze kutumia umeme wake kwa ukamilifu, kwa sasa tunafanya mgao wa matumizi ya megawati 27 kwa saa 12, leo Tanzania,kesho Rwanda na kesho kutwa Burundi,” ameongeza.